The House of Favourite Newspapers

Fahamu kinachosababisha kiharusi (Stroke)

0

stroke_hem_isoKiharusi kinampata binadamu baada ya eneo la ubongo kukosa damu kwa saa 24 ama zaidi au kunapotokea kizuizi cha damu au mishipa ya damu kushindwa kusafirisha damu au mshipa huo unapopasuka.

Kiharusi kimegawanyika katika aina kuu mbili kulingana na jinsi kinavyotokea, kwanza ni:
1. Kiharusi cha kukosa hewa kwenye ubongo kitaalamu huitwa Ischemic Stroke.
Aina hii ya kiharusi hutokea iwapo usambazaji wa damu katika sehemu ya ubongo hupungua na kusababisha tishu za ubongo za eneo lililoathirika kushindwa kufanya kazi zake vizuri.

Hiki hutokea baada ya mshipa wa ateri kuziba kutokana na kuganda kwa damu, hali ambayo inasababisha damu isisafiri vyema na kuelekea kwenye ubongo.

Hali hiyo pia hufanya damu iliyoganda kuziba mishipa midogo ndani ya ubongo kitaalamu huitwa Cerebral Thrombosis au kipande cha damu kumeguka na kwenda kuziba mshipa wa damu kwenye ubongo yaani Cerebral Embolism.

Lakini tatizo hili linaweza kutokea pale damu inapoganda sehemu nyingine ya mwili na kusafiri hadi kwenye mishipa ya ateri, hivyo kusababisha damu kwenda kwenye ubongo kukwama.

Hata hivyo, tatizo hili linaweza kusababisha kitu kinachoitwa Lacunar Stroke, yaani vimirija vidogovidogo sana vya damu vilivyopo ndani ya ubongo, vinaziba.
Hapo sasa binadamu huwa anakumbwa na kiharusi kinachojulikana kitaalamu Lacunar Stroke japokuwa mara nyingi hii haiwaletei sana shida wagonjwa.

Ingawa kiharusi kinaweza kumkumba mtu yeyote lakini watu wazima wenye umri kuanzia miaka 40 kuendelea juu ndiyo hushambuliwa zaidi na maradhi hayo.
Wiki ijayo, tutaeleza tiba yake kwa undani zaidi nini cha kufanya.

Leave A Reply