The House of Favourite Newspapers

Fahamu Kuhusu Virusi Vya Corona Na Ujauzito

0

KUNA mengi yasiyofahamika kuhusu madhara ya Virusi vya Corona kwa wajawazito na akina mama wanaonyonyesha. Lakini uelewa wa madhara ya virusi hivi utaongezeka kadiri muda unavyokwenda.

Kuwa mjamzito huleta wasiwasi na hali ya sintofahamu kwa mama wengi watarajiwa, hata kama kila kitu kinakwenda sawa.

 

Wanahitaji kuepuka aina fulani ya vyakula, mfano; samaki wasiopikwa vizuri na jibini laini. Hii ni kwa sababu miili yao inabadilika kwa kiasi kikubwa kila siku na utaratibu wake wa kawaida unaweza kuvurugika.

 

Taifa la Uingereza ni moja ya nchi ambazo hivi karibuni zimewahusisha wanawake wajawazito katika kundi la watu walio kwenye hatari kubwa ya kupata maambukizi haya.

Inashauriwa wanawake wajawazito kukaa mbali na mikusanyiko ya watu ili kupunguza nafasi za kupata Virusi vya Corona. Inaeleweka, wajawazito wengi na familia zao wana wasiwasi na wamechaganyikiwa kwa sababu ya ujio huu wa Corona.

 

Pamoja yote hayo, ukweli unabaki kuwa hatuna ufahamu wa kutosha kuhusu madhara ya virusi hivi vya Corona vinavyosababisha Ugonjwa wa COVID-19 kwa wajauzito. Kuwepo kwa ufahamu wa kutosha husaidia kuchukua hatua za uhakika.

 

Uwepo mdogo wa wanawake wajawazito waliopata maambukizi haya pamoja na ufahamu wa kutosha wa Virusi vya Corona kwa jumla utatusaidia kutoa ushauri wa ziada kwa wanawake wajawazito kuchukua tahadhari mapema.

 

Mwanzoni ilidhaniwa kipindi cha ujauzito kinga ya mwili ya mwanamke inadhoofika na kumfanya kuwa katika hatari ya kupata maambukizi. Hata hivyo, kama ilivyo vitu vingi vinavyohusiana na mwili wa binadamu ushahidi mpya unaonesha kuwa kinga ya mwili ya mjamzito hupanda kipindi cha ujauzito na wakati mwingine huwa ni ya kubadilikabadilika.

 

Mabadiliko haya ya kinga ya mwili kipindi cha ujauzito ni muhimu kwa ajili ya kumpa nafasi mtoto anayeendelea kukua katika hatua tofauti za ujauzito. Kwa mfano katika hatua za kwanza za ujauzito kinga ya mwili inabadilika ili kuruhusu upandikizaji katika mwili. Wakati mwingine mfumo wa kinga unahitaji kujirekebisha katika njia tofauti, mfano mzuri ni wakati mwili wa mwanamke unajiandaa kupata uchungu wa kujifungua.

 

Jambo la muhimu katika maelezo yote haya ni kwamba kuwa na mfumo wa kinga wenye kubadilikabadilika inakuweka kwenye hatari kubwa ya matatizo ya Virusi vya Corona kama vile shida katika upumuaji na hata homa ya mapafu (pneumonia).

 

Kitu cha kwanza cha kutiliwa mkazo ni wanawake wajawazito waendelee kuhudhuria kliniki katika hospitali isipokuwa kama wameambiwa vinginevyo na mkunga au daktari wao.

 

Kwa sasa hakuna sababu ya kubadilisha mpango wako wa kujifungua, kama uliandaa hapo awali. Mpango wa kujifungua unahusisha mahali unapotarajia kujifungulia (hospitali, zahanati, kituo cha afya au nyumbani) na aina gani ya dawa za maumivu unatarajia kupata.

 

Lakini ikiwa umeonekana na dalili zinazoashiria maambukizi ya Virusi vya Corona, kama kikohozi kikavu au joto kubwa la mwili, kubanwa kifua na kupumua kwa shida, ni lazima ujitenge (self-isolation) na wasiliana na daktari au mkunga wako haraka.

Vilevile, kwa wanawake wajawazito wenye matatizo mengine ya kiafya wanahitaji kuwa makini zaidi na kukaa mbali na mikusanyiko ya watu ikiwezekana kufikiria kujitenga (self-isolation) kipindi cha ujauzito.

 

Wanawake waliopata ugonjwa wa kisukari, aina ya ugonjwa wa kisukari ambayo ni matokeo ya ujauzito ijulikanayo kama ugonjwa wa kisukari kipindi cha ujauzito (gestational diabetes), wanatakiwa kuchukua tahadhari na kupunguza migusano na watu.

 

Kuwa mgonjwa wa kisukari wakati wa ujauzito ni kundi la hatari hata bila kupata Virusi vya Corona kwa sababu ugonjwa huu wa kisukari unaongeza ugumu wakati wa ujauzito na kujifungua. Zaidi ya hapo, viwango vikubwa vya sukari katika damu kwa muda mrefu bila kutibiwa na kuangaliwa vizuri vinaweza kudhoofisha mfumo wa kinga zaidi.

Kutokana na mfumo wa kinga unaobadilika kila hatua wakati wa ujauzito ni vizuri wanawake wasio na matatizo ya kiafya kuchukua tahadhari na kukaa mbali na watu pale inapobidi.

 

Kama ilivyo wajawazito wengi wanaishi na wenzi wao au mara nyingine mtoto au watoto wao wengine, ushauri huu ni vizuri kufuatwa ili kupunguza nafasi ya kuweka afya ya mama mjamzito katika hatari ya kupata maambukizi ya Virusi vya Corona.

 

Tahadhari hizo ni pamoja na kufanya kazi ukiwa nyumbani kwa wale wanaoweza, kataa mgusano wa aina yoyote na watu na epuka sehemu za mikusanyiko.

 

Mwisho kabisa, ili kuwasaidia wajawazito kuwa na ujauzito wenye afya na kinga ya mwili nzuri katika kipindi hiki. Ni vizuri kuzingatia mlo bora wenye madini chuma kwa wingi (kama mboga za majani zenye kijani kilichokolea, samaki na mayai) na madini ya foliki ambayo yanapatikana kwenye maharage, kunde, maharage ya kijani n.k. Bila kusahau vidonge vya vitamini vya kila siku ulivyoandikiwa na daktari wako vinasaidia pia. Kwa ushauri; wasiliana nami kwa namba hiyo juu.

Leave A Reply