The House of Favourite Newspapers

Fahamu CD4 Zinavyofanya Kazi Mwilini

0

Wiki iliyopita nilieza kuhusu hatua za mtu kuwa na Ukimwi na kutaja CD4, wengi wamenipigia simu kutaka nifafanue hicho ni nini kitaalam.CD ni kifupi cha maneno ya kitaalam, yaani Cluster of Differentiation.

Hii ni aina mojawapo ya kiasili kilichoundwa kwa protini na mafuta (yaani glycoprotein) ambacho kinapatikana juu ya uso wa seli nyeupe za damu zijulikanazo kama Thelper Cells, Regulatory T-Cells, Monocytes, Macrophages na Dendritic Cells ambazo kazi yake kubwa ni kupambana na maradhi mbalimbali.

Zimepewa jina la CD4 kuonesha kuwa ni aina ya nne katika kundi la viasili vya CD. Kazi zake kubwa ni kusaidia baadhi ya chembe nyeupe za damu kupambana na wadudu waenezao maradhi mbambali katika mwili wa binadamu.

CD4 husaidia kukuza na kupitisha taarifa kutoka kwenye vipokeo vilivyopo kwenye T-Cells. Taarifa hii huzitahadharisha chembechembe nyeupe za damu kujiandaa kupambana na vidudu vilivyovamia mwili kwa kutumia njia mbalimbali. Aina hii ya chembechembe nyeupe za damu inayopambana na uvamizi wa mwili huitwa T-Lymphocytes.

CD4 ni aina ya protini inayopatikana katika ukuta wa seli zinazojulikana kama T-Helper Cells (pia hujulikana kama CD + Lymphocyte).
Virusi vya Ukimwi (VVU) hushambulia na kujishikiza kwenye protini hii kabla ya kupata uwezo wa kuathiri seli za T-Helper.

Seli hizi za T-Helper ndizo hulinda mwili dhidi ya maambukizi mbalimbali na hivyo kuchangia katika kustawi kwa kinga ya mwili.
Kupungua kwa seli hizi mwilini husababisha kupungua kwa kinga ya mwili na hivyo mtu kupata magonjwa nyemelezi.
Baadhi ya magonjwa nyemelezi yanayoweza kumpata mtu mwenye ugonjwa (VVU/Ukimwi) ni pamoja na magonjwa ya mfumo wa kupumua kama vile ugonjwa wa Homa ya Mapafu (Pneumocyctic Carinii Pneumonia), Kifua Kikuu (TB) na Saratani.

Mengine ni magonjwa ya mfumo wa chakula kama vile Cryptosporidiosis, Candida (fangasi), Cytomegolavirus na kadhalika.

Lakini pia mgonjwa akipungukiwa CD4 huweza kupata magonjwa ya mfumo wa fahamu yaani Central/Peripheral Nervous System kama vile Cytomegolavirus, Toxoplasmosis, Cryptococcosis, Mkanda wa Jeshi na Saratani.
Mengine ni magonjwa mbalimbali ya ngozi (Skin Diseases) hasa Saratani ya Ngozi.

VIPIMO
Kutokana na uhaba wa vifaa vya kupimia kiwango cha seli aina ya CD4 katika nchi mbalimbali, Shirika la Afya Duniani (WHO), limetengeza mwongozo mwingine ambao utamsaidia mhudumu wa afya kutambua kama mgonjwa amefikia hatua ya ugonjwa wa Ukimwi na anastahili kuanza tiba au la.
Itaendelea wiki ijayo.

Leave A Reply