Elfu 2 Yaua Vijana Wawili

KUNA watu hudharau fedha kwa kusema: “Shilingi elfu mbili kitu gani?” Lakini ni kiasi hichohicho ndicho kilichosababisha vijana wawili wapoteze maisha.

Waliofariki dunia katika tukio lililowasikitisha watu ni Ibrahimu Hashim ‘16’ na Innocent Paschal ‘20’, wakazi wa Majohe nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

 

HABARI KAMILI

Chanzo cha habari kinaeleza kuwa, Jumapili ya wiki iliyopita majira ya saa moja jioni vijana hao wawili walihitilafiana kutokana na kudaiana kiasi hicho cha fedha.

Ibrahim ‘Ibra’ ndiye aliyekuwa akimdai Innocent ‘Inno’ ambapo siku ya tukio kijana huyo alimshinikiza mdeni wake amlipe fedha zake bila kukosa.

“Inno alimwambia Ibra kuwa siku hiyo hakuwa na fedha lakini alimwambia kuwa atamlipa siku inayofuata, Ibra hakukubali.

 

“Basi ikatokea hali ya kutofautina,” chanzo kilichoomba jina kuhifadhiwa kililiambia Risasi Jumamosi na kuongeza kuwa purukushani kati ya vijana hao zilimfanya Ibra achukue kisu na kutaka kumchoma Inno.

Inaelezwa kwamba baada ya Inno kuona hayuko salama alilazimika kutimua mbio kupisha shari lakini Ibra alianza kumfukuza huku akiwa na kisu mkononi.

 

IBRA AUAWA

Pamoja na kwamba Ibra ndiye aliyekuwa anamkimbia Inno lakini taarifa zilizokuja baada ya muda mfupi ni kwamba; Ibra ameuawa kwa kuchomwa visu.”

Udadisi wa kiuandishi unaweza kutoa picha ya eneo la tukio ambako kilipata chanzo cha kusimulia ilivyokuwa; kwamba huwenda kutokana na Ibra kuwa mdogo kiumri alizidiwa nguvu na Inno na kufanikiwa kumpokonya kisu kisha kumuua kwa kumchoma nacho mwilini.

 

MSIKIE BABA WA IBRA

“Ilikuwa mida ya saa mbili hivi usiku, nikiwa nimekaa ndani na mke wangu, ghafla akaja kijana mmoja akiwa anakimbia huku akiwa na damu mwilini, akaniambia, ‘baba Ibra twende mtoto wako amechomwa kisu yupo chini.’

“Tulipofika eneo la tukio nikamkuta mwanangu amelala chini huku akitokwa na damu nyingi, nikamgeuza nikiamini huwenda bado mzima,” alisema Hashim Dando, baba yake Ibra.

Hata hivyo, fikra za Dando kwa mwanaye hazikuwa sahihi kwa sababu baada ya kumgeuza mwanaye aligundua kuwa tayari kijana wake alikuwa amegeuka jina na kuitwa marehemu.

 

INNO ASAKWA

Baada ya kugundua uwepo wa mauaji hayo taarifa ilitumwa polisi ambapo askari walifika kwa wakati eneo la tukio na kuanza kumsaka mtuhumiwa.

Hata hivyo, wakati polisi wakiwa na mwili wa marehemu kwenye gari kuelekea hospitali kwa ajili ya kuuhifadhi na kuuchunguza, taarifa ziliwafikia kuwa mtuhumiwa amepatikana.

Bila shaka taarifa hiyo ilikuwa jema kwao, hivyo kuamua kugeuza gari ili wamchukue Inno na kuondoka naye kwa ajili ya mahojiano jambo ambalo halikufanyika sawa na matakwa yao.

 

SIKIA SIMULIZI YA BIBI WA INNO

Bibi wa Inno, Esther Emmanuel alipotafutwa na mwandishi wetu ili asimulie kilichomtokea mjukuu wake siku ya tukio alisema:

“Nakumbuka ilikuwa siku ya Jumapili saa sita usiku, mimi na familia yangu wote tulikuwa tumelala na Inno alikuwemo ndani.

“Ghafla wakaja watu na kuanza kugonga mlango kwa nguvu huku wakipiga kelele kuwa wanahitaji tufungue mlango, walikuwa wanarusha mawe na mchanga ndani.

 

“Basi ikabidi tuamshane, wote tukatoka vyumbani tukakaa sebuleni, muda huo wote wale watu wakawa wanaendelea tu kugonga mlango kwa fujo, sasa shangazi yake Inno akawauliza nyie ni akina nani? Na kama mnataka tuwafungulie mlango kwa nini mmekuja peke yenu? Kwa nini msingekuja na viongozi wa serikali ya mtaa ili na sisi tuwaamini?

“Baada ya kusema hivyo mmoja akajibu akasema ‘mimi ni askari,’ tukamwambia tupe kitambulisho, akatoa kupitia dirishani, basi yule shangazi wa marehemu akakiangalia akamrudishia.

 

“Ila wakati wote huo tunaongea tulikuwa bado hatujafungua mlango, wakaendelea kulazimisha tufungue mlango, sisi tukawakatalia.

“Wakatuambia kama hamtaki kufungua basi sisi tunabomoa na kweli wakabomoa mlango na kufanikiwa kungia ndani kuendesha msako wa kumnasa Inno.

 

INNO AJARIBU KUTOROKA, ANASWA

“Basi walipoingia wakaanza kumtafuta Inno, kumbe Inno alikuwa amesikia kelele hizo ikabidi aende akajifiche chumbani kwangu (kwa bibi).”

Hata hivyo, maficho hayo hayakuweza kumsaidia Inno kwani kundi hilo la watu lilifanikiwa kumfikia nakuondoka naye huku likimshambua kwa kumpiga na vitu mbalimbali.

 

INNO NAYE AUAWA

Katika hali mbayo ni ya kusikitisha watu hao ambao awali walidai kuwa waliambatana na polisi katika kumnasa Inno, walimchukua kijana huyo hadi kule yalikotokea mauaji wa Ibra ambako walizidisha kipigo na kumfanya Inno aishiwe nguvu.

 

Akiwa katika hali ya kupigania roho yake, Inno alijaribu mara kadhaa kuomba watu wasimhukumu lakini hakusikilizwa, ndiyo kwanza kipigo cha kutumia mawe na fimbo na ngumi kilizidi kumzidia.

Mwisho wa yote kijana huyo alisalimu amri kwa kuirejesha roho yake kwa Mungu na kuwa tayari kuingia mavumbini alikotokea jambo ambalo liliwafanya polisi waliokuwa wamerudi kumchukua mtuhumiwa kulazimika kuondoka na maiti za vijana wawili waliopoteza maisha kutokana na kisa cha shilingi elfu mbili.

 

MSIKIE MJUMBE

Naye mjumbe wa eneo hilo, Ally Muruma, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kwamba amehuzunishwa sana kwani Ibra alikuwa mtoto mwema na mwenye heshima.

“ Nilipata taarifa za kifo cha Ibra asubuhi nikiwa nyumbani kwangu nimesikitika.”

 

VIFO VYAACHA SIMANZI

Gazeti hili lilifanikiwa kuhudhuria misiba yote miwili ambapo lilishuhudia wananchi wengi wa eneo hilo wakiwa na simanzi huku kila mtu akisimulia namna vijana hao walivyoishi mtaani hapo.

“Vijana wote walikuwa wema tu, Ibra alikuwa fundi makenika na Inno alikuwa akifanya biashara ndogondogo,” alisema mkazi mmoja wa eneo hilo ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini.

 STORI: Memorise Richard, Risasi Jumamosi

Loading...

Toa comment