The House of Favourite Newspapers

Eid Mubaraka! Nakukumbusha Kufanya Haya Sikukuu Hii!

 ASSALAM aleikum! Nianze kwa kuwaambia wasomaji wangu wote popote mlipo; EID MUBARAK! Mungu awajaalie kila la heri, msherehekee sikukuu hii kwa furaha na amani.

Lakini sasa, kama ambavyo tumeamrishwa kukumbusha katika yaliyo mema, leo nataka kuzungumza na Waislamu ambao wamekuwa kwenye mfungo na sasa wanaingia kwenye kusherehekea Sikukuu ya Idd. Hapo ulipo sema ALHAMDULILLAH!

 

Ndugu zangu, kuna watu huko mtaani ambao hunishangaza sana inapofikia sikukuu hii na nyingine za kidini. Hawa ni wale wanaotumia siku hiyo kufanya matukio mabaya, kumuasi Mungu kwa kufanya maovu. Hili si jambo zuri hata kidogo.

 

Hebu tafakari, ni wangapi ambao walitamani sana kuiona siku ya leo wakiwa wazima lakini hawapo duniani? Leo hii wewe umejaaliwa neema hiyo halafu unataka kumkasirisha Mungu kwa kufanya yale aliyoyakataza, huku ni kumbipu Mungu na nakuhakikishia atakupigia!

Ifike wakati tuwe ni watu wenye kushukuru kwa neema anatupatia Mungu. Hata hivyo katika kukumbushana leo nimeona niwaletee yale ambayo unastahili kuyafanya katika kusherehekea sikukuu hii ya Idd.

 

USISAHAU IBADA

Siyo sawa mtu kusali siku ya Idd tu lakini kama umeshindwa kusali siku zote zilizopita, siku ya Idd hakikisha unahudhuria msikitini na kutekeleza ibada hiyo muhimu sana. Hakikisha kila unachokifanya siku hiyo kinakuwa ni sehemu ya ibada.

 

SAIDIA WASIOJIWEZA

Katika sikukuu kama hizi itakuwa haileti picha nzuri kama wewe utakuwa unakula pilau, kuku na juisi lakini jirani yako hajui atakula nini.

Hivyo basi kutokana na uwezo wako, saidia wale wasiojiweza chakula, fedha na hata nguo ili nao wafurahie sikukuu hiyo kama wengine.

 

IWE SIKU YA FURAHA

Hakikisha familia yako yote pamoja na ndugu zako wanaifurahia siku hii. Wanunulie nguo mpya wale wanaokutegemea, kipikwe chakula kizuri. Kwa wale walio mijini, kama ndugu zako wako kijini, usiwasahau! Hakikisha nao wanafurahi.

 

JUMUIKA NA WENZAKO

Waalike marafiki na hata ndugu zako ili msherehekee pamoja. Hii ina raha yake, ni tofauti na kusherehekea wewe na wanao tu.

SEHEMU ZA KWENDA

Endapo mtafikiria kwenda ‘out’, ni vyema mkajiweka mbali na zile sehemu zilizokubuhu ufuska kama vile klabu, baa au kwenye fukwe ambazo watu huvaa nusu uchi na kujipitisha mbele za watu.

USITUMIA OVYO PESA

Kwa nini utumie pesa zako ovyo tena wakati mwingine kwenye mambo ya anasa? Umakini katika kila shilingi yako unatakiwa kila siku. Kumbuka siku za sikukuu si za kutumbua pesa.

KUMBUKA WAZAZI WAKO

Wapo ambao wako mijini na wazazi wao wako vijijini, lakini kila sikukuu wao hutuma tu vitu na pesa lakini hawaoni umuhimu wa kwenda kufurahi na wazazi wao. Kama una nafasi, sikukuu kama hizi zinanoga sana kula na wazazi.

USISAHAU KUTOA SADAKA

Siku hizi itakuwa jambo jema kama utazitumia ukiwa kwenye nyumba za ibada lakini pia sadaka inatakiwa kutolewa kwa kiwango cha ziada.

USIMUASI MUNGU

Wapo ambao wanaweza kujizuia kunywa pombe siku zote lakini siku za sikukuu lazima waonje. Kuna ambao siku za sikukuu wanazini sana. Haya ni mambo yanayomkera Mungu hivyo jiepushe nayo.

USALAMA WA KIFAMILIA

Itakuwa si jambo jema watu walio nyuma yako kutoka nyumbani na kwenda kusikojulikana. Watoto wakitoka kwenda matembezini wawe chini ya uangalizi. Epuka kuwaachia waende sehemu kama vile ufukweni, maeneo yenye magari mengi na sehemu za mbali.

Hii ni kwa sababu siku za sikukuu matukio ya watoto kupotea, kugongwa na gari, kufa maji na mengineyo hutokeo. Kwa maana hiyo ni vyema ulinzi wa familia ukaongezeka ili siku ipite salama.

HILI LA MAVAZI

Imekuwa ni kawaida yetu kununua nguo mpya za sikukuu. Niwakumbushe tu kwamba, hakikisha wanao na hata nyie wazazi mnavaa nguo zenye kusitiri miili yenu. Kumbukeni kwamba, hata kuvaa kwa stara ni sehemu ya ibada na endapo utavaa nguo zinazoacha wazi sehemu muhimu za mwili wako utakuwa unapata dhambi.

Ni hayo tu kwa leo, niwatakie sikukuu njema ndugu zangu!

Comments are closed.