The House of Favourite Newspapers

EXCLUSIVE: KOCHA MPYA YANGA AISUBIRI SIMBA KWA HAMU (Video)

Kocha mpya wa Yanga Mkongomani Zahera Mwinyi.

 

KOCHA mpya wa Yanga, mzaliwa wa DR Congo, Zahera Mwinyi jana mchana alimalizana na uongozi wa klabu hiyo na kuwaambia mashabiki kwamba anajua vilivyo ugumu na umuhimu wa mechi dhidi ya Simba Jumapili ijayo.

 

Zahera alitua nchini juzi alfajiri ambapo jana alifanya mazungumzo ya kina na uongozi na wakakubaliana kwenye mambo mengi ya msingi na leo Jumatano asubuhi atatua Morogoro tayari kusalimiana na wachezaji hao na ataangalia mambo kadhaa ndipo arejee Dar es Salaam kusaini mkataba wa kazi.

 

Kocha huyo anayezungumza Kiswahili kwa lafudhi ya Kikongomani, amepewa rasmi nafasi ya George Lwandamina aliyeikimbia Yanga na kurudi katika klabu yake ya zamani ya Zesco. Hivyo atasaidiwa na Noel Mwandila na Shadrack Nsajigwa.

 

Akizungumza na Championi Jumatano, Jijini Dar es Salaam jana muda mfupi kabla ya leo kwenda Morogoro kuiangalia timu, kocha huyo alisema; “Nimekaa kwenye timu nyingi kubwa za Ulaya, najua timu kubwa zilivyo. Kuna vitu namalizana na Kamati, kazi itaanza muda wowote.”

 

Alipoulizwa kama anajua Yanga inakabiliwa na mechi ngumu dhidi ya Simba Jumapili alisisitiza kwamba taarifa hizo anazo na wala hana presha yoyote anajua nini cha kufanya kwavile ana uzoefu mkubwa alioupata Barani Ulaya.

 

“Nimecheza mechi nyingi ngumu Ulaya, nina uzoefu nazo. Simba naijua ni timu ngumu lakini najua jinsi ya kuikabili,” alisisitiza kocha huyo ingawa uwezekano wa yeye kukaa kwenye benchi Jumapili ni mdogo kutokana na vibali vya kazi pamoja na kutokaa na timu muda mrefu.

 

Mwinyi ambaye ana uraia wa Ufaransa akiwa amezaliwa miaka 46 iliyopita DR Congo, Championi Jumatano linajua kwamba ameunganishiwa mchongo huo na kiungo Pappy Kabamba Tshishimbi.

 

“Namfahamu Tshishimbi kwa kumsikia lakini siyo kwa kukutana naye, hivyo nitafanya naye kazi kikamilifu,” alisema kocha huyo.

 

Kocha huyo mwenye Leseni A ya Uefa alisema kuwa amewahi kufanya kazi na Roul Shungu aliyewahi kuinoa Yanga miaka ya nyuma na analijua vizuri soka la Afrika na anajua ushindani ni mkubwa hivyo atapambana, hana hofu yoyote.

 

AFC Tubize ya Ubelgiji ilimpa Ukocha Mkuu mwaka 2010 ambapo alidumu kuanzia Julai mpaka Agosti, kisha akaondoka na kujiunga na timu ya Taifa ya DR Congo kama Kocha msaidizi lakini baadaye mwaka 2014 alirudi tena Tubize kama kocha wa muda.

Amewahi kuifundisha pia DC Motema Pembe ambayo ni moja kati ya klabu kubwa za DR Congo lakini mpaka anatua Jangwani jana Jumanne alikuwa kwenye benchi la timu ya Taifa na kile kikosi kilichopigwa mabao 2-0 ndani ya Uwanja wa Taifa alikuwa benchi.

 

Mara ya mwisho Yanga kuwa chini ya Kocha Mkongo ilikuwa mwanzoni mwa miaka ya 2000 ambapo, Polycarpe Bonghanya alikinoa kikosi hicho kilichokuwa na mastaa kadhaa wa Congo akiwemo Patrick Katalay, Pitchou Kongo na Alou Kiwanuka lakini Kocha huyo aliishia kutimuliwa na wanachama ambao walimfungia geti la Uwanja wa Kaunda asiingie mazoezini asubuhi huku wakimtakia “closed..closed” wakimaanisha pamefungwa kwavile alikuwa hajui Kiingereza zaidi ya Kilingala.

 

Bonghanya alipingwa na wanachama kwa madai kwamba timu ilikuwa haifanyi vizuri.

Kibarua kikubwa

Mtihani wa kwanza wa Kocha huyo ni kwenye hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho inayoanza mapema mwezi ujao lakini vilevile kucheza vizuri karata zake kutetea ubingwa wa Yanga unaonyemelewa na Simba.

Comments are closed.