The House of Favourite Newspapers

FAHAMU DALILI ZA HATARI KIPINDI CHA UJAUZITO

KUNA baadhi ya dalili ambazo mjamzito akiziona zinaashiria tatizo hivyo leo tutajadili kwa kifui dalili hizo tukiwa na imani kwamba zitamsaidia msomaji wetu.  Dalili zifuatazo ni muhimu kuzipa uzito wake na kuzifuatilia kwa makini zikitokea kwa sababu ni za hatari kwa mjamzito. Kama ukizipata dalili hizi ni vyema kuwasiliana na mtaalamu wa afya au daktari wako au kituo cha kliniki ya wajawazito unachohudumiwa haraka iwezekanavyo.

KUTOKWA DAMU

Matone au kutokwa na damu kidogo bila maumivu ni kawaida kipindi cha mwanzo cha ujauzito. Inawezekana ni kuvuja kwa damu kunakosababishwa na zile homoni zinazouongoza mzunguko wako wa hedhi ziliendelea kutolewa kwa nguvu ya ziada na kusababisha kuvuja kwa damu kidogo. Usiwe na wasiwasi kuhusu aina hii ya kutokwa damu, kwani hali hii huondoka yenyewe na si rahisi kumdhuru mtoto wako.

Pamoja na hilo, ni vyema kuwasiliana na mkunga au daktari wako kama utatokwa na damu ukeni katika hatua yoyote ya ujauzito wako. Inaweza ikawa inamaanisha kuna tatizo kubwa kwenye ujauzito wako. Ukitokwa na damu pamoja na maumivu makali ya muda mrefu upande mmoja wa tumbo lako inaweza ikawa ni dalili ya mimba kuwa nje ya mji wa mimba au kutokwa kwa damu kwingi, ikiungana na maumivu ya muda mrefu ya mgongo au tumbo la chini inaweza kuwa ni dalili ya kutoka kwa mimba.

MAUMIVU YA TUMBO

Maumivu makali au vichomi katikati au juu kidogo ya tumbo, yakiambatana na kchefuchefu na kutapika, inaweza kumaanisha kitu kimoja kati ya vifuatavyo. Unaweza ukawa na kuvimbiwa kulikopitiliza, kiungulia au tumbo kuchafuka.

Kama upo kwenye miezi mitatu hadi sita ya ujauzito wako, hii inaweza kuashiria ni presha ya mimba ya awali. Hii ni dalili hatari na itahitaji matibabu ya haraka. Maumivu makali upande mmoja au pande zote kwenye tumbo lako la chini yanahitaji uchunguzi kugundua kama sio kitu cha kushtua.

Kwa kiwango cha chini kabisa inaweza pia ikawa ni dalili za mimba kutungwa nje ya mji wa mimba, mimba kutoka, uchungu uliowahi, uvimbe kwenye kizazi – uliovunjika na kuanza kuvuja damu kwa ndani yake na kuachia kwa kondo la nyuma kitaalamu huitwa placenta.

HOMA

Kama una ujauzito na una homa ya jotoridi zaidi ya digrii 37.5c, na bila dalili za mafua, ni vyema kumuona daktari siku hiyohiyo. Kama jotoridi ni zaidi ya nyuzi joto 39c wasiliana au fika kwa daktari wakati haraka kwani inawezekana umepata maambukizi, akigundua hilo atakuandikia dawa za kupambana na bakteria na kukushauri upate mapumziko.

KUTOONA VIZURI

Kama una kizunguzungu au macho kutoona vizuri, kuwa na ukungu au giza ukiwa mjamzito ni vema umuone daktari haraka hasa kama ni katika miezi mitatu hadi sita ya ujauzito wako. Matatizo haya kwenye mfumo wa kuona yanaweza yakawa ni dalili za presha ya mimba ya awali kitaalamu huitwa Pre-eclampsia.

KUVIMBA MWILI

Kuvimba au kuumuka (oedema) kwenye mikono, uso, macho ni kawaida mwishoni mwa ujauzito. Mara nyingi sio kitu cha kuleta wasiwasi. Lakini kama kuvimba huku ni kukubwa na kumetokea ghafla, kukiambatana na kichwa kuuma na matatizo ya kuona kwako, inawezekana ikawa ni presha ya mimba ya awali (pre-eclampsia). Kama utaona dalili yoyote kati ya hizi wasiliana na daktari bila kuchelewa.

KUUMWA KICHWA

Kama maumivu makali ya kichwa yanaendelea kwa masaa mawili hadi matatu, na pia una matatizo ya kuona kwako na kuvimba sana kwa mwili wako, inawezekana ukawa na presha ya mimba ya awali (pre-eclampsia). Kama presha ya mimba ya awali ikitokea, mara nyingi huwa ni katika nusu ya mwisho ya ujauzito wako au punde tu baada ya kujifungua.

USHAURI

Mjamzito uonapo dalili hizi tulizozitaja ni vema haraka sana ukamuona daktari lakini pia kama unatoka damu ghafla kusikoambatana na maumivu yoyote, wahi haraka ukaonane na daktari wako.

PAMOJA na hilo, ni vyema kuwasiliana na mkunga au daktari wako kama utatokwa na damu ukeni katika hatua yoyote ya ujauzito wako  Dk. Marise anapatikana Marise Dispensary, njia panda ya Mabibo mkabala na kituo cha mafuta.  Simu: 0713 252394

Comments are closed.