Fahamu kirusi cha Ukimwi kinavyoishi mwilini

 ILI kuweza kuingia ndani ya seli za binadamu na kuzaliana, kirusi cha ugonjwa wa Ukimwi kifupi HIV hutumia kiasili cha CD4 kama njia ya kupita. Katika kufanikisha hilo, kuna hatua kuu sita katika mzunguko wake wa maisha. Baada ya mtu kupata maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) kwa njia yoyote ile na VVU kuingia ndani ya mzunguko wa damu wa mwanadamu, hatua ya kwanza katika mzunguko wa maisha wa HIV ni kunata na kujiunganisha na CD4.

HIV huanza maisha yake kwa kuunganisha ncha za proteini zilizojitokeza kwenye utando wake zijulikanazo kama gp120 kwenye vipokeo kitaalamu receptors vya CD4. Muunganiko huu wa CD4 na gp 120 hubadilisha kabisa umbo la gp120 hali ambayo huruhusu HIV kujipachika katika vipokeo visaidizi (co-receptors) vilivyoko kwenye utando wa juu wa seli ya binadamu.

Vipokeo hivi visaidizi hujulikana kama chemokine receptors CCR5 au CXCR. Kuhusu ni aina gani kati ya vipokeo hivi visaidizi hutumika wakati wa uambukizi wa HIV, inategemea ni aina gani ya seli nyeupe kati ya macrophage au T-helper cell inayoshambuliwa wakati huo.

Baada ya hapo, aina nyingine ya ncha za proteini zilizo kwenye utando wa nje wa HIV ziitwazo gp41 nazo hubadilika umbo lake na hivyo kuwezesha HIV kuachia aina nyingine ya protini inayoitwa fusion peptide kwenye seli nyeupe ya damu. Protini hii huwezesha utando wa juu wa HIV kuungana na utando (cell membrane) wa seli nyeupe inayoshambuliwa.

Hatua ya pili ni HIV kupenya na kuingia ndani ya seli nyeupe ya damu ya binadamu kitendo kinachojulikana kama Viral Penetration/Fusion. Kitendo cha kuungana kwa utando wa juu wa HIV na ule wa seli nyeupe ya damu husababisha kutokea kwa tundu katika utando wa seli nyeupe. Kitendo hiki huwezesha kibeba kinasaba cha HIV kusukumwa moja kwa moja mpaka ndani ya seli nyeupe ya damu ya binadamu kupitia kwenye tundu hilo.

Hatua ya tatu ni kujivua gamba kwa HIV. Hatua hii kwa jina lingine hujulikana kama uncoating. Kujivua gamba huku husaidia kuruhusu vinasaba vya HIV pamoja na vimeng’enyo muhimu kwa ajili ya kubadilisha vinasaba vya RNA kwenda DNA.

Hatua ya nne ni ubadilishaji wa RNA ya virusi kuwa DNA ya virusi kwa kutumia kimeng’enyo cha reverse transcriptase. Kitendo hiki hujulikana kitaalamu kama reverse transcription kwa sababu hutokea kinyume na vile kinavyotakiwa kutokea kwa viumbe hai wengine. Kwa kawaida, kitendo cha transcription hufanyika kwa kubadilisha DNA kuwa RNA na si kinyume kama chake.

Baada ya DNA hii ya virusi kutengenezwa ndani ya ute wa seli ya binadamu, hubadilishwa kuwa aina fulani ya RNA iitwayo messenger RNA, yenye uwezo wa kuamrisha seli kufanya kazi mbalimbali kulingana na mahitaji ya mwili. Kisha aina hii ya RNA yenye uzi mmoja hubadilishwa tena kuwa DNA ya virusi yenye nyuzi mbili. Matukio haya yote hufanyika ndani ya ute wa seli nyeupe ya damu.

Hatua ya tano huitwa integration. Baada ya HIV kufanikiwa kubadilisha RNA yake kuwa DNA, ni lazima sasa HIV aingize DNA yake hii mpya kwenye DNA ya seli ya binadamu ili aweze kuthibiti kikamilifu na kuamrisha matendo na kazi zote za seli nyeupe ya binadamu ili seli hiyo iweze kufanya inavyotaka HIV. Itaendelea…


Loading...

Toa comment