Fahamu Chanzo Cha Magonjwa ya Moyo-2
Tunaendelea kuelezea magonjwa ya moyo.
MAGONJWA ya moyo yameshika kasi hapa nchini kiasi cha kutishia uhai wa watu wengi. Hata hivyo maradhi haya kwa asilimia 80 yanazuilika kama hatua za mapema zitachukuliwa. Ndiyo maana upo usemi usemao, kinga ni bora kuliko tiba hivyo ni vema kuchukua hatua mapema kuliko kusubiri tatizo likukumbe. Pale unapoona dalili zisizo za kawaida fika haraka katika huduma za afya kwa ushauri, ikumbukwe kuwa gharama za kutibu magonjwa haya huwa ni kubwa ukilinganisha na magonjwa mengine pia muda wa kukaa hospitalini huwa ni mrefu. Tatizo la moyo linaweza kuanza na kupotea kwa muda mfupi lakini usipolitatua mapema huenda likawa sugu hivyo kuhitaji matibabu ya kina na kukugharimu maishani. Nitaeleza kifupi matibabu, uchunguzi na namna ya kujikinga.
DALILI
Kinachosikitisha hadi sasa katika tasnia ya magonjwa ya moyo, ni kwamba mtu anaweza asione dalili zozote za moja kwa moja za magonjwa ya moyo, hadi wakati mishipa ya damu ya moyo inapokuwa imeziba kabisa au kushindwa kuruhusu damu kwa kasi na kiwango kinachotakiwa.
Mara nyingi, hakuna dalili inayojitokeza moja kwa moja kwa wagonjwa wa aina hii, hadi pale moyo wenyewe unaposhindwa kufanya kazi ghafla (Heart Attack) au mtu anapopata Kiharusi (Stroke). Zaidi ya maelezo hayo ya wataalam wa magonjwa ya moyo, dalili zinapojitokeza mapema huweza kutofautiana kutegemea na aina ya ugonjwa wa moyo, ingawa dalili hizo nazo hazijitokezi mapema kama ilivyo kwa magonjwa mengine. Hata hivyo, dalili kuu za magonjwa ya moyo ni pamoja na maumivu ya kifua (Hii ni dalili kuu ya ugonjwa wa moyo); moyo kwenda mbio na kumfanya mtu akose pumzi au kushindwa kupumua; kuvimba miguu, tumbo na
mishipa ya shingoni kujitokeza nje; maumivu ya mgongo, mabega, shingo na taya; tumbo kujaa, kichefuchefu, na kutapika; kukosa usingizi; kupoteza fahamu na kikohozi kisichokwisha.
MATIBABU NA UCHUNGUZI
Ingawa pia yapo mambo mengi ya kuchunguza yaani maabara na picha nitagusia yale yanayohusu picha maalum za mwili. Uchunguzi wa msingi unahusisha picha ya x-ray ya kifua kuona ukubwa wa moyo na uwepo wa maji katika mapafu. Kipimo cha
‘echocardiogram-kipimo hiki huchunguza sehemu za moyo kama vile chemba, vyumba, valvu, mishipa na mfumo wa vimishipa vya fahamu katika moyo. Kipimo cha electrocardiography-ECGkuangalia shinikizo la damu, mapigo ya misuli ya moyo, kuoza kwa misuli ya moyo na hali ya kiumeme katika moyo.
MATIBABU
Baada ya daktari wako kukufahamisha kutokana na dalili ulizonazo ndipo atafanya uamuzi ama upewe dawa au usipewe dawa. Kupumzika muda mrefu ili usiuchoshe moyo wako wenye tatizo lakini pia mgonjwa anatakiwa alale katika mkao maalum utakaosaidia apumue vizuri yaani mito zaidi ya miwili huwekwa nyuma ya mgongo na kichwa. Kama kuna kitanda maalum robo ya kitanda
huinuliwa juu kidogo.
Kutotumia chumvi na kunywa maji kipindi cha ugonjwa. Mambo mengine ya kuzingatia ni kula mlo usio na mafuta mengi ya wanyama, kula mboga na matunda zaidi katika kila mlo na vyakula visivyokobolewa. Matibabu ya dawa huwa ni maisha yako yote ili kuurudisha moyo katika hali ya kawaida na kufanya kazi ya kusukuma damu.
Katika huduma za afya wataalam wa moyo watakuelimisha zaidi juu ya madhara ya dawa na ugonjwa kwa mfano ushauri nasaha wa tatizo linalowapata wagonjwa hawa huwa na upungufu wa nguvu za kiume kwa kipindi cha ugonjwa lakini baada ya kupata nafuu mtu hurudi katika hali yake. Dawa ni kama vile za kupunguza mrundikano wa maji mwilini, kuifanya misuli ya mwili ikunjuke zaidi na kusukuma damu, dawa za kutanua mishipa ya damu na mwisho ni kutibu tatizo lililosababisha moyo kushindwa kufanya kazi.
Yapo baadhi ya magonjwa ya moyo yanayosababisha moyo kushindwa kufanya kazi ambayo kwa kawaida huwa hayaponi. Hivyo dawa nyingi ni zile za kusaidia moyo ufanye kazi vizuri, na dawa hizi unapaswa kutumia kufuatana na maelekezo ya daktari kwani endapo utazidisha kipimo zina madhara na pengine kusababisha moyo kusimama na hatimaye kifo. Namna ya kujikinga na tatizo hili kiujumla Fika mapema katika huduma za afya pale unapoona dalili, jenga utamaduni wa kupima mapigo yako ya moyo, sukari ya mwili na kiwango cha lehemu mwilini (cholestrol) hii inasaidia kujua mwenendo wa afya yako. Lehemu ni mafuta mabaya yanayosababisha kuharibika mishipa inayopeleka damu katika misuli ya moyo.
Kufanya mazoezi mara kwa mara na mapema kabla ya kupata matatizo ya kiafya ni nzuri kwa afya yako. Mazoezi yanaufanya mwili utumie mafuta ya ziada yaliyorundikana mwilini na pia kuufanya mwili kuwa na mzunguko mzuri wa damu, angalau mazoezi ya kutembea kwa siku kwa dakika 15-30 yanatosha. Epuka hasira, shinikizo la kiakili.Epuka matumizi ya pombe kupita kiasi na tumbaku kwani vitu hivi vina madhara katika moyo na mishipa ya damu. Ugonjwa wa moyo huweza kumpata mtu yeyote bila kujali umri, na katika siku za karibuni mtindo wa maisha umewafanya watu wengi kupata maradhi haya kutokana na ulaji holela wa mlo usiozingatia afya na kuacha kufanya mazoezi