The House of Favourite Newspapers

Eng. Hersi: Mjadala Ulioanzishwa Kuhusu Udhamini ni Siasa Chafu

0

MKURUGENZI wa Uwekezaji wa GSM na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Eng. Hersi Said amesema mjadala ulioanzishwa na baadhi ya wachambuzi kuhusu udhamini wa kampuni ya GSM kwa vilabu mbalimbali ligi kuu ni siasa chafu kwa kuwa sio jambo geni katika ulimwengu wa soka.

 

Akizungumza na EA Radio, Injinia Hersi amesema yapo makampuni makubwa duniani ambayo yanadhamini klabu nyingi tu na hakujawahi kuwa na mjadala wowote.

 

“Watu wanaleta siasa chafu na mimi nasema hizi ni takataka. Mbona kampuni kama Emirates inadhamini vilabu vingi tu vinacheza ‘Champions League’. Ina maana Arsenal wakicheza na AC Milan utasema mmoja amwachie mwenzake?,” alihoji Eng. Hersi.

 

Aidha, Hersi amesema wao katika klabu ya Yanga wanasaidia tu, timu inaongozwa kwa kufuata misingi na taratibu za klabu yenyewe na sio kufuata matakwa ya GSM.

 

“Yanga inalipa mishahara yenyewe, ina mifumo yake ya kuajiri watu sisi tunasaidia tu. Yanga ni timu kubwa huwezi kufananisha na hawa makolo. Huwezi kumleta mchezaji kama Bangala halafu hajui mshahara analipwa na nani..

 

“Hii ni klabu kubwa, tunafanya kazi ya kurejesha heshima yake, watu waipende tena. Angalia mechi ya juzi Yanga inafungwa goli mashabiki wanapiga makofi, tunarudisha tunafunga la pili na la tatu na bado kuna dakika kama 900 za kucheza,” aliongeza Hersi.

 

Hersi pia aligusia mfumo wa uwekezaji ambao klabu ya Yanga imeamua kufuata baada ya kushauriwa na La Liga akiamini unakwenda kuinufaisha klabu hiyo.

 

“Tumechagua mfumo wa wanachama na wawekezaji kwa 51% kwa wanachama na 49% kwa wawekezaji. Hili tumejifunza La Liga na ndio maana unaweza ukaona kwanini Real Madrid na Barcelona zinapendwa na watu duniani.

 

“Tumejifunza kitu kikubwa sana na mabadiliko ya Yanga yatakwenda kuwa ya mfano. Timu hizi zinajiendesha kwa hasara kwa miaka mingi ndio maana zimekwama. Ukisema hivi mtu anaweza asikuelewe lakini ukitazama mapato ya klabu na matumizi ndio utajua kwanini zinajiendesha kwa hasara,” amesema Hersi.

Leave A Reply