The House of Favourite Newspapers

Eymael Kusajili Wapya Kumi Yanga

0

VIONGOZI wa Yanga wamempa kocha mkuu wa timu hiyo, Mbelgiji, Luc Eymael jukumu zito la kuamua usajili wa wachezaji kumi ambao mikataba yao inafikia kikomo mwishoni mwa msimu huu wa Ligi Kuu Bara.

 

Hatua hiyo imekuja baada ya hivi karibuni kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Bernard Morrison raia wa Ghana kuongezewa mkataba wa miaka miwili kutoka ule wa mwanzo wa miezi sita uliotarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu huu.

 

Kwa mujibu wa kanuni za Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), mchezaji anaruhusiwa kufanya mazungumzo na klabu yoyote itakayomuhitaji kama mkataba wake ukibaki miezi sita.

 

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Spoti Xtra, uongozi wa Yanga tayari umeanza kufanya mazungumzo na baadhi ya wachezaji wake inaowahitaji kwa ajili ya kuwaongezea mipya.

Mtoa taarifa wetu aliwataja wachezaji hao ni Said Juma Makapu, Deus Kaseke, Mrisho Ngassa, Juma Abdul, Kelvin Yondani, Jafari Mohamed, Vincent Andrew ‘Dante’, Ramadhani Kabwili, Feisal Salum ‘Fei Toto’ na David Molinga.

Aliendelea kusema kuwa, hatma ya wachezaji hao wote amekabidhiwa kocha mkuu wa timu hiyo, ambaye ndiye atakayeamua mchezaji gani anaona aongezewe mkataba.

 

“Jumla ya wachezaji saba wamemaliza mikataba yao, hivyo kocha Luc ndiye amekabidhiwa jukumu la kupendekeza usajili wa wachezaji wake katika msimu ujao.

 

“Kocha tayari ana majina yake ambayo ameyapendekeza katika usajili kwa wale ambao mikataba yao inamalizika mwishoni mwa msimu huu.

 

“Upo uwezekano mkubwa wa panga kubwa kupita katika timu hiyo katika kuelekea msimu ujao, hiyo ni baada ya kocha kuona wapo baadhi ya wachezaji ni mizigo na hawana mchango katika timu,” alisema mtoa taarifa huyo.

 

Makamu Mwenyekiti wa timu hiyo, Frederick Mwakalebela, alipoulizwa kuhusiana na hilo, alisema: “Msimu ujao tunataka kutengeneza timu itakayokuwa imara itakayotupa mataji mbalimbali na tunataka kuhakikisha tunalitimiza hilo, jukumu la usajili lote tunamuachia kocha na lengo ni kuleta wachezaji wengine zaidi ya Morrison ambaye ni mchezaji tishio katika timu.”

Leave A Reply