The House of Favourite Newspapers

ENEO HATARI UPORAJI BAJAJ LATIKISA

HUWEZI kuamini, eneo la Msasani Bonde la Mpunga ambalo ni makazi ya watu wenye nazo kutokana na hali inayojidhihirisha ya uwepo wa majengo ya kifahari, limegubikwa na matukio ya uhalifu wa uporaji wa Bajaj.

 

Kufuatia kukithiri kwa matukio hayo hivi karibuni raia wema wa eneo hilo walifika kwenye ofisi za gazeti hili, Sinza Mori jijini Dar na kuelezea kilio hicho wakisema kwa sasa wanaishi roho mkononi kufuatia matukio hayo. Mmoja wa raia hao aliyeomba hifadhi ya jina lake alisema majambazi hao wamekuwa wakifanya uhalifu huo hadharani hali ambayo wanaihofia kuwa baada ya uporaji wa Bajaj watawaingilia ndani na kuwadhuru kwa kuwa wameshabaini kuwa eneo hilo wanaweza kufanya lolote bila kupata upinzani wowote.

 

Kufuatia hali hiyo, mwandishi wa gazeti hili alifunga safari mpaka eneo hilo na kuonana na mjumbe wa nyumba 50 aliyejitambulisha kwa jina la Mateo Makange (Pichani) ambaye alithibitisha kukithiri kwa matukio hayo mtaani hapo ambapo alisema kwa mwezi mmoja wameshuhudia matukio hayo zaidi ya sita. “Yaani hapa kwa mwezi tunashuhudia matukio hayo zaidi ya sita, waendesha Bajaj wanakodiwa huko wanakotoka wanaletwa eneo hilo kwa ajili ya kukabwa na kunyang’anywa vyombo vyao vya moto.

“Hivi tunavyoongea usiku wa kuamkia jana kuna jamaa amekabwa paleee… na kuporwa Bajaj mwingine hivi juzijuzi naye ameibiwa hapa chini unapopaona na michubuko ya lami siku hiyo ya sakata ndiyo hii unayoiona hata bado haijafutika vizuri,” alisema mjumbe huyo huku akimuonesha mwandishi wetu maeneo hayo.

 

Kuhusu usalama wa eneo hilo mjumbe huyo amesema amekuwa akishirikiana na mjumbe mwenzake aliyemtaja kwa jina moja la Khadija na wamekuwa wakiyaripoti matukio hayo polisi lakini haoni jitihada zozote zinazofanywa kukomesha matukio hayo.

 

Kufuatia matukio hayo, mwandishi wetu alimtafuta kwa njia simu Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Kamishna Msaidizi, Jumanne Muliro ambaye alitoa wito kwa kiongozi huyo wa eneo hilo na waathirika wa uvamizi huo kwenda kuripoti polisi. “Mimi ndiye mwenye takwimu za matukio, hivyo hilo tukio la juzijuzi sina taarifa nalo, kila mtu anayeona kuna uhalifu asiishie kulalamika huko mitaani, aende kituo cha polisi ili tufanyie kazi,” alisema Kamanda Muliro

 

STORI: RICHARD BUKOS, DAR

Comments are closed.