The House of Favourite Newspapers

ELEWA JINSI YA KUEPUKA KIFAFA CHA MIMBA (ECLAMPSIA)

Mjamzito aliyepata kifafa cha mimba kwenye ujauzito uliopita, ana uwezekano mkubwa wa kupata tena. Imegundulika kuwa iwapo mwanamke anazaa na mwanaume mwingine tofauti na aliyezaa naye awali, uwezekano wa kupata kifafa cha mimba huongezeka.  Ujauzito kwa mwanamke mwenye umri zaidi ya miaka 40 huongeza uwezekano wa kupata kifafa cha mimba. Ingawa hakuna kinga ya uhakika ya kifafa cha mimba, wanawake walio kwenye makundi hayo yaliyotajwa hapo juu kuwa na uwezekano mkubwa wa kupata ugonjwa huu wanaweza kujikinga kwa kutumia vidonge vya aspirin na madini ya calcium.

Kabla ya kutumia dawa hizi ni muhimu kupata ushauri wa kitaalam wa daktari. Tiba pekee ya kifafa cha mimba ni kumzalisha mjamzito. Hii ni kwa sababu ugonjwa huu husababishwa na kuwepo kwa kondo la nyumba ndani ya kifuko cha uzazi. Bila kutoa kondo la nyumba mgonjwa hawezi kupona. Iwapo ugonjwa huu utagundulika kabla mtoto hajakomaa na kuwa tayari kwa kuzalishwa Daktari anaweza kushauri mjamzito alazwe na kuangaliwa kwa ukaribu wakati ikisubiriwa kukomaa kwa mtoto.

Vilevile daktari anaweza kushauri mjamzito apewe dawa ya kuharakisha kukomaa mapafu ya mtoto. Iwapo hali ya mjamzito ikibadilika na kuwa mbaya, kumzalisha huweza kuwa ni lazima hata kama mtoto hajakomaa kwa sababu kuna hatari kubwa ya mama na mtoto kuathirika iwapo ujauzito utaendelea. Mojawapo ya hatari inayoweza kutokea iwapo ujauzito utaachwa kuendelea ni mtoto kufia tumboni,

kupoteza fahamu kwa mjamzito na kupata dalili za “degedege“, damu kupoteza uwezo wa kuganda na kusababisha mjamzito kupoteza damu nyingi, damu kuganda mwilini na kuziba mishipa, kondo la nyumba kujitenga na kifuko cha uzazi kabla ya mtoto kuzaliwa, figo za mjamzito kushindwa kabisa kufanya kazi, mjamzito kupata kiharusi (stroke) au mjamzito kupoteza maisha.

Kwenye kumzalisha mama mwenye kifafa cha mimba, njia mbalimbali huweza kutumika kutegemeana na hali ya mjamzito. Kama hali sio mbaya sana na njia ya uzazi imeshaanza kufunguka, mjamzito anaweza kupewa dawa za kuanzisha uchungu na kujifungua kwa njia ya kawaida. Kujifungua kwa njia ya operesheni hulazimika kwa wajawazito wenye msukumo mkubwa sana wa damu na wale ambao hali zao sio nzuri au kunapokuwepo na sababu nyingine ya kujifungua kwa operesheni.

Kabla ya kujifungua, mjamzito mwenye msukumo mkubwa wa damu (High blood pressure) hupewa dawa za kupunguza msukumo wa damu. Ili kuzuia uwezekano wa kupata degedege, daktari anaweza kushauri mgonjwa apewe madini ya magnesium kwa njia ya dripu.

Kwa sababu ugonjwa wa kifafa cha mimba huongeza uwezekano wa damu kuganda mwilini, daktari anaweza kushauri mgonjwa atumie dawa ya kuzuia damu kuganda. Baada ya kujifungua, msukumo wa damu unategemewa kurudi kwenye hali yake ya kawaida katika muda wa saa 24. Hata hivyo, ni vizuri mama aliyejifungua katika hali hii kuangaliwa kwa saa 48 kabla hajaruhusiwa kwenda nyumbani. Hii hutegemea na uwepo na nafasi ya kulaza wagonjwa kwenye hospitali.

USHAURI

Kwa vile upo uwezekano wa msukumo wa damu kuendelea kuwa juu moja kwa moja. Mzazi hushauriwa kupima msukumo wa damu mara kwa mara, iwapo baada ya wiki sita (siku 40) itaonekana msukumo wa damu unaendelea kuwa juu, basi hushauriwa kuendelea na matibabu ya msukumo mkubwa wa damu kama wagonjwa wengine wenye ugonjwa wa msukumo mkubwa wa damu.

Comments are closed.