The House of Favourite Newspapers

Esma Miaka 8 ya Kukurukakara Penzi la Petit

0

AHMED Manungwa ‘Petit Man’ ni meneja wa wanamuziki mbalimbali wa Bongo Fleva. Baadhi ya waliopitia mikononi mwake ni pamoja na Mirrow na Jordan kisha baadaye akawapokea mastaa kama Billnass na Nuh Mziwanda chini ya lebo yake ya LFLG.

 

Hiyo ndiyo kazi iliyoanza kumpa jina mjini kabla ya kupaishwa na uhusiano wake wa kimapenzi kisha ndoa na dada wa mwanamuziki mkubwa wa Bongo Fleva ndani na nje ya nchi, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ au ‘Mondi’. Huyu si mwingine ni mwanamama maarufu kwenye mitandao ya kijamii (sosholaiti), Esma Khan almaarufu kama Esma Platnumz.

 

Petit au Petie na Esma wamejaaliwa mtoto mmoja wa kike aitwaye Taraj. Wawili hawa wamedumu penzini kwa takriban miaka nane iliyojaa kukurukakara za kutosha.

 

Walianza na uhusiano wa kimapenzi wa boyfriend na girlfriend. Baadaye waliingia kwenye ndoa. Wakiwa kwenye ndoa, waliwahi kuachana kisha wakarudiana.

 

Hata hivyo, kukurukakara hazikuishia hapo kwani baadaye waliachana tena ambapo kila mmoja alipata mwenza mwingine. Petit akadaiwa kuchepuka na chipukizi wa Bongo Fleva, Malkia Karen kabla ya kuamua kuoa mwanamke mwingine, huku Esma naye akienda kwa mwanaume mwingine.

 

Unaambiwa penzi la kweli halifi! Hicho ndicho kilichotokea kwa wawili hawa ambapo mwishoni mwa mwaka jana, walirudiana na kuamua kutulia kujenga familia yao. OVER ZE WEEKEND imekusogezea wawili hawa ambapo wanafunguka juu ya safari yao ya mapenzi hadi leo;

OVER ZE WEEKEND: Watu wanawaona tu, lakini hawajui mlikutana wapi na ilikuwaje?

 

PETIT MAN: Nakumbuka nilikuwa ninapenda kwenda nyumbani kwa Wema, wakati huo pale Kijitonyama. Halafu Esma alikuwa anakuja pale kwa wifi yake (wakati huo Wema akiwa mpenzi wa Mondi).

 

Halafu Aunt (Ezekiel) naye tulikuwa tukikutana wote pale. Sasa siku moja Aunt akaona kama mimi na Esma tuna dalili ya kupendana, hivyo akaunganisha mambo. Hatimaye tukawa wapenzi na baadaye tukafunga ndoa.

OVER ZE WEEKEND: Ni kitu gani ulichokipenda kwa Esma?

 

PETIT MAN: Siku zote mapenzi hayaulizwi kwa nini ulimpenda huyu, ila ninachojua ni upendo wa dhati, yaani mnajikuta tu mioyo yenu inaongea kimyakimya kisha mnajikuta tu mko pamoja. Kikubwa ni kwamba Esma ni mwanamke anayependa sana maendeleo kila kukicha.

OVER ZE WEEKEND: Kwa nini mara nyingi mnagombana?

 

PETIT MAN: Kwenye mapenzi ya kweli hakukosi kugombana na mara nyingine unakuta hakuna sababu kubwa zaidi ya wivu tu, ndiyo unafanya tunagombana. Hata hivyo, tukishaachana na kila mtu kuwa kivyake, tunakumbukana na mwisho wa siku tunarudiana bila kuangalia nani anasema nini au atasema nini.

 

OVER ZE WEEKEND: Petit umemuoa dada wa mwanamuziki mkubwa, inakuwaje kwa upande wa familia ya Esma?

PETIT MAN: Mimi nimemuoa Esma na siyo dada wa nani. Ninachojua ni kwamba familia ya mke wangu inaniheshimu na kunipenda mno.

 

OVER ZE WEEKEND: Vipi kuhusu mwanamke mwingine uliyemuoa kisha ukamuacha na kurudi kwa Esma?

PETIT MAN: Nina mke mmoja ambaye niko naye kwa sasa. Siwezi kumzungumzia mtu mwingine kwa sababu niko na mke wangu, Esma. Haitaleta picha nzuri.

 

OVER ZE WEEKEND: Miaka nane kwenye mapenzi siyo michache, lakini pia siyo mingi. Je, ni changamoto gani mmepitia?

PETIT MAN: Changamoto ni nyingi sana, lakini tunajitahidi kuzikabili wenyewe na kuzimaliza bila kumshirikisha mtu yeyote. Ikifikia hatua ya kumshirikisha mtu, basi ujue ni jambo kubwa. Ninachoamini mimi ni kwamba hakuna barabara isiyokosa kona au milima na mabonde. Hicho ndicho ambacho tumekishuhudia kwa miaka hiyo.

 

OVER ZE WEEKEND: Inasemekana wewe na Diamond haziivi, tatizo ni nini?

PETIT MAN: Kwa nini zisiive, wakati ni shemeji yangu? Hayo ni maneno ya watu na mitandao, lakini ukweli ni kwamba tuko vizuri sana na tunaheshimiana. Watu hawatuoni pamoja kwa sababu kila mtu anakimbizana na maisha.

OVER ZE WEEKEND: Kwa upande wako Esma, unamzungumziaje mumeo?

 

ESMA: Kwa kweli ni mume bora kabisa. Haijalishi tumepitia kukurukakara kiasi gani, lakini kikubwa ni baba ambaye anaipenda na kuijali sana familia yake na hilo ndilo kubwa kwangu.

OVER ZE WEEKEND: Ulijisikiaje uliposikia mumeo ameoa?

ESMA: Niliona kawaida sana kwa sababu nilijua Petie ni mume wangu na atarudi tu kwa sababu nilijua wazi hana furaha huko alipo, bali furaha yake ipo kwangu. Nilijua atarejea.

 

OVER ZE WEEKEND: Je, unakutana na changamoto gani kama mwanamke kwenye ndoa yako?

ESMA: Changamoto ni za kawaida sana kwa sababu mimi ni mwanamke ambaye naelewa vizuri maisha, hivyo sisumbuki na chochote kwa upande wangu maana niko imara.

 

OVER ZE WEEKEND: Mnatarajia kuongeza mtoto mwingine?

ESMA: Hiyo ni lazima. Tunatarajia kuongeza watoto, tena siyo mmoja ni wengi kwa sababu hatuna tatizo na mtu. Kwa nini tusizae kwa sababu tunatafuta maisha kwa nguvu zetu zote.

 

OVER ZE WEE-KEND: Ulish-awahi kupigana kwa sababu ya Petit?

ESMA: Hapana na siwezi kufanya hivyo hata siku moja kwa sababu mimi ni mwanamke ninayejitambua mno. Mambo ya kupigana kwa sababu ya mwanaume, yalishapitwa na wakati, hivyo siwezi kufanya hivyo.

 

IMELDA MTEMA

 

Leave A Reply