The House of Favourite Newspapers

Eric Shigongo: Dimbwi la Damu-02

Ndege British Airways kutoka London ilitua katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Dar es Salaam saa kumi na moja jioni na abiria wote waliteremka na kuanza kutembea kuelekea nje ya uwanja ambako wenyeji wao waliwasubiri.
“Hoyce ulisema unaishi wapi kweli?”
“Naishi Masaki ambako kuna nyumba yetu ila wazazi wangu wanaishi Himo, Marangu Moshi!”
“Kwa hiyo kuna watu watakuja kukupokea siyo?”
‘Nafikiri hivyo kwa sababu wana taarifa za ujio wangu!”

“Sawa lakini kama ukitaka kuwasiliana na mimi utanipigia simu kwa namba zilizoandikwa kwenye kadi hii! Mungu akubariki sana Hoyce ahsante kwa kampani yako nzuri, nimefurahi sana kusafiri na wewe!”
Hoyce hakujibu kitu macho yake yalikuwa bado yapo juu ya kadi aliyopewa, alionekana kutoamini alichokisoma katika kadi hiyo! Alianza kurudia tena na tena kuisoma kadi hiyo Martin akiwa amesimama pembeni yake.

“Managing Director,
Martin Assets Limited! Martin Tours Limited, Martin Transporters Limited, Tanzamine Limited, Martin pipelines limited. Zote hizi ni kampuni zake?” Alisoma na kujiuliza Hoyce.
Aliponyanyua macho kumwangalia Martin alikuta vijana kama watano hivi wakinyanyua mabegi yake yote na mwingine akichukua koti lililokuwa mkononi mwa Martin, aliyekuja mwisho alikuja na mwavuli akaufungua na kumfunika Martin kwa juu ili asichomwe na jua! Yote haya yalimshangaza Hoyce, alishindwa kuamini kama mtu aliyekwenda Uingereza kutafutiwa kazi angeweza kupokelewa namna hiyo.

Alibaki mdomo wazi bila kupata jibu la maswali yaliyoendelea kichwani mwake! Aligundua waziwazi kuwa alikuwa amedanganywa na Martin! Baada ya fikra za muda wa dakika mbili alimkumbuka Martin, alishasikia habari akiwa nchini Uingereza, watu walimwongelea kama Mtanzania kijana aliyepata mafanikio.
Mara nyingi sana aliitembelea tovuti yake na kuona shughuli alizozifanya kijana huyo, kweli alikuwa ni kijana mdogo mwenye mafanikio makubwa! Lakini Hoyce hakuwahi hata siku moja kufikiri angeweza kukutana naye ana kwa ana na hata kuongea naye.
“Hivi kweli wewe ndiye Martin?” aliuliza Hoyce akionyesha kutoamini.
“Hapana Martin ni kaka yangu!” alificha.
“Siyo kweli ni wewe acha utani basi!” alisema Hoyce huku akionyesha msisitizo.
“Ok! Ni mimi!”

“Sasa kwanini ulinificha tangu tuondoke London?”
“Kwa sababu huwa sipendi sana kujulikana!”
“Mh!” Hoyce aliguna.
“Ahsante Hoyce kwa kusafiri na mimi tafadhali nipigie simu!” alisema Martin na baadaye kuanza kutembea kuelekea mahali gari lililokuja kumpokea lilipoegeshwa, mlango ulifunguliwa na kijana mwingine na Martin aliingia ndani bila kugusa mahali popote, Hoyce alibaki akishangaa! Alishindwa kuelewa Martin alikuwa kijana wa aina gani kwani kwa kijana wa kawaida lazima angetamba na kujisifu kwa mali alizonazo ili kumshawishi yeye amkubali kimapenzi.

Martin aliishi Arusha hivyo baada ya kupokelewa kwa gari lake mwenyewe alisafiri kwa muda wa masaa matano na kuingia mjini Arusha usiku, katika muda huo tayari alishapokea simu za Hoyce kumi na tano! Kwa vitendo hivyo tayari alishaelewa kuwa mtoto alishaanza kupagawa kama ilivyokuwa kawaida ya Martin kuwapagawisha watoto wa watu.

“Watoto wa kike bwana yaani tayari keshalewa penzi! Wakati aliniambia anampenda sana mpenzi wake wa Uingereza, hawa viumbe ni dhaifu sana, nafikiri mtoto mwenyewe hajatulia!” Aliwaza Martin akimsagia Hoyce.
Hivyo ndivyo walivyoanza na mawasiliano kati yao hayakukomea siku hiyo kwani baadaye yaligeuka kuwa penzi zito lililopelekea wao kufunga ndoa miezi sita tu baada ya kukutana na kuwa mke na mume! Richard Ford alipokuja nchini kumtembelea Hoyce alikuta tayari amekwishaolewa alilia machozi kwa uchungu na kuahidi kulipa kisasi.

“I will kill them in a bad accident let me go back home once I come back they will know my name!”(Nitawaua katika ajali mbaya sana, acha nirudi nyumbani nikirudi watalijua jina langu!) alisema Richard kwa hasira akiwa amedhamiria kuua.
****
Mwaka mmoja baada ya ndoa yao walijaliwa kupata watoto wawili mapacha wa kike aliitwa Victoria na wa kiume aliitwa Nicholaus! Walikuwa watoto wazuri sana waliowaunganisha Hoyce na Martin zaidi, waliishi maeneo ya Uzunguni mjini Arusha na biashara za Martin zilizidi kukua, safari zake za nje ya nchi ziliongezeka maradufu mpaka akalazimika kuwa na ofisi katika nchi za Uswiss, Ufaransa na Ubeligiji, ambako aliajiri Wazungu kumfanyia kazi kama wawakilishi waliopokea madini yake na kuyauza.

****************

Sikukuu ya miaka 5 ya kuzaliwa Nicholaus na Victoria:
Siku hiyo ya jumapili Agosti 16, ilikuwa ni kati ya siku nne ambazo Martin alikuwa nchini Tanzania kupumzika na familia yake, akiwa nchini nchini ilikuwa ni lazima afanye tafrija yoyote na familia yake!Siku hiyo ilikuwa ni siku ya sikukuu ya kuzaliwa kwao! Watu wengi walifurika nyumbani kwao kusherehekea sikukuu hiyo.
“Mama wawili bado kitu gani au kila kitu kimekamilika?”
‘Kila kitu tayari ila bado keki tu!”
“Sasa tufanyaje?”
“Labda tuifuate pale best bites niliweka oda yangu na nikalipia nusu, wale ni mabigwa wa kutengeneza keki hapa Arusha!”
“Basi wewe baki mimi niende nikaichukue!”
“Hapana bwana twende wote!”
“Wewe baki tu!”

“Bwanae sitaki au una mipango yako nini?”
“Siyo hivyo nataka ubaki na watoto bwana!”
‘Sitaki bwana hebu twende wote na mimi nikalishe macho kila siku ndani!” Alizidi kung’ang’aniza Hoyce.
“Ok! Twende si umeng’ang’ania, tatizo lako mke wangu huniamni sijui kwanini?” Alisema Martin kwa utani.
“Siyo hivyo lakini kuna ubaya gani mtu akichunga mali zake?”
“Panda twende basi mpenzi!”
Wote walipanda garini lakini kabla gari halijaondoka Vicky alilikimbilia gari hilo!
“Mom!Mom! where are you going?”(Mama! Mama! Mnakwenda wapi?)
“To the best bites for your birthday cake!”(Tunakwenda best bite kufuata keki yenu ya siku ya kuzaliwa)
“Can I come with you mom?(Niwafuate mama?) Aliuliza Vicky.
“Ok! Get into the car!”(Haya panda basi garini) alisema Hoyce na Vicky alipanda bila kuchelewa Nicky hakutaka kuondoka aliendelea kucheza mpira na rafiki zake.

Hoyce alimwita Nicky kabla gari halijaondoka na mtoto aliondoka mbio.
“We are going downtown, take care of everything and make sure every friend of yours has a glass of juice Ok? We wont delay coming back!”(Tunakwenda mjini tafadhali angalia kila kitu nyumbani na hakikasha rafiki zako unawapa juisi ya kutosha sawa? Tutarudi sasa hivi!) Hoyce alimwambia Nicholaus akiwa na uhakika angerudi.
“Niiiicky!” Vicky alimwita kaka yake akatoa mkono wake wa kulia nje na kumpungia.
“Yoooo!” Nicholaus aliitika.

“See you later! I will sing happy birthday to you ok?”(Tutaonana baadaye nitakuimbia wimbo wa bethidei sawa?) Vicky alisema huku akicheka lakini Nicky hakujibu alikimbia kuelekea kwenye dirisha la dereva.
“Daddy!Daddy! Daddy! Buy me Ice cream when you come back ok?”(Baba!Baba!Baba! Ninunulie Ice cream mnaporudi sawa?) Nicholaus alimwambia baba yake.

Alikuwa kipenzi kikubwa cha baba yake, hawakuwa baba na mtoto tu bali mtu na rafiki yake, Martin alishindwa kuelewa bila mtoto wake Nicholaus kuwepo furaha yake ingekuwa wapi! Hoyce pia alifahamu kuwa Martin alimpenda sana Nicholaus na kwa sababu hiyo naye akajikuta akimpenda sana Victoria, mtoto mmoja akawa na mama na mwingine wa baba.
Hakuna mtu kati yao aliyejua wala kuhisi kuwa siku hiyo ingeishia kuwa machozi na majonzi makubwa katika familia yao, hakuna mtu aliyehisi kuwa wasingeonana tena, hakuna mtu aliyejua hawakuwa na masaa hata matatu mbele yao! hakuna mtu aliyejua walikuwa wakimwacha Nicky katika mateso makubwa.

Walipofika best bite waliichukua keki na kulipa pesa iliyobaki, Vicky alimkumbusha Martin kununua Ice cream, akafanya hivyo na wote wakaingia tena ndani ya gari tayari kwa kurudi nyumbani! Kabla gari halijaingia barabarani Vicky aliongea kwa sauti.
“Baba nataka maputo ya bethidei!”
“Tutayanunua wapi saa hizi mwanangu?”

“Labda twende supermarket ya Imalaseko!” Alishauri Hoyce.
Bila kutia neno kwa sababu Martin alitaka kumridhisha mtoto wake alikata kulia na kuanza kuliendesha gari lake aina ya Landcruiser kuelekea katikati ya mji lilikokuwa duka kubwa la Imalaseko ambalo liliuza kila aina ya bidhaa bora katika jiji la Arusha.
Gari ilitembea kwa kasi na wakati huo huo mawazo ya Martin kama ilivyowafanya biashara wengi duniani yalishahama ndani ya gari na kwenda sehemu nyingine akiziwazia biashara zake mbalimbali nje ya Tanzania.
“Mamaaaa weee! Martin! Baba wawili!” Hoyce alipiga kelele.
“Nini mke wangu?” Martin alishtka kama mtu aliyetoka usingizini
“Treni hilo hulioniii?”

Martin alipogeuza macho yake kuangalia upande wa pili alilia macho yake yalipokutana na kichwa cha treni kikija kwa kasi! Alipiga kelele lakini haikusaidia kitu, dereva wa treni hakusimama treni liliigonga gari yao na kupita juu yake! Ikawa kimya kabisa, treni halikusimama liliendelea na safari yake.

Je, nini kitaendelea?
Tukutane Jumanne mahali hapa.
Share kadiri uwezavyo kwa ajili ya kuisambaza hadithi hii tamu.

Darassa Anusurika Kifo kwa Ajali Hii Mbaya ya Gari Huko Kahama Shinyaga

Comments are closed.