The House of Favourite Newspapers

Ewura, Sumatra ni ‘Kajipu Uchungu’, Katumbuliwe!

0

Bei ya mafuta ghafi katika soko la dunia imeshuka. Kwa mujibu wa viwango vya bei ya mafuta katika soko hilo mwanzoni mwa mwezi huu, pipa moja liliuzwa dola 30, ikiwa ni punguzo kubwa.

Bei hiyo ilipanda zaidi Mei mwaka jana, ilipokuwa ikiuzwa kwa dola 60 kwa pipa moja, lakini tangu wakati huo imekuwa ikipungua kila mwezi hadi kufikia bei hiyo ya mwezi huu.

Kwa mujibu wa mtandao wa Macrotrends, unaorekodi bei ya mafuta ghafi katika soko la dunia, katika miaka kumi iliyopita, nishati hiyo ilikuwa ghali zaidi Juni 2008, wakati pipa moja lilipouzwa kwa dola 144.

Tangu bajeti ya mwisho ya serikali ya mwaka jana iliyosomwa Julai, ambapo bei ya bidhaa hiyo katika soko la dunia ilipokuwa ni dola 47, haijawahi kupanda, zaidi ya kushuka kila mwezi.

Lakini wakati bei hiyo ikishuka kila mwezi, hapa nchini, bei yake inashuka kwa mbinde, tena kwa kiasi kidogo mno. Nilipata kumsikiliza Meneja Mawasiliano wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), Titus Kaguo alipokuwa akijibu malalamiko ya wananchi juu ya ukimya wa chombo hicho katika kupunguza bei ya mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa.

Alitoa utetezi dhaifu unaolenga kuwalinda wafanyabiashara wa nishati hiyo na kuwabana watumiaji wa mwisho. Kwa sababu ni jambo lisiloakisi vyema kuona kuwa gharama za uendeshaji zinabakia kuwa zilezile wakati bei ya bidhaa inashuka, tena kwa kasi.

Kinachoshangaza ni kuwa wakati Ewura imekuwa na kigugumizi cha kushusha bei ya mafuta kuendana na ile ya soko la dunia, imekuwa na kasi ya ajabu ya kupandisha pale bei hiyo inapopanda katika soko la dunia.

Utetezi wao mara zote ni eti bei inaposhuka katika soko la dunia, waagizaji wanakuwa bado wana mafuta waliyoagiza kwa bei ya zamani, hivyo kuwashushia ni kuwaumiza. Hawasemi ni vipi bei ikipanda na wao wanapandisha mara moja wakati wafanyabiashara hawa bado wana stoku waliyonunua kwa bei ya zamani!

Ewura ni jipu linalopaswa kutumbuliwa mara moja. Kaguo anasema Ewura kama Mamlaka haifaidiki na kupanda kwa bei ya mafuta kwa sababu yenyewe hupata gawio kulingana na lita za bidhaa na wala siyo bei yake sokoni.

Hili linaweza kuwa sawa, lakini katika mazingira ya biashara hii, hauwezi kuacha kuungana na wananchi wanaoamini kuwa baadhi ya vigogo wa Ewura wanafaidika kwa kufungamana na wafanyabishara katika kuwaumiza wananchi.

Wananchi wanapaswa kufaidika na kila punguzo la mafuta linalotokea kama ambavyo wanaumizwa na kila ongezeko lake katika soko la dunia.

Lakini wakati mafuta yakipungua bei, unashangaa mamlaka nyingine ya Usimamizi wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) nayo inashiriki kuwanyonga wananchi mchana kweupe.

Nauli za daladala jijini Dar es Salaam kwa mfano zimepanda katika maeneo mbalimbali. Wenye magari wanapunguziwa bei ya mafuta, lakini wasafiri, ambao ndiyo walalahoi, wanaongezewa nauli.

Tunataka kuona Sumatra nayo ikipunguza nauli kote nchini ili kila mmoja anufaike na punguzo la mafuta katika soko la dunia, kama anavyoumizwa pale bei hizo zinapopanda.

Chombo hiki nacho ni jipu lingine linalopaswa kutazamwa vizuri na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Leave A Reply