The House of Favourite Newspapers

Eymael: Morrison Atawamaliza Simba

0

LUC Eymael, Kocha Mkuu wa Yanga amesema kuwa kiungo wake mshambuliaji Bernard Morrison yupo tayari kuimaliza Simba kwenye mchezo wa hatua ya nusu fainali wa Kombe la Shirikisho unaotarajiwa kuchezwa keshokutwa Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa.

 

Morrison hakuwa kwenye kikosi kilichoivaa Biashara United, Julai 5 kwenye Uwanja wa Karume lakini alipanda ndege kutoka Dar kwenda Kagera, Julai 6, akajiunga na kikosi kisha kucheza dhidi ya Kagera Sugar baada ya Eymael kuhitaji huduma yake.

Akizungumza na Championi Ijumaa, Eymael alisema wachezaji wake wote wapo tayari kwa ajili ya mchezo dhidi ya Simba ikiwa ni pamoja na kiungo wao aliyemtungua Aishi Manula, Morrison mnamo Machi 8 katika mchezo wa Ligi Kuu Bara.“Nadhani umemuona Morrison yupo kwenye kikosi na yupo tayari kwa ajili ya mchezo dhidi ya Simba.

 

Amesharejea tayari kikosini na mchezo wetu dhidi ya Kagera Sugar amefunga bao moja lililotupa ushindi, unafikiri nini kitatokea?“Wachezaji wengine wanaendelea vizuri, nikianza na Haruna Niyonzima yeye ninampa 50/50 mpaka sasa, Juma Abdul ninampa 100, Kaseke (Deus), Ngassa,(Mrisho), Jaffary (Mohamed) wote wapo fiti ni suala la kusubiri na kuona mambo yatakuwaje,” alisema Eymael.Mchezo wa Julai 12, utakuwa ni dabi ya tatu kwa Simba na Yanga kukutana msimu huu, Yanga ikishinda moja na kupata mabao matatu huku Simba ikiifunga mabao mawili, mchezo wa kwanza ukimalizika kwa sare.

 

Mshindi wa mchezo huo atakutana na mshindi wa mchezo kati ya Sahare All Stars itakayocheza dhidi ya Namungo FC kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, kesho Jumamosi.

 

KOCHA ATAMBA KUZIJUA MBINU

Wakati huohuo, Eymael amefichua kuwa anafahamu namna ya kucheza na Simba, hivyo hapati tabu ya kukiandaa kikosi chake kuelekea katika mchezo huo.“Ukicheza na mpinzani wako kama Simba lazima umheshimu, lakini uwe makini katika kuziba nafasi zako ili wao wasipasiane kwenye lango lako.

Simba wanashauku ya kutufunga, kwa hiyo watajisahau na sisi tutatumia kujisahau kwao kuwafunga. Mashabiki waje kwa wingi, maana naahidi kucheza soka lenye burudani,” alisema Eymael.

STORI: Lunyamadzo Mlyuka na Issa Liponda

 

Leave A Reply