The House of Favourite Newspapers

FAHAMU HATARI ZA KIAFYA KWA WAJAWAZITO

 UJAUZITO unachangia mabadiliko mbalimbali ya mwili tangu mwezi wa kwanza hadi mwanamke anapojifungua. Katika kipindi chote za kulea mimba, mjamzito anakabiliwa na mabadiliko tofauti ya kiafya yanayotokana na hali aliyonayo.  Katika kipindi hiki, ujazo wa damu ya mwanamke huongezeka ingawa kwa wachache hutokea ikapungua, kiwambo cha mbavu hutanuka na mabadiliko ya mfumo wa homoni hutokea ambayo husababisha matatizo mbalimbali kiafya japo ni ya kawaida ingawa hayatakiwi kufumbiwa macho.

Hivyo, ni vyema kwa mjamzito kuwa karibu na huduma za afya badala ya kusubiri hadi siku ya kuhudhuria kiliniki au muda wa kujifungua unapokaribia. Kuhudhuria hospitali mara kwa mara husaidia kuzigundua mapema dalili zinazoashiria tatizo linaloweza kumuathiri mama na mtoto aliye tumboni. Hebu tuyaangalie baadhi ya matatizo yanayohitaji umakini katika kipindi cha ujauzito.

SHINIKIZO LA JUU LA DAMU

Shinikizo la juu la damu ambalo kitaalamu huitwa preeclampsia hutokea ghafla kwenye wiki ya 20 ya ujauzito. Hali hii ikidumu kwa siku chache inaweza kusababisha kufeli kwa figo, kutetemeka mara kwa mara hata kama si wakati wa baridi, kutengeneza jeraha kwenye ini na kusababisha matatizo mengine kwenye mfumo wa upumuaji hivyo kuhatarisha maisha ya mjamzito. Mjamzito anashauriwa kupunguza ulaji wa vyakula vyenye mafuta mengi na kufanya mazoezi ya mwili ujauzito unapofikisha miezi mitano na kuendelea kujiepusha na shinikizo la juu la damu linaloweza kujitokeza katika kipindi hiki.

UGONJWA WA KISUKARI

Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) za hivi karibuni zinaonyesha kisukari huwapata karibu asilimia 15 ya wajawazito wote. Hali hii hutokea baada ya kondo la nyuma au plasenta ambayo ni mfuko wa unaopitisha chakula na mahitaji mengine kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, kuzalisha homoni nyingi zinazozuia insulini kuratibu kiwango cha sukari mwilini.

Kwa kawaida, insulini hurekebisha kiasi cha sukari inayoingia mwilini hivyo isipofanyakazi kama inavyotakiwa sukari huendelea kubaki kwenye damu na kumuathiri mtoto aliye tumboni. Mwanamke anashauriwa kutokula vyakula vilivyosindikwa na vya sukari nyingi, kufanya mazoezi mara kwa mara na kufanya vipimo angalau mara moja kwa mwezi kuanzia miezi mitatu ya ujauzito wake ili kudhibiti matatizo yanayoweza kujitokeza.

MAGONJWA YA MOYO

Mfumo mzima wa moyo wa mwanamke hubadilika wakati wa ujauzito. Ujazo wa damu hubadilika pia, mapigo yake huongezeka na shinikizo la damu hupanda.

Mara nyingi mabadiliko haya huwa hayana madhara na wanawake wenye historia ya matatizo ya moyo wakati wa ujauzito wanaweza kuathirika wao na watoto walio tumboni. Kati ya asilimia moja hadi tatu ya wajawazito hupata matatizo haya kutokana.Japo kiwango hicho ni kidogo lakini ni kupata ushauri na vipimo vya mara kwa mara ili kuepukana na madhara yanayotokana na mabadiliko haya.

UPUNGUFU WA DAMU

Upungufu wa damu ni tatizo linalojitokeza wakati wa ujauzito kutokana na upungufu wa seli nyekundu za damu. Madini ya chuma ni kitu muhimu sana ili kusaidia uzalishaji wa seli nyekundu za damu lakini wanawake wengi hawana uhifadhi wa kutosha wa madini chuma mwilini kutokana na sababu za kimaumbile. Mtoto pia anahitaji kiasi fulani cha madini ya chuma.

Tatizo hili linaweza kusababisha matatizo mengine kama vile kujifungua kabla ya wakati au kuzaa mtoto mwenye uzito mdogo na matatizo ya ukuaji wa mtoto baada ya kuzaliwa. Mjamzito anashauriwa kula vyakula vinavyoongeza damu kwa wingi kama vile mboga za majani, matunda na nyama nyekundu na kutumia dawa za kuongeza madini ya chuma kuanzia miezi mitatu ya ujauzito hadi wakati wa kujifungua ili kuepuka anemia.

MAUMIVU YA MGONGO

Maumivu ya mgongo na kiuno linawapata karibu wanawake wote kwa nyakati toauti. Wajawazito wengi hupata maumivu ya mgongo na kiuno mara nyingi kuanzia muhula wa tatu wa ujauzito yaani mwezi wa sita. Kwa baadhi tatizo hili huwaletea shida kiasi cha kushindwa kufanya shughuli nyingine. Hii ni kawaida kutokana na mabadiliko ya mwili na maumbile yanayotokea mwilini siku hadi siku wakati wa ujauzito. Kwa kipindi hiki mwanamke anashauriwa kupata muda mrefu wa kupumzika na anaweza kutumia dawa za kutuliza maumivu lakini ni lazima matumizi ya dawa hizi yaambatane na ushauri wa daktari.

Wajawazito wengi hupendelea kula vitu ambayo kwa mtu wa kawaida hawezi kuvila. Ulaji wa udongo, vitu vyenye asidi na ukakasi mwingi hususan matunda mabichi kama vile maembe malimau na vitu vingine vichachu umekithiri sana kwa wajawazito kutokana na mabadiliko ya mwili yanayosababisha kuvurugika kwa ladha midomoni.

Tabia hii inawaweka hatarini wajawazito kupata ugonjwa unaoitwa pica. Huenda ni ugonjwa ambao wengi hawaufahamu ila unaotokana na ulaji wa vitu ambavyo havipo kwenye kundi la chakula ambalo mtu anapaswa kutumia kama mlo.

Wajawazito wapo hatarini zaidi kupata ugonjwa huu kutokana na tabia ya kula vitu ambavyo haviendani na mahitaji ya lishe. Wajawazito wanashauriwa kuacha kula vitu ambavyo haviendani na lishe ya mjamzito kuepuka magonjwa kama pica ambayo yanaweza kuathiri mfumo wa chakula hata kusababisha kuzaa mtoto njiti.

MAUMIVU YA KICHWA

Wajawazito wengi hupata maumivu ya kichwa mara kwa mara hasa katika miezi mitano ya kwanza ya ujauzito yanayoisha mwanzo wa muhula wa tatu, yaani mwanzoni mwa mwezi wa sita wa ujauzito. Maumivu haya ni kawaida kutokana na mabadiliko yanayojitokeza kwenye mfumo wa homoni na mjamzito anaweza kuyakabili kwa kutumia dawa za kupunguza maumivu baada ya kupata ushauri wa daktari.

Wakati mwingine maumivu haya yakidumu kwa zaidi ya miezi sita mfululizo yanaweza kuashiria tatizo jingine kubwa zaidi ya kichwa chenyewe. Ni muhimu sana kwa wakati huu kupata msaada wa kitabibu ili kubaini tatizo kwa sababu maumivu ya kichwa anayoyapata mjamzito yakidumu kwa muda mrefu yanaweza kuashiria matatizo kama vile uvimbe au kuvuja damu ndani ya ubongo.

Comments are closed.