The House of Favourite Newspapers

FAHAMU SABABU ZA FIGO KUSHINDWA KUFANYA KAZI!

FIGO ni viungo vilivyomo ndani ya mwili vyenye kazi ya kuchuja uchafu uliomo kwenye damu. Vinahusika pia na uratibu wa shinikizo la damu, madini yenye umeme ndani ya damu na uzalishaji wa chembe nyekundu za damu.  

 

Kati ya sababu nyingi za figo kushindwa kufanya kazi ni shinikizo la juu la damu na ugonjwa wa kisukari. Kwa takwimu inaonyesha kuwa zaidi ya nusu ya watu wazima wenye matatizo ya figo husababishwa na magonjwa hayo. Kwa kisukari; kama haujatibiwa ipasavyo, sukari itajijenga ndani ya damu na ikiwa nyingi huharibu seli hivyo hupunguza uwezo wa figo kuchuja uchafu.

 

Kuna aina mbili za kisukari, kwanza kisukari ambacho mwili unashindwa kuzalisha tezi inayomeng’enya sukari kwenye damu (insulin). Kisukari cha pili ni pale mwili unaposhindwa kutumia vizuri insulin inayozalishwa.

 

Kwa tatizo la shinikizo la juu la damu; ni pale kunapokuwa na shinikizo kubwa la damu kuliko ukubwa wa mishipa yake. Kama shinikizo hilo litaongezeka litasabisha ugonjwa wa moyo, mshtuko na ugonjwa sugu wa figo.

 

Sababu nyingine ni kuharibika kwa seli zinazohusika na uchujaji wa uchafu, hali inayosababisha kupungua kwa mkojo, kutokutolewa kwa protini katika mkojo na kuvimba kwa mikono na miguu. Nyingine ni magonjwa ya kurithi kama vile ‘Polycystic’ yaani vivimbe kutokea ndani ya figo hivyo kushindwa kufanya kazi. Magonjwa kama haya siyo ya kawaida lakini huanza wakati mtoto akiwa bado tumboni.

 

Dalili za kushindwa kwa figo ni pamoja na kuongezeka kwa uchafu ndani ya mwili ambao husababisha udhaifu, kuhema kwa shida, uchovu na kuchanganyikiwa. Kushindikana kuondolewa kwa kemikali ya potasiamu katika mirija ya damu husababisha mapigo ya moyo na kifo cha ghafla. Wakati mwingine dalili zinaweza zisijitokeze hata kama tatizo lipo.

 

Uchunguzi wa magonjwa ya figo hufanywa kwa kupima kemikali ya urea ya naitrojeni iliyomo kwenye damu na kuchunguza kiwango cha uchujaji wa uchafu (glomerular filtration rate -GFR). Kama matibabu yatakwenda vizuri figo inaweza kurudia katika hali yake ya kawaida.

 

Kujiepusha na shinikizo la damu na kujilinda na kisukari ni njia bora za kujilinda na magonjwa sugu ya figo. Kwa kawaida utendaji wa figo hupungua kwa jinsi umri unavyoongezeka.

Figo ikishindikana kabisa kutibika, kinachofanywa ni kuchuja uchafu kwa kutumia mashine maalumu (dialysis) au kupandikiza figo nyingine. Ingawa matibabu ya figo yameimarika, bado mtu anaweza kudumu na tatizo hilo kwa miaka 20 hadi 30. Asilimia 20 ya watu wanaotibiwa kwa dialysis huwa wamechelewa kugundua matatizo hayo kwa muda mrefu.

 

Baadhi ya matatizo ya figo yanaweza kutibika hadi kurejea kwenye hali yake ya kawaida. Kwa bahati mbaya magonjwa ya figo huendelea na figo zisiwezekane kabisa kurudia kwenye hali yake ya kawaida. Figo zina jukumu kubwa katika mwili, siyo tu kuchuja uchafu kwenye damu ili kuepukana nao, pia kuratibu madini yaliyomo ndani ya damu, shinikizo la damu na kuchochea uzalishaji wa chembechembe nyekundu za damu.

 

Figo huwa zinakaa karibu na tumbo mbele ya ukuta wa mgongo na ziko mbili kila upande wa uti wa mgongo. Zinapata damu kutoka kwenye mishipa ya ateri moja kwa moja kutoka kwenye mshipa mkuu wa aota na kuirudisha damu hiyo moja kwa moja kwa mishipa ya veini kwenda kwenye vena cava.

Figo zina uwezo wa kufuatilia kiwango cha umaji maji wa damu, kuongezeka kwa madini kama vile sodiamu na potasiamu na tindikali kwa mwili mzima. Huchuja uchafu wa vyakula vilivyochakatwa mwilini. Uchafu mkubwa unaochujwa mwilini ni pamoja na urea ya nitrojeni. Damu inaposhuka kwenye figo, vichocheo vyake huamua kiasi cha maji kiende kuwa mkojo kulingana na uwingi wa madini yaliyomo ndani ya damu.

Kwa mfano, kama mtu anaharisha au ameishiwa na maji kutokana na ugonjwa mwingine, figo huzuia maji yaliyopo yasiende kuwa mkojo na hapo mkojo huwa wa njano. Lakini kama maji yako mengi mwilini, mkojo huwa na msafi. Kazi hiyo hufanywa na homoni inayoitwa renin ambayo huzalishwa na figo ikiwa ni sehemu ya uratibu wa shinikizo la damu na hali ya mwili.

Figo pia huzalisha homoni ya ‘erythropoietin’ ambayo huchochea uti wa mgongo kuzalisha chembechembe nyekundu za damu. Kuna seli maalumu katika figo ambazo huratibu kiwango cha hewa ya oxygen ndani ya damu. Kama kiwango hicho kitashuka ‘erythropoietin’ huongezeka na kuchochea uzalishaji wa chembe nyekundu za damu. Baada ya figo kuchuja uchafu, mkojo huzalishwa na kupelekwa kwenye kibofu kupitia mrija wa ureta. Hutunzwa hapo ukisubiri mtu, mnyama akojoe

Comments are closed.