The House of Favourite Newspapers

Elewa sababu za mtu kukojoa damu (Haematuria)

UGONJWA wa kukojoa damu ambapo kwenye mkojo kunakuwa na chembechembe za damu nyekundu (red blood cells), kitaalam huitwa haematuria.  Kukojoa damu ni dalili ya kuonesha kuwa mtu huyo anayekojoa damu ana magonjwa katika mfumo wake wa mkojo kama vile magonjwa ya kichocho au magonjwa mengine yanayoshambulia kibofu cha mkojo au kwenye figo, jambo ambalo ni hatari kwa anayeugua.

SABABU

Magonjwa yanayoshambulia mfumo wa mkojo kama vile U.T.I, magonjwa ya zinaa hasa kwa wanawake, vijidudu kama staphylococcus saprophyticus, mawe kwenye figo (kidney stone) kuvimba kwa tezi zinazozalisha manii kwa wanaume ambao umri ni mkubwa; yaani wazee hukumbwa na tatizo hili.

Sababu nyingine ni kama kupata ajali na kuumia sehemu za mfumo wa mkojo (trauma), kupata magonjwa kama kansa ya kibofu cha mkojo, hii hutokea mara nyingi hasa vijijini ambapo watu wanacheza au kuogelea kwenye madimbwi ya maji yaliyotuama (yasiyotembea).

Sababu zingine ni mtu kuugua magonjwa ya upungufu wa damu mwilini maarufu kama sickle cell anemia na magonjwa mengine ya figo kama vile nephotic syndrome na mengine mengi ambayo yanajulikana kwa kitaalam na siyo rahisi kuyafafanua kwa Kiswahili. Ni vema kumuona mtaalam wa afya uonapo mkojo wako una damu ili aweze kujua sababu na kukupa dawa za kukutibu.

AINA YA UGONJWA WA KUKOJOA DAMU

Kuna aina mbili za damu kutoka kwenye mkojo. Moja ni ile ambayo damu huchuruzika na kuonekana vizuri kwenye mkojo. Hii hujulikana kitaalam kama macroscopic haematuria au gross haematuria ambayo hutokea kwa wagonjwa wa kichocho au waliopata ajali zinazodhuru kibofu.

Aina nyingine ya kutoka damu kwenye mkojo ni ile inayoonekana kwa mbali na mara nyingine huonekana wakati mgonjwa anapopimwa mkojo, aina hii kitaalam hujulikana kama microscopic haematuria.

JINSI YA KUGUNDUA TATIZO

Mara nyingi tatizo la kukojoa damu hugundulika baada ya mgonjwa kwenda hospitalini na kuonana na wataalam wa afya kuchunguza afya zao na akachukua maelezo yake vizuri na kuagiza mgonjwa akapime mkojo ili kugundua tatizo.

Kipimo cha ultrasound husaidia kujua tatizo linalosababisha mgonjwa akojoe damu. Lakini pia mashine ya X-Ray husaidia kugundua kama mgonjwa ana mawe kwenye figo ambayo nayo husababisha mkojo kuchanganyika na damu. Kipimo kingine cha kisasa kinachogundua tatizo la mtu kukojoa damu ni CT-Scan, hiki kina uhakika ila ni kipimo ghali sana na hupatikana kwenye hospitali kubwakubwa tu nchini.

TIBA NA USHAURI

Tiba ya uhakika hupatikana baada ya kujua sababu inayosababisha mgonjwa akojoe damu, hiyo hugundulika baada ya vipimo kama vile mtu kuwa na kichocho.Mgonjwa akigundulika kuwa na maradhi hayo ya kichocho, basi atapewa dawa na kama ni maambukizi ya njia ya mkojo kama vile U.T.I mgonjwa atapewa dawa husika na mtaalam.

Ikiwa mgonjwa anakojoa damu kutokana na kuwa na magonjwa ya zinaa nayo yatatibiwa ama kwa vidonge au kwa sindano. Yapo magonjwa mengine yanayosababisha mgonjwa kukojoa damu kama vile yale ya figo, basi nayo akipimwa yakigundulika kuwa tatizo ni hilo, atatibiwa na atapona kabisa.

Ushauri muhimu ni kwamba watoto wasichezee maji yaliyotuama (yaliyosimama) hasa kwenye mabwawa vijijini na mijini, wakigundulika kuwa walicheza; basi haraka wapelekwe hospitalini kupimwa mkojo ili kama wamepata maambukizi, atibiwe kabla hali haijawa mbaya.

Comments are closed.