FAGIO KALI CCM

HALI ya mambo ndani ya Chama Cha Mapinduzi ‘CCM’ kinachounda serikali si shwari kutokana na kuwepo kwa madai kuwa, kuna baadhi ya makada wa chama hicho wanamhujumu mwenyekiti wao ambaye ni Rais Dkt. John Magufuli kuelekea uchaguzi mkuu 2020. Kutokana na sababu hiyo baadhi ya wanachama na wakereketwa wa chama hicho wamekuwa wakiomba lipitishwe fagio la chuma ndani ya chama kuwang’oa wasaliti kabla ya kufikia uchaguzi mkuu ujao.

Wanachama ambao wametajwa waziwazi nao kwa wakati tofauti kukanusha tuhuma za kumhujumu mwenyekiti ni makatibu wakuu wastaafu wa CCM, Abdulrahman Kinana na Yusuf Makamba. Wengine ni Waziri wa Zamani wa Mambo ya Nje, Bernard Membe, Nape Nnauye na January Makamba aliyetumbuliwa Jumapili akiachishwa kazi na Rais Magufuli ya kuhudumu kama Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu anayeshughulikia Muungano na Mazingira.

‘KLIPU’ ZA SAUTI ZILIZOVUJA ZAKOLEZA MOTO

Wakati madai ya wasaliti kuwepo ndani ya CCM yakiendelea kufukuta huku mwanaharakati huru Cyprian Musiba akijitokeza na kuwataja wale aliowaita wasaliti,  ‘klipu’ za sauti zinazodaiwa kudukuliwa kutoka kwenye mawasiliano ya wanachama hao zilivuja na kuzua gumzo mitaani na kwenye mitandao ya kijamii. Licha ya kudaiwa kuwa sauti zinazosikika katika ‘klipu’ hizo zilizojaa mikakati na maudhui ya kupingana na msimamo wa Rais Magufuli ndani ya chama hicho ni za Makamba (baba), Makamba (mtoto), Kinana, Nape na Membe watuhumiwa hao hawajajitokeza kuzikana au kuzikubali sauti hizo. Jambo hilo lilizidi kuibua hisia kali kwa baadhi wanachama wa CCM na kuzidisha shinikizo kwa viongozi wa juu kuwataka wachukue hatua za kuwaondoa makada wote wanaotuhumiwa kwa usaliti.

“Namuomba katibu mkuu wetu (Bashiru Ally) hawa watu (wanaomsaliti na kumsema vibaya rais) wafukuzwe kwenye chama,” alisema Livingstone Lusinde, Mbunge wa Mtera kupitia CCM.

FAGIO LA CHUMA KUPITA CCM

Chanzo makini kutoka ndani ya chama hicho tawala kinasema kuwa, mkakati uliowekwa na viongozi ukisimamiwa na Mwenyekiti Magufuli ni kuwafukuza wasaliti wote ndani ya chama. “Huwezi kupanga nyumba moja na shetani, lazima kumfukuza ili heri iwepo, chama chetu kinataka taifa lenye heri. “Kama chama tunaamini hatuwezi kuwatumikia vyema wananchi waliotuweka madarakani kama tutakuwa na wasaliti ndani ya chama chetu,” chanzo hicho kilisema.

MAKAMBA ATOLEWA MFANO

Aidha chanzo hicho bila kufafanua zaidi kilisema: “Makamba (January) yupo wapi? Tumbuatumbua inaendelea si kwa wasaliti wa kusambaza ‘klipu’ tu za kudharau mamlaka hadi kwa wale ambao hawaendani na kasi ya kuleta maendeleo aliyonayo Rais Magufuli. “Wewe mwenyewe umekuwa shahidi, mawaziri, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na wateule wengine wa rais wamekuwa

kikaangoni, yule ambaye anazembea katika kazi anatimuliwa bila kujali ukubwa wake ndani ya chama au serikali.”

BANA AFUNGUKA TUMBUATUMBUA YA MAGUFULI

Akizungumza na Uwazi juzi (Jumapili) kuhusu mwenendo wa Rais Magufuli kuwatumbua wateule wake akiwemo Makamba, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Benson Bana alisema: “Mimi sioni kama ni jambo baya kwa sababu anayewateua ndiyo anawatumbua, lengo lake ni kupata anaotaka waendane na kasi yake. “Hata Makamba (January) watu wanasema ametolewa kwa sababu ya utovu wa nidhamu inawezekana ikawa kweli lakini habebi picha kwamba ndani ya CCM kuna usaliti.”

WASALITI KUNYIMWA NAFASI ZA UONGOZI

Habari kutoka ndani ya CCM zinaeleza kuwa hakuna mwanachama hata mmoja ambaye atabainika kuwa ni msaliti atakayepata nafasi ya kuteuliwa kugombea nafasi ya uongozi ukiwemo udiwani na ubunge katika uchaguzi mkuu utakaofanyika mwakani. “Mimi nawashauri wananchama wenzangu kuacha kujihusisha na masuala ya utovu wa nidhamu na usaliti, vinginevyo

watajikuta katika mkwamo wa kisiasa ndani ya chama chetu,” kilisema chanzo chetu. Alipotafutwa Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Bashiru Ally ili azungumzie yale yanayoendelea ndani ya chama chake, alipokea simu na mwandishi wetu alipojitambulisha kwake, alikaa kimya kwa muda kisha kukata simu na haikupatikana tena.

KINANA, MAKAMBA WALALAMIKIWA

Aidha, siku chache baada ya makatibu wakuu wastaafu wa CCM, Kinana na Makamba kuandika waraka kwenda kwenye baraza la wazee kulalamika kuwa Musiba amekuwa akiwachafua kwa kuwatuhumu kupanga njama za kumkwamisha Rais Magufuli katika mbio zake za urais 2020, baadhi ya makada wa chama hicho wamewashukia vongozi hao wa zamani na kusema ‘wanakivuruga chama.’ “Huwezi kuwa na mgogoro na Musiba halafu ukaomba nguvu ya chama kikubwa kama CCM ikutetee, ina maana Kinana mtu ambaye ni komredi katika siasa hajui hata njia ya kudili na watu kama Musiba? “Nadhani mzee Kinana ni bora angefunga zipu kwenye mdomo wake kuliko kujitokeza hadharani na kutaka kuleta mtafaruku ndani ya chama ambao hauna afya kwa taifa letu,” alisema mbunge mmoja wa CCM kutoka Kanda ya Magharibi ambaye hakutaka jina lake liandikwe.

MAGUFULI AZIDI KUPONGEZWA

Wakati hayo yakiendelea ndani ya chama chake, pongezi kutoka ndani na nje ya nchi zimekuwa zikimiminika kwa Rais Magufuli kutokana na utendaji kazi wake uliotukuka huku akisifiwa kwa kupiga vita rushwa na ufisadi. Katika siku za hivi karibuni, marais Yoweri Museveni wa Uganda na Uhuru Kenyatta wa Kenya walipomtembelea nyumbani kwake Chato mkoani Geita walimwagia sifa Rais Magufuli kwa kufanya mageuzi makubwa ya kiuchumi. Nao baadhi ya makada wa CCM akiwemo Joseph Kasheku ‘Musukuma’, Mbunge wa Geita Vijijini alisema wanaompinga Rais Magufuli wanatakiwa kukamatwa na kushitakiwa ikiwa ni pamoja na kufukuzwa ndani ya chama kwa sababu wanalihujumu taifa.


Loading...

Toa comment