The House of Favourite Newspapers

FAHAMU MAMBO MUHIMU KUJADILIANA KABLA YA KUOANA

BOYFRIEND and Girlfriend ndiyo jina la kolamu, tukijadiliana mambo muhimu ambayo vijana walio kwenye urafiki, kabla ya kufikiria kuhusu uchumba na baadaye ndoa wanapaswa kuyajua. Wapo baadhi ya vijana, huingia kwenye uhusiano kichwa kichwa. Akishaona amempenda mvulana au msichana fulani, huishia hapo tu. Anawaza kuhusu ndoa. Siyo sahihi rafiki zangu. Lazima kuchunguza kwanza na kujadiliana kwa kina kuhusiana na mwelekeo wa maisha yenu yajayo na baadaye ndoa. Vijana wengi wamekuwa wakiwasiliana nami wakiuliza sana kuhusu uhalali wa kuoana katika imani za dini tofauti. Ni jambo lenye changamoto kubwa sana na limesababisha migogoro mara nyingi kwenye uhusiano wa vijana wengi.

Kutokana na uzito wake nimeona ni vyema nikaandika hapa mada hii, lakini yenye mwendelezo zaidi kuhusu pia suala la kabila na mila za makabila mbalimbali ili kukupa mwanga wa mwenzi unayetarajia kuingia naye kwenye ndoa. Kimsingi hayo ni kati ya mambo ya msingi zaidi kujadiliana na mwenzi wako mtarajiwa kabla ya kufikiria kuhusu ndoa.

VIPI KUHUSU DINI?

Inasemwa sana kuwa, mapenzi hayachagui dini, kabila, rangi wala kitu kingine chochote cha kufananisha. Inaweza kuwa sawa, lakini kwa wakati mwingine siyo sawa hususan kwenye suala la imani ya dini. Imani ni msingi wa maisha ya binadamu. Ni kile unachokiamini kimapokeo ambacho ni mwongozo sahihi wa maisha yako ya baadaye. Wakati mwingine mtu anaweza kubadili imani yake baada ya kuwa mtu mzima na huenda akapata mafundisho mapya ambayo yatamvutia na kuona ndiyo njia sahihi ya mwongozo wa safari yake hapa duniani.

Mwongozo huo ndiyo msingi. Kwa maneno mengine, kwa sababu kila dini ina msingi wa imani yake, ina miiko na taratibu zake, hutokea baadhi ya makatazo ya upande mmoja, upande wa pili ikawa halali. Ni sahihi zaidi kuoana mkiwa katika imani moja ya dini, tena mnaoabudu katika tawi moja – ni nzuri zaidi. Hii itasaidia wote kuwa na mafundisho yanayofanana juu ya taratibu za maisha kwa utashi wa dini.

NI SAHIHI KUOANA DINI TOFAUTI?

Kisheria inakubalika. Pamoja na kukubalika huko, kama nilivyozungumza katika kipengele kilichopita ni rahisi kusababisha msuguano na kushindwa kupata utatuzi mzuri wa kiimani hasa kwa sababu imani ndiyo kimbilio na msingi wa kwanza katika maisha ya binadamu.

Wengi ni mashahidi juu ya ndoa za Kiserikali, hazina uhakika wa kudumu. Mnaoana leo, ukiona mwenzako huelewani naye baada ya wiki moja inaweza kubatilishwa na talaka kutolewa mara moja. Hii ni tofauti na zile za imani za dini, maana kabla ya kufikiria suala la talaka kuna njia za mazungumzo – mafundisho na ushauri wa kiimani zaidi.

Imani nyingi zinasisitiza suala la upendo na kusamehe, wakati kwenye sheria huangaliwa kwenye matatizo na matakwa ya ninyi mnaoamua kutengana. Hata hivyo, ikiwa umezungumza na mwenzako, mmejadiliana mapema kuhusiana na ndoa yenu ya mseto, mnaweza kuoana. Muhimu ni kila mmoja kutoa nafasi kwa mwenzake ya kuabudu anapotaka kwa uhuru bila kuingiliwa.

Mbali na hayo, lazima kujadiliana kuhusu imani za watoto. Ama kuwe na mgawo wa kufuatwa kwenye imani au kuwaacha watoto huru kuchagua imani watakayopenda baada ya kuwa watu wazima. Hapo ndipo utakapokutana na changamoto; itawezekanaje mtoto akae hadi utu uzima bila kuwa na imani ya dini? Ni jambo la kutafakari kwa kina.

KUBADILI DINI KWA AJILI YA NDOA VIPI?

Hili limekuwa likizua migogoro mara nyingi sana kwenye uhusiano wa vijana wengi. Wameanza uhusiano bila kugusia kabisa suala la dini. Baada ya kuzoeana na kila mmoja kuridhishwa na mwenzake, wanakuja kugundua kuna kikwazo cha dini.

Hapa huanza kushawishiana mmoja wao (hasa msichana) abadili ili waweze kufunga ndoa. Kiukweli si sahihi na kuna athari nyingi ambazo mtu anaweza kuzipata kwa kubadilisha imani yake ili aoe/ aolewe. Wiki ijayo tutaendelea, USIKOSE!

Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Uhusiano anayeandikia Magazeti ya Global Publishers. Ameandika vitabu vingi, vikiwemo True Love, Let’s Talk About Love na Maisha ya Ndoa vinavyopatikana kwa oda. Kwa sasa anaandaa kitabu chake kipya cha SIRI ZA NDOA YENYE FURAHA kitakachotoka hivi karibuni.

Comments are closed.