Ee! Mungu wangu!

EEE Mungu wangu! Hutaacha kusema hivyo ukifanikiwa kumuona Nezia Maregesi, mkazi wa Majita mkoani Mara ambaye ana uvimbe mguuni wenye zaidi ya kilo 50.

Flora Lauo anayerusha kipindi cha Frola Nitetee kwenye Runinga aliliambia UWAZI kuwa amemuibua mama huyo mwenye mateso ya ajabu hivi karibuni na kwamba yuko kwenye harakati za kumpeleka hospitali.

 

“Baada ya kuletewa habari za mama huyo nililazimika kusafiri hadi Mara, hali niliyomkuta nayo inasikitisha na kama unavyomuona kwenye picha,” alisema Flora alipozungumza na mwandishi wetu akiwa kama ‘sosi’ wa habari.

Akisimulia chanzo cha mguu wake kuvimba kiasi hicho, Nezia ambaye machozi hayamuishi machoni anapoeleza mkasa wake anasema:

“Miaka miwili na nusu nikiwa na ujauzito nilikuwa natoka kijijini kwetu kwenda kuwatembelea ndugu zangu kijiji jirani.

 

“Ghafla nikasikia kitu kama mwiba umenichoma mguuni, nilipoangalia sikuuona lakini nilikuwa nasikia maumiu makali, nikavua viatu kutazama vizuri sikuuona.

“Basi ikabidi niendelee na safari huku nikisikia maumivu, tangu hapo sijawahi kupona, mguu ukawa unavimba, maumivu nayo ndiyo usiseme.” Maelezo hayo yanayoacha mswalli mengi juu ya kutoonekana kwa mwiba, jeraha litokanalo na mtu kuchomwa na kitu chenye ncha kali aliyatoa Nezia huku akibubujikwa na machozi, yanahuzunisha.

 

Alisema, amehangaika kutafuta tiba hospitalini na kwa waganga wa kienyeji lakini hakuna nafuu inayopatina zaidi ya uvimbe kuongezeka hadi kufikia kiunoni na kuathiri sehemu zake za siri.

Mateso yamekuwa sehemu ya maisha ya Nezia huku akidai kukosa msaada wa kumnasua kwenye machungu ambapo amelazimika kurudi kwa mama yake mzazi akiwa na mwanaye.

“Wakati tatizo linatokea nilikuwa mjamzito kama nilivyokuambia baadaye nilijifungua, mwanangu ana miaka miwili.

 

“Sasa sijui ni kutokana na hali yangu kuwa hivi, mimi na mume wangu tuliachana,” alisema Nezia huku akifuta machozi na kuongeza.

“Kuna wakati namuomba Mungu bora anichukue labda naweza kwenda kupumzika lakini…,” kilio kinakatiza maelezo yake na kumlazimisha mwandishi ampe maneno ya faraja.

Kuhusu nini alichoambiwa na madaktari kuhusiana na tatizo lake, mwanamke huyo alisema hakuna ugonjwa uliogundulika.

 

Hata hivyo, Flora ambaye kwa sasa anasimamia uchunguzi wa afya ya Nezia amesema amewasiliana na madaktari katika Hospitali ya Bugando mkoani Mwanza kwa lengo la kumpeleka kufanyiwa vipimo.

“Sijafahamu gharama za matibabu zitakuwa ni shilingi ngapi kwa sababu hajapimwa kujua anawezaje kutibiwa,” alisema Flora.

Mtu ambaye ataguswa na tatizo hili anaweza kuwasiliana na Flora Nitetee kwa namba za simu 0759 665 555.

STORI: MWANDISHI WETU, UWAZI

Loading...

Toa comment