Exim Yamteua Balozi Mwapachu Kuwa Mwenyekiti Bodi ya Wakuregenzi

Mwenyekiti mpya wa Bodi ya Wakurugenzi Benki ya Exim Tanzania, Balozi Juma Mwapachu.

Benki ya Exim Tanzania imemteua Balozi Juma Mwapachu kuwa Mwenyekiti wake mpya wa Bodi ya Wakurugenzi, akichukua nafasi ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi hiyo Said Mwema ambaye amemaliza muda wake kwa mafanikio kulingana na sera ya uongozi wa benki hiyo.

 

Balozi Juma V. Mwapachu ambaye kwasasa ni Mkurugenzi, Bodi ya Wakurugenzi, kampuni ya Heritage Insurance Tanzania Limited tangu 1998, Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Alliance Life Assurance Tanzania Limited tangu 2014, ana uzoefu mkubwa akiwa amewahi kushika nyadhifa mbalimbali serikalini, katika mashirika ya umma, sekta binafsi na kwenye asasi za kiraia nchini Tanzania, kikanda na kimataifa.

 

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari hii leo, Bodi ya Wakurugenzi ya benki hiyo imemshukuru Balozi Mwapachu kwa uongozi wake wa mfano na mchango wake akiwa kama Mkurugenzi katika Bodi hiyo tangu 2011 ikibainisha kuwa akiwa Mkurugenzi wa Bodi hiyo Balozi Mwapachu alihakikisha kuwa Benki hiyo inaendelea kusonga mbele kimkakati na kiutendaji.

 

“Uzoefu wake mwingi, maarifa na uongozi aliouthibitisha utazidi kuipatia benki kasi ya kuendelea na ubunifu, kutafuta ukuaji wa baadaye, na kuimarisha zaidi msimamo wetu tukiwa miongoni mwa taasisi kubwa za kifedha nchini,” alisema Afisa Mtendaji Mkuu wa benki hiyo Jaffari Matundu wakati akitoa maoni yake kuhusiana na uteuzi huo.

 

Balozi Mwapachu ana Shahada ya Sheria kutoka Chuo Kikuu cha Afrika Mashariki (1969) Stashahada ya Juu katika Sheria za Kimataifa kutoka Chuo cha Sheria ya Kimataifa cha Indian Academy (1978), Udaktari wa Fasihi (Honoris Causa-2005) kutoka Chuo Kikuu cha Dar- es-Salaam na Udaktari wa Sayansi ya Siasa (honoris Causa 2012) kutoka Chuo Kikuu cha Taifa cha Rwanda.

 

Katika uongozi wa nafasi za juu Balozi Mwapachu amewahi kuwa Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa (2002-Aprili 2006), Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (Aprili 2006-Aprili 2011) na Mwenyekiti wa Kamati ya Watendaji Wakuu katika Utatu wa COMESA-EAC-SADC (2008-2011). Pia Balozi Mwapachu amewahi kuwa Rais wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kimataifa (SID) kutoka 2012-2016.

 

Mjumbe mteule wa Bodi ya Benki ya Exim Tanzania, Irene Madeje-Mlola.

Kwa miongo kadhaa ya utumishi wake, Balozi Mwapachu ameongoza uanzishwaji wa taasisi mbali mbali ikiwemo Chemba ya Biashara Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA), Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI) na Baraza la Biashara la Afrika Mashariki.

 

Katika hatua nyingine, Bodi ya Benki hiyo pia ilitangaza kumteua Irene Madeje-Mlola kama mjumbe mpya wa Bodi

Irene Madeje-Mlola ana Shahada ya Uzamili katika Utawala wa Biashara kutoka Shule ya Masuala ya Utawala ya Maastricht ya nchini Uholanzi na Taasisi ya ESAMI na Shahada ya Biashara (Bcom) kutoka Chuo Kikuu cha Dalhousie nchini Canada.

 

Irene ni Mkurugenzi wa Kampuni aliethibitishwa na Jumuiya ya Madola ya Utawala wa Kampuni na pia ana cheti cha Uongozi wa Kimkakati wa Fedha Jumuishi kutoka Shule ya Biashara ya Harvard. Bi Irene amebobea kwenye maeneo kadhaa ikiwemo mabadiliko ya biashara, ujumuishaji wa kifedha, usimamizi wa miradi na uongozi wa jumla. Kwasasa Bi Irene ni Mkurugenzi wa Uendeshaji katika taasisi ya Financial Sector Deepening Tanzania (FSDT) akisimamia Idara ya utaalamu na uendeshaji.

 

Anatarajiwa kuongeza mchango wake wa uzoefu mkubwa kutoka katika nafasi mbali mbali za uongozi na usimamizi alizoshikilia katika Sekta za Fedha na Mawasiliano; baada ya kufanya kazi katika majukumu ya kimkakati na ya uongozi katika mashirika ya kimataifa kama vile Benki ya Scotia, Benki ya Royal ya Canada, Benki ya Barclays, Vodacom, Airtel, na taasisi ya Financial Sector Deepening Tanzania (FSDT) ambayo ameisaidia katika mabadiliko yake.

Katika jukumu lake la sasa, Irene ameshiriki katika mabadiliko makubwa na nafasi ya ndani ambayo imefungua njia kwa shirika katika kuchochea ujumuishaji wa kifedha na kusaidia nchi kufikia malengo ya Kitaifa. Pamoja na uongozi wake katika ajenda ya ujumuishaji wa kifedha wa kijinsia nchini Tanzania, alifanya kazi kwa karibu na baraza la Kitaifa la ujumuishaji wa kifedha ili kuhakikisha wanawake na vijana wanapewa kipaumbele katika mkakati wa Kitaifa.

 

Irene ana uzoefu mkubwa katika sekta ya mawasiliano na kibenki ambapo amefanya kazi katika nafasi za uongozi wa juu ndani na nje ya nchi. Aliongoza mabadiliko makubwa katika Sekta ya mawasiliano ambapo alisimamia utafutaji wa wafanyakazi zaidi ya 500 kutoka nje ya shirika (outsourcing), njia iliyoongeza ufanisi mzuri wa biashara kwa shirika.

 

“Akiwa hodari katika ukuzaji wa mifumo mpya, usimamizi mzuri na uanzishaji wa shughuli ndogo ndogo katika mashirika, Irene anabeba haiba ya uvumbuzi na fikra za kimkakati ambazo zitakuwa muhimu kwa ukuaji wa Benki yetu” alisema Matundu.

Na Mwandishi wetu.

Toa comment