Exclusive: Baba Amjibu Mama Kanumba; Asema “Anaomba Rambirambi Baa!”- Video
WAKATI ni miaka saba imekatika tangu tasnia ya filamu Bongo na taifa zima kwa jumla lipate pigo la kuondokewa na aliyekuwa nguli wa uigizaji nchini, marehemu Steven Kanumba, +255 Global Radio imezungumza na mama wa msanii huyo, Bi. Florah Mtegoa, aliyedai kwamba hakumpa pesa za urithi mzazi mwenzake, Baba Kanumba, kwa sababu alimkataa na kumtelekeza mtoto huyo ambaye baadaye alikuja kuwa nyota kitaifa.
Kupitia kipindi cha Kata Mbuga cha Global Radio, mama huyo amefunguka kwa mara ya kwanza mgogoro wake na Baba Kanumba, ambao unatajwa kuwa unasababishwa na mali za mtoto wao na kudai kuwa, hata hivyo, alikuwa mchepuko wake tu kwa sababu baba huyo alikuwa na mkewe na watoto, ndiyo maana alimtelekeza.
Hata hivyo, baba huyo, Mzee Charles Kanumba, mwenye maskani yake mkoani Shinyanga, naye amepangua tuhuma hizo na kudai kuwa hakuwahi kumtelekeza mtoto akisema alikuwa akiishi na Kanumba tangu akiwa mdogo hata ndugu zake wanamfahamu vizuri.
Aidha, mzee huyo amesema hakufika msibani kwa sababu alikuwa akiumwa wakati msiba huo ulipotokea lakini alituma ndugu zake na walifika. Katika kushusha tuhuma zaidi, amesema mzazi mwenzake huyo amekuwa akiomba rambirambi kwa ajili ya marehemu hadi kwenye baa na kumbi za starehe.


Comments are closed.