Erasto Nyoni: Waarabu wanaacha pointi Dar

KIRAKA wa Simba, Erasto Nyoni, amefunguka kuwa ana imani kubwa kwamba watawachapa wapinzani wao Waarabu, Al Ahly na wataacha pointi watakapocheza nao kesho Jumanne.

Kiraka huyo ambaye leo Jumatatu anaanza rasmi mazoezi na wenzake baada ya kutoka kipindi cha majeruhi, kesho Jumanne atawashuhudia wenzake wakipambana na Al Ahly katika Ligi ya Mabingwa Afrika.

Mechi hiyo ambayo itapigwa katika Dimba la Taifa jijini Dar, itakuwa ya pili baada ya ile ya kwanza ambayo ilipigwa nchini Misri na Simba kupoteza.

Nyoni ameliambia Championi Jumatatu kuwa anaamini kwamba watafanya vizuri mbele ya wapinzani wao hao na kupata matokeo baada ya wao kujifunza kutokana na makosa ambayo waliyafanya kwenye mechi ya kwanza.

“Ile mechi ya kwanza tulifanya makosa baadhi na ndiyo maana wenzetu wakapata ule ushindi ambao wameupata lakini safari hii nadhani mambo yatakuwa tofauti kwetu.

“Tumejifunza kwa kile ambacho kilitokea na walimu wamelifanyia kazi hilo, ninaamini kabisa kwenye mechi hii kwa sababu tuko nyumbani basi tutapata matokeo mazuri, kikubwa mashabiki wetu wasikate tamaa, bali waje kutusapoti kwa nguvu,” alisema Erasto.

Toa comment