FAHAMU MADHARA YA PUMU KWA WAJAWAZITO

TAFITI kadhaa zimeonesha kuwa takribani theluthi moja ya wajawazito wenye pumu hupata nafuu kipindi cha ujauzito, theluthi nyingine hupata matatizo kipindi hiki na theluthi iliyobakia huwa na hali ya kawaida kama kabla ya ujauzito.  Kwa kawaida dalili za pumu hujirudia kama awali miezi mitatu baada ya kujifungua. Dalili za pumu kwa mjamzito zinaweza kuwa mbaya zaidi kuanzia wiki ya 24 hadi 36 (mwezi wa sita mpaka wa nane). Ni mara chache sana mjamzito anapata shambulizi la pumu wakati wa kujifungua.

Ni asilimia 10 tu ya wajawazito wenye pumu wanaopata shambulizi la pumu wakati wa kujifungua. Baadhi ya dawa zinazotumika wakati wa ujauzito na baada ya kujifungua huongeza madhara ya pumu, hivyo ni vizuri kumueleza daktari kwamba una pumu kabla ya kupewa dawa. Aidha, si vyema kunywa dawa kwa mazoea.

Wanawake wenye pumu isiyoweza kudhibitiwa kipindi cha ujauzito hupata madhara ya kuzaa mtoto njiti (premature baby), kuzaa mtoto mwenye uzito mdogo, kifafa cha mimba, shinikizo la damu (Hypertension), na iwapo atapata shambulizi hatari wakati wa ujauzito mtoto anaweza kufa kwa kukosa hewa ya oksijeni.

TIBA NA USHAURI

Kwa ujumla matibabu ya pumu hujumuisha kuepuka visababishi vya ugonjwa huu na matumizi ya madawa kwa walio na hali mbaya. Aidha, kwa wanaopata ugonjwa huu kwa sababu ya msongo wa mawazo hupewa ushauri nasaha kwa ajili ya kusaidia kutatua matatizo yanayowakabili.

Vilevile inashauriwa kwa wenye tatizo hili, kuwa na dawa karibu muda wote kwa ajili ya matumizi pindi shambulizi litakapotokea. Pia inashauriwa sana kuepuka mazingira na hali za baridi ambazo huweza kuchochea kutokea kwa shambulio la ugonjwa huu.

Matibabu ya kutumia dawa hujumuisha matumizi ya dawa za kusaidia kupunguza na kuondoa makohozi (expectorants), dawa zinazosaidia kutanua mirija ya hewa (bronchodilators), dawa za kuondoa mcharuko mwili kama vile cortisone ya drip (hasa wakati wa dharura) au nebulizer, na dawa za kuzuia mzio (antihistamine drugs).

Kwa wagonjwa wenye pumu ya ghafla na wenye hali mbaya (acute asthma) matibabu hujumuisha matumizi ya dawa za kutanua mirija ya hewa (bronchodilators) pamoja na kuongezewa hewa ya oksijeni, dawa za kutuliza mcharuko mwili (steroids) pamoja na dawa za kutuliza kukakamaa kwa misuli ya mwili (intravenous muscle relaxants).

Aidha kwa vile mara nyingi shambulizi hili linaweza kuwa la hatari sana, mgonjwa hulazwa hospitali na huongezewa hewa ya oksijeni, na kwa wagonjwa wasioweza kupumua kabisa, husaidiwa kufanya hivyo kwa kutumia mashine maalum iitwayo mechanical ventilator.

Kwa wagonjwa wenye pumu sugu, jambo la muhimu ni kuepuka visababishi vya pumu na kuendelea na matumizi ya dawa zinazosaidia katika kutanua mirija ya hewa. Kwa wagonjwa wanaopata mashambulizi ya mara kwa mara wanaweza kushauriwa na daktari kutumia dawa kadhaa zikiwemo zile zinazopunguza mcharuko mwili (mast cell inhibitors, inhaled steroids au oral steroids), pamoja na dawa za kutuliza kukakamaa kwa misuli ya mwili (muscle relaxants).

Aidha ni vema pia kutibiwa na kudhibiti kutokea kwa magonjwa yote yahusuyo mfumo wa hewa. Ni vema pia kuepuka matumizi ya dawa za jamii ya beta-blockers kwa wagonjwa wenye shinikizo la damu na ambao pia wana pumu.

Loading...

Toa comment