The House of Favourite Newspapers

FAHAMU HATARI YA UGONJWA WA HOMA YA INI

KUTOKANA na umuhimu wa kuwaelimisha watu kuhusu ugonjwa wa homa ya ini, nimeona vema kurudia kuandika kuhusu maradhi haya ili kuokoa na ikiwezekana kupata kinga na kujihadhari zaidi ili kuukwepa.

Ugonjwa wa homa ya ini ni ugonjwa unaoambukizwa kwa njia ya virusi ambavyo vikishaingia mwilini, hushambulia ini kabla ya kugeuka kuwa sugu.

 

Virusi hivyo vinaitwa ‘HBV’ ukiwa ni ufupisho wa kitaalam ‘Hepatitis B Virus.’ Ni virusi vinavyosambazwa kwa njia ya damu au majimaji mengine ya mwilini, kama vile mate au jasho na takwimu za kitafiti zinaeleza kuwa takriba watu 1,000,000 wanapoteza maisha duniani kote kila mwaka, kutokana na ugonjwa huo.

Ni ugonjwa unaohitaji tahadhari, kwani kuchelewa kwake kuutibu kunazaa balaa kubwa. Inapokuwa mgonjwa hajatibiwa, hutengeneza uvimbe katika ini na kusababisha kansa ya ini na baadaye inaishia katika kifo.

 

UNAVYOAMBUKIZWA

Virusi vya HBV vimewekwa katika hatari kubwa zaidi za kiafya duniani. Maambukzi yake huwa ni kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto wakati wa kuzaliwa.

Pia inaweza kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine, hususan katika kipindi cha utotoni.

Kama ulivyo Ukimwi, virusi vya homa ya ini pia huambukizwa kwa njia ya kujamiiana, mate, jasho na mwingiliano wowote ule wa damu.Pia kuna baadhi ya mambo kama vile kuchangia vitu vya ncha kali, miswaki, taulo na ama kubadilishana nguo au kukumbatiana wakati wahusika wanatokwa jasho.

 

Ugonjwa wa homa ya ini ni miongoni mwa magonjwa hatari, ambayo kwa mujibu wa tovuti ya serikali, imeelekezewa jicho la pekee katika kupigana nayo.

Kitaalamu, kama tulivyoona hapo juu, homa ya ini inatokana na virusi vinavyoitwa ‘Hepatitis B’ vyenye kawaida ya kuwapata

watu wa rika zote, lakini watoto wenye umri chini ya miaka mitano ndiyo wanatajwa kuwa wathirika zaidi.

 

DALILI ZAKE

Miongoni mwa dalili za ugonjwa huo ni: Mafua, kuumwa kichwa kunakoenda na uchovu wa mwili ukiwa na homa kali. Athari zingine ni mgonjwa anapoteza hamu ya kula na anatawaliwa na kichefuchefu, huku wakati mwingine anataka kutapika.

Hilo linaendana na mgonjwa kupatwa na maumivu ya tumbo na kuharisha. Hiyo ni hali inayomkuta mgonjwa baada ya siku tatu hadi nne baada ya kupata maambukizi.

Katika sehemu za wazi za mwili, dalili zinazotawala ni macho, ngozi na viganja hubadilika na kuwa rangi ya njano.

Dalili zingine ni mwili wa mgonjwa kuwa dhaifu na anapungukiwa uzito, kinyesi cha mgonjwa kinakuwa na mwelekeo wa rangi nyeupe na anajisaidia mkojo mweusi.

 

KINGA, TIBA NA ATHARI

Mtoto anayeugua homa ya ini, hata anapopona hupatwa anabakiwa na athari ya kusinyaa ini anapokuwa mkubwa, hatua inayoishia kwenye hatari ya kifo.

Ili kujikinga, kuna malekezo ya kitaalaam kama mosi ni mhusika anapaswa kupewa chanjo inayoenda sambamba na zile zinazohusu magonjwa ya donda koo, kifaduro, pepopunda, homa ya uti wa mgongo na kichomi.

Chanjo hiyo inayotibu magonjwa hayo, kitaalamu inaitwa ‘DTP-HepB-Hib’ au ‘Pentavelent.’

 

Chanjo hiyo inatolewa kwa kufuata ratiba maalum inayoanzia umri wa wiki sita; chanjo ya pili ni anapokuwa na umri wiki 10; na ya tatu anapofikia wiki 14

Kwa bahati mbaya, licha ya kuwapo kinga ya maradhi hayo, tiba yake bado haijapatikana na kinachofanyika kwa mgonjwa ni kumpatia huduma ya kutuliza makali ya dalili za ugonjwa.

 

USHAURI

Ugonjwa wa homa ya ini hukingwa kwa chanjo. Mpeleke mtoto katika kituo cha huduma za afya akapate chanjo.

Hakikisha mtoto amekamilisha dozi tatu za chanjo kwa utaratibu uliowekwa, ili apate kinga kamili. Epuka njia zote zinazoweza kusababisha maambukizi,” inafafanua tovuti ya serikali.

 

Ugonjwa wa homa ya ini ni hatari zaidi ya Ukimwi. Hakikisha mtoto anapata chanjo ya kuzuia ugonjwa wa homa ya ini.

Watu takriban 1,000,000 wanapoteza maisha duniani kote kutokana na ugonjwa wa homa ya ini. Ugonjwa huu kama haujatibiwa, hutengeneza uvimbe katika ini na kusababisha kansa ya ini na baadaye kifo.

 

Tafiti za kitaalamu zinaonyesha kuwa virusi hivyo ni hatari kuliko hata vya Ukimwi, kwa sababu vinaweza kuishi nje ya mwili wa binadamu (yaani nje ya mfumo wa damu) kwa siku saba.

Virusi vya Ukimwi (VVU) havina uwezo wa kuishi nje ya mfumo wa damu hata kwa dakika moja.Inapokua mwilini

kwa binadamu, kuna hatari ya mgonjwa kuambukizwa kupitia jasho.

Kwa wastani kirusi cha HBV ( kinachosababisha homa ya ini) kikishaingia mwilini, hupevuka ndani ya siku 75. Hata hivyo, upo uwezekano wa kupevuka kati ya siku 30 hadi 180.

 

Ndani ya siku 30 mpaka 60 mtu mwenye HBV anaweza kugundulika ikiwa atapimwa. Mtu mwenye homa ya ini ana wastani mdogo wa kuishi kuliko mwenye Ukimwi. Kwa maana hiyo, mwenye maambukizi ya virusi vya homa ya ini hufariki dunia kuliko mwenye VVU.

Hatari nyingine kwa baadhi ya wagonjwa kutooyesha dalili, jambo linalohatarisha afya ya wengi, kwani wanakosa tahadhari dhidi ya mgonjwa.

Watu wengi hawaonyeshi dalili yoyote. Kwa maana hiyo, mtu anaweza kuishi na HBV na kusababisha maambukizi kwa wengine bila kugundulika. Hata hivyo, watu wengine husumbuliwa na homa kali na dalili ambazo hudumu kwa wiki kadhaa.

 

HATARI ILIKOJIFICHA

Kati ya 80 na 90 ya watoto wachanga wanaambukizwa Homa ya Ini katika umri kati ya kuzaliwa na mwaka mmoja.

Ni maradhi yenye mwenendo wa kuambukiza katika umri kati ya mtoto anapozaliwa na mwaka mmoja, kati ya asilimia 30 na 50 ya watoto wanaomabukizwa Homa ya Ini kabla ya kufikisha umri wa miaka sita, hufariki.

 

Pia asilimia 90 ya watu wazima wanaopata maradhi hayo, tatizo hilo hutoweka ndani ya miezi sita, kutokana na athari hizo kuelemewa na uimara wa ini. Asilimia tano wa wagonjwa ndio wanaofariki.

Katika mchanganuo huo wa kitaalam, asilimia kati ya 15 na 25 ya watu wazima waliowahi kupata maambukizi hayo utotoni, nao hufariki.

Itaendelea wiki ijayo.

Na Dk. Marise Richard

Dk. Marise anapatikana Marise Dispensary, njia panda ya Mabibo mkabala na kituo cha mafuta. Simu: 0743 228 925

Comments are closed.