The House of Favourite Newspapers

Fahamu CPR Huduma Iliyookoa Maisha ya Christian Eriksen

0

 

MASHABIKI wa kandanda wiki iliyopita walipatwa na huzuni baada ya mchezaji wa timu ya taifa ya Denmark, Christian Eriksen kupata mshtuko wa moyo ‘cardiac arrest’ na kuanguka uwanjani akiwa anachezea nchi yake dhidi ya Finland katika mechi za kuwania kombe la Euro 2020.

 

Mchezaji huyo ambaye pia anachezea klabu ya Inter Millan ya nchini Italia nusura apoteze maisha iwapo asingepatiwa huduma ya kufufua moyo na mapafu viweze kufanya kazi tena yaani CPR.

 

Kwa mujibu wa Daktari wa timu yake, Morten Boesen alisema “Eriksen alikuwa amepoteza fahamu kabisa. Tukampatia huduma ya kwanza ya kuhuisha moyo na mapafu (CPR) ili moyo uanze tena kufanya kazi, alikuwa amepata mshtuko wa moyo,” Boesen alisema.

 

CPR NI NINI

Kwa mujibu wa Dk. Sadick Sizya kutoka Jukwaa la Afya Mtandaoni(VOH) anasema CPR ni kifupisho cha neno “Cardiopulmonary resuscitation” ikiwa na maana ya kufufua moyo na mapafu viweze kufanya kazi. Ni kitendo cha kubana kifua ili kuweza kurejesha mapigo ya moyo kwa mtu ambaye amepatwa na mshituko wa moyo.

 

CPR inakazi mbalimbali na inawezesha kutoa msaada wa hali ya juu kuliko inavyofikiriwa. CPR inafanya kazi zaidi ya “kuwezesha moyo kusukuma damu.” CPR ni huduma ya kwanza inayowezesha kupelekwa kwa hewa safi ya oxygen kwenye ubongo na viungo vingine muhimu hadi mgonjwa atakapopata matibabu rasimi.

 

Je unajua kuwa 75% ya matukio yote ya mshtuko wa moyo hutokea nyumbani? CPR inampa mtu nafasi maradufu ya kumuokoa mara apatapo shambulio la mshtuko wa moyo.

 

JIFUNZE KUFANYA CPR

CPR inaokoa maisha ndio maana ni muhimu kila mmoja kujifunza mbinu hii.

Weka kisigino cha mkono wako kwenye mfupa wa kifua katikati ya kifua cha mtu huyo. Weka mkono wako mwingine juu ya mkono wako wa kwanza na unganisha vidole vyako. Jiweke na mabega yako juu ya mikono yako.

 

Kwa kutumia uzito wa mwili wako (sio mikono yako tu), bonyeza moja kwa moja chini kwa 5cm hadi 6cm (2 hadi 2.5 inches) kwenye kifua cha mgonjwa, bonyeza na kuachia ‘compression’ ili kuruhusu kifua kurudi katika nafasi yake ya asili.

 

Rudia compressions hizi mara 100 hadi 120 mara kwa dakika hadi ambulensi itakapokuja. Kila baada ya compressions za kifua 30, toa pumzi za uokoaji kwa mtu huyo.

Stori: Gabriel Mushi

 

Leave A Reply