
KWA mujibu wa ripoti ya Human Rights Watch, maandamano ya Januari 2001 yaliondoka na roho za waandamanaji 35 katika kisiwa cha Pemba huko Zanzibar ambao walikuwa ni wafuasi wa chama kikuu cha upinzani kwa wakati huo; CUF; waliingia barabarani kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2000.
Vikosi vya usalama vya Tanzania vikiongozwa na Jeshi la Polisi viliyazima maandamano hayo kwa risasi za moto na kusababisha vifo, majeruhi na wakimbizi, jambo ambalo lilimsikitisha na kumtia doa Rais Mstaafu Hayati Benjamin Mkapa kwa kuwa alikuwa madarakani tukio lilipotokea na amekiri kwenye kitabu cha historia ya maisha yake.
Rais Amani Abeid Karume, Rais wa awamu ya nane wa Zanzibar na Maalim Seif Sharif Hamad, Novemba 5, 2009, walikutana kutia saini maridhiano ya kuundwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) baada ya majadiliano.
Kuibuka kwa makubaliano ya kiungwana mwaka 2009 ilikua ni furaha kubwa kwa Wazanzibari wapendao amani na maendeleo.
Kamati ya maridhiano chini ya Mwenyekiti, marehemu Hassan Nassor Moyo ikiwa na wajumbe kutoka CCM na CUF, walikaa na kuyapatia muafaka mizozo ya kisiasa ya visiwa hivyo.
Makubaliano haya yalikuja kufahamika kama Maridhiano kwa kizungu reconciliation ambapo mwishoni mwa Januari, 2010 kuliletwa hoja binafsi na aliyekuwa Mwakilishi wa Jimbo la Magogoni (CUF), Abubakar Khamis Bakari kwenye Baraza la Wawakilishi, ilipendekeza marekebisho ya Katiba ya Zanzibar ya 1984 ili kuwepo na Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).
Hoja hii pia ilipendekeza kuundwa kwa nafasi mbili za Makamu wa Rais ili awepo wa kwanza na wa pili na kugawanywa kwa nafasi za uwaziri kwenye Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) baina ya vyama viwili vitakavyopata kura nyingi kwenye uchaguzi mkuu.
Hoja hii ilichangia katika kuweka wazi kwamba Zanzibar ni moja wapo ya nchi mbili kwenye Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hii ilikidhi haja ya Wazanzibari wengi walioona kwamba nchi yao imemezwa na Tanganyika, kama wazanzibari wanavyosema.
Wazanzibari walipiga kura ya maoni Julai 2010 kuidhinisha makubaliano ya kugawana madaraka ya serikali kulingana na matokeo ya uchaguzi mkuu.
Matokeo ya kura ya maoni yalionyesha utayari wa Wazanzibari kuweka nyuma uadui na chuki uliotawala kwa muda mrefu.
Asilimia 66.4 walipiga kura ya kukubali Maridhiano na kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK). Kampeni na matokeo ya uchaguzi wa Oktoba 2010 pia yalidhihirisha dhana na Maridhiano.
Licha ya wasiwasi wa uhalali wa ushindi wa Dk. Ali Mohammed Shein wa CCM, dhana ya Maridhiano iliwalazimu CUF kukubali matokeo. Matokeo yalionyesha Dk. Shein alishinda kwa kura kiduchu kwa kupata asimilia 50.1 ya kura na Maalim Seif Shariff Hamad kupata asilimia 49.9.
Rais Shein alipokea nchi ambayo ilikua imesheheni ahadi ya matumaini, amani na mshikamano. Japo kugawanywa kwa madaraka kulikua kwenye ngazi ya uwaziri pekee, uhasama miongoni mwa watu ulipungua sana hasa baina ya wafuasi wa CCM na CUF kwani kabla ya maridhiano chuki, ubaguzi na fitna zilitawala nchi nzima.
Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete mwishoni mwa mwaka 2010 alihutubia taifa kuhusiana na masuala mbalimbali na aliainisha umuhimu wa katiba mpya ya nchi itakapokuwa inatimiza miaka 50 ya Uhuru (Uhuru wa Tanganyika) mwaka 2011. Mojawapo ya mambo ambayo alisema katiba mpya itatatua mikwaruzo katika muungano.
Mchakato wa kupokea maoni ya wananchi kupitia Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya uongozi wa Jaji Joseph Warioba kulianza kuchafua hali ya hewa visiwani Zanzibar. Mihemko na tofauti za vyama viwili vikuu vya CCM na CUF vilianza kuonekana tena.
Licha ya kasoro zilizokuwa katika muundo wa SUK na zaidi nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais katika serikali hiyo, kulikuwa na maelewano na kuheshimiana.
Katika mchakato wa kukusanya maoni, hususan kwenye suala nyeti la muundo wa muungano, vyama hivi viwili vilitofautiana. Wakati CCM walitaka mfumo wa serikali mbili kuendelea, CUF kilipendekeza muungano wa mkataba. Katika kipindi hiki tuliona kuibuka kwa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu (Jumiki) maarufu kama Uamsho.
Kikundi hiki, kupitia mihadhara kilizungumzia masuala mbalimbali likiwemo suala tata la utaifa wa Zanzibar, jambo ambalo liliwagawa zaidi Wazanzibari.
Rais Kikwete mwishoni mwa mwaka 2013, alitangaza wajumbe watakaoelekea Dodoma kwenye Bunge Maalamu la Katiba (BMK) kujadili mapendekezo ya Katiba Mpya (Rasimu ya Warioba).
Wajumbe hawa walikuwa ni pamoja na wajumbe wote wa Baraza la Wawakilishi, Wabunge, na wajumbe wateule waliowakilisha asasi mbalimbali. Mkutano wa Dodoma tulianza kuona migawanyiko ambayo ilichangia kuyumba kwa dhana ya Maridhiano ya Zanzibar.
Mchakato mzima kwenye BMK ulisheheni vituko, na hatimaye maoni ya wananchi kutupiliwa mbali baada ya kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kutoka nje ya Bunge na kususia hivyo dhana ya Maridhiano ilikuwa imekufa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Katika hatua ambayo haitawahi kusaulika, ni aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salum Jecha, alipofuta uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 bila kufuata Katiba huku matokeo ya majimbo 31 kati ya 54 yakiwa yamekwishatangazwa, maridhiano yakasahaulika.
MAKALA; ELVAN STAMBULI, UWAZI

