The House of Favourite Newspapers

Fahamu Athari za Vyakula Vyenye Wanga Mwilini

LEO nataka nikueleze kidogo kuhusu sayansi ya chakula aina ya wanga. Mwili wako hutumia vyakula vikuu aina tatu ambavyo ni wanga, protini na mafuta.

Unatakiwa ujue kuwa gramu moja ya wanga hutengeneza nishati ya mwili kalori nne, ambapo protini nayo hutengeneza kalori nne na mafuta (Fats) hutengeneza kalori tisa, unaona ni zaidi ya mara mbili ya nishati zinazotengenezwa na chakula cha wanga. Hii ina maana kuwa tunaweza kupunguza kula chakula aina ya wanga na tukaishi tukiwa na nguvu nyingi zaidi.

Zipo sababu za kupunguza kula chakula chenye wanga. Unaweza kupunguza au kuacha kabisa ulaji wa vyakula vyenye wanga nyingi, mfano mikate, ugali mweupe, wali, ‘baga’, tambi, mihogo nk. Hakikisha kitendo hicho kiendane na kuongeza kiwango cha ulaji wa mafuta na vyakula vya protini mwilini mwako katika lishe yako. Hii itaufanya mwili wako kuanza kutumia mafuta kama nishati ya mwili ya kwanza kwa kujitengenezea nguvu.

Viungo vya binadamu kama ini na figo vinapokuwa vinatumia mafuta kuzalisha nishati ya mwili hutengeneza viini vya nishati viitwavyo ketone bodies, ambavyo hivi ndivyo hutumiwa na seli za mwili kujitengenezea nishati kwa wingi. Hivyo basi, unapokuwa unajizuia kutumia vyakula vya wanga, mwili wako utatumia karibia siku tano hadi wiki kuanza kutumia mafuta kama nishati ya mwili na hicho kitendo tunaita keto adaption.

Keto adaption ni ile hali ya mwili wako kujenga mazoea ya kutumia mafuta kama chanzo cha nishati ya mwili na hapo ndipo utaanza kuona mabadiliko katika mwili wako. Utakuwa unajisikia mwenye nguvu na utashangaa dalili mbalimbali zilizokuwa zinakusumbua zinapotea hii ni kwa sababu ya uwezo mkubwa wa ketone bodies katika mwili wako dhidi ya sukari (glucose).

Sote tunajua kwamba ulaji wa vyakula vya wanga kwa wingi na vyakula vyenye sukari nyingi vinaongeza kiwango cha sukari kwenye damu zaidi ya kiwango ambacho mwili wako unaweza kuhimili. Mfano; kiwango cha kawaida cha sukari kinachohitajika mwilini mwako ni kijiko kimoja cha chai, hiki hakiwezi kukuletea matatizo kwenye mwili. Binadamu anaishi kwa sukari inayokadiriwa kuwapo kwenye damu kama kijiko kimoja tu cha chai.

Unywaji wa soda moja unaweza kuongeza zaidi ya vijiko 10, hivyo basi mwili wako unakuwa unashindwa kuhimili sukari iliyozidi. Kwa wale wanaopenda kula baga, inakadiliwa kuwa baga moja ya kati inaweza kutoa sukari zaidi ya vijiko 12 kwenye damu.

Swali la kujiuliza ni; mwili unapeleka wapi sukari iliyozidi wakati miili yetu inahitaji sukari kiwango kidogo kama kijiko kimoja tu ili kuishi? Mwili hutengeneza maji kutoka kwenye seli za kongosho ziitwazo beta seli, maji haya ni homon iitwayo Insulin, kazi kubwa ya insulin ni kutunza glucose hii katika damu kwa matumizi ya baadaye, na inatunza katika kiasi maalum katika mfumo wa Glycogen na kiasi kikubwa katika mafuta.

Hivyo basi, mafuta haya huhifadhiwa katika sehemu mbalimbali kama tumboni, shingoni, mikononi, kifuani na kiunoni. Mafuta haya huhifadhiwa katika mfumo wa Tryglycerides ambayo haya ni miongoni ya mafuta mabaya mwilini mwako.

Sasa mtu anayekuambia wanga nyingi katika chakula chako ni salama anakudanganya kwa kiasi kikubwa kwani tunaona jinsi gani ulaji wa kiwango kingi cha vyakula vya wanga na sukari vinavyosababisha sukari kupanda kupita kiasi na insulin kuanza kuhifadhi katika mafuta.

Tumekaririshwa kuwa adui mkuu wa mwili ni mafuta (fats) na kujisahau kuwa ulaji mbovu wa vyakula vya wanga na sukari ni hatari zaidi kwani tunaishia kulea vitambi na magonjwa sugu, hii yote ni kutokana na kutofuatilia lishe nzuri na salama kwako. Makala haya huandaliwa na Mtaalamu wa Lishe, Abdallah Mandai kwa ushauri wasiliana naye kwa namba hizo hapo juu.

BAKWATA MWANZA WATOA TAMKO LINGINE STENDI ya IGOMBE KINACHOENDELEA – “WAISLAM WATULIE”…

Comments are closed.