The House of Favourite Newspapers

FAHAMU AINA ZA UGUMBA (INFERTILITY); KUJIKINGA-2

 WIKI iliyopita wakati tunaanza mada hii, tuliona maana ya ugumba na aina zake. Ambapo kama mtakumbuka pia nilieleza sababu zinazosababisha tatizo hilo.  Nilieleza sababu kadhaa za ugumba kwa wanawake, hebu tuendelee kuona sababu nyingine zaidi…

UNYWAJI WA POMBE

Sababu nyingine ni unywaji pombe kupindukia, kuwa na nagonjwa ya muda mrefu kama kisukari (diabetes), magonjwa ya kina mama (Pelvic inflammatory infection, PID), magojwa ya zinaa au saratani.

SIGARA

Pia uvutaji sigara, madawa ya kulevya kama kokeni, bangi, hashishi nk, matatizo ya hedhi, wanawake wanaopata hedhi bila kutoa mayai (anovulatory menstrual cycle), kuwepo kwa cervical antigens ambazo huua mbegu za mwanamume na hivyo kusababisha kwa mwanamke kutopata ujauzito.

KWA WANAUME

Tatizo la ugumba – linaweza kutokea kwa mwanamume wakati wa; kupungua idadi ya mbegu za kiume (decrease number of sperm), mbegu kuzuiwa kutolewa (blockage of sperm) na mbegu za kiume ambazo hazifanyi kazi yake vizuri.

Kwa mwanamume, tatizo la ugumba husababishwa na; ,mazingira yaliyo na kemikali zinazoathiri uwezo wa mwanaume kumbebesha mimba mwanamke, kukaa sehemu zenye joto kali sana kwa muda mrefu, matatizo kwenye mfumo wa viashiria vya asili, unywaji pombe kupindukia, matumizi ya madawa ya kulevya kama kokeni, bangi, hashishi nk, hupunguza idadi na kiwango (quality) cha mbegu za kiume, kuzeeka na kutumia dawa za vichocheo vya mwilini ama kukosekana kwa baadhi ya vichocheo mwilini (hormonal deficiency).

Ugumba kwa mwanaume unaweza kutokea kwa sababu ya kuwa na magonjwa ya korodani (testicular infections) au kwenye mishipa ya korodani (epididymis)

TIBA

Tiba ni kama ifuatavyo; Ushauri nasaha na kuwaelimisha wapenzi wawili. Matatizo mengi ya ugumba hutokea kutokana na uelewa au ufahamu mdogo wa elimu ya uzazi na ya kujamiiana kwa wapenzi au wanandoa. Kuna wanaume wengi ambao hufika kilele haraka wakati wa kujamiana na hivyo kutoa mbegu ya kiume mapema kabla ya muda muafaka (premature ejaculation), hii husababisha  kutopata ujauzito ambapo lawama zote hupelekwa kwa mwanamke pasipo mwanamume kugundua kuwa tatizo ni lake.

Ifahamike kwamba hakuna muda uliotengwa ambao ni muafaka wa kufika kilele kwa mwanamume. Tatizo lingine ni kutofahamu lini hasa ni muda muafaka wa kujamiana ili kushika mimba kwa urahisi. Kuna wanawake ambao hawajui hata mzunguko wao wa hedhi (yaani hawajui wanaanza na kumaliza hedhi lini na wakati wa hedhi wanatumika kwa muda wa siku ngapi).

Ongeza nafasi yako ya kushika ujauzito kwa kujamiana angalau mara 3 kwa wiki kuelekea wakati wa ovulation au kujamiana wakati wa kipindi chote cha ovulation. Ovulation hutokea wiki 2 kabla ya mzunguko wako mwengine wa hedhi, kama una mzunguko wa hedhi wa siku 28 (yaani kila baada ya siku 28 unapata hedhi), ni vizuri kujamiana angalau kwa siku 3 kati ya siku ya 7-18 baada ya kupata hedhi. Wanywaji wapunguze kunywa pombe kupindukia, kuvuta sigara, kuacha matumizi ya bangi, kokeni nk ili kujiweka salama katika kupata tatizo hilo.

Comments are closed.