The House of Favourite Newspapers

Fahamu Sababu za Maumivu ya Matiti

MAUMIVU ya matiti hutokea mara kwa mara kwa wanawake, hasa kwenye matiti yenyewe au karibu na kwapa. Hujulikana kwa kitaalamu kama mastalgia.

Matiti huweza kuuma yenyewe au kupata maumivu pale unapoyashika. Hali hii huwapa baadhi ya wanawake hofu wakidhani kuwa ni dalili ya saratani au mimba.

 

Maumivu ya matiti peke yake kwa sehemu ndogo yanahusishwa na kansa. Kuna aina mbili za maumivu ya matiti; Maumivu yanayotokana na hedhi ya kila mwezi ambayo mwanamke anapata ikiwa ni sehemu ya maumbile ya kibaiolojia na yanaweza kutokea kwenye matiti yote mawili.

 

Aina ya pili ni maumivu ambayo hayatokani na hedhi au mzunguko wa damu ambapo husababishwa na maambukizi au kunyonyesha. Hutokea zaidi kwenye misuli ya kifua ambapo huathiri titi moja au yote mawili na wakati mwingine sehemu ndogo tu ya titi. Matiti yanaweza kuwa na vivimbe visivyo saratani (cysts) ambavyo hujaa maji na kusababisha maumivu ya kujirudiarudia. Zifuatazo ni sababu za kupata maumivu kwenye matiti:

 

KUPATA HEDHI

Premenstrual syndrome. Hali hii ni ya mabadiliko ya vichochezi vya uzazi ambavyo hujitokeza kabla ya hedhi kuanza. Husababisha matiti kujaa na kuuma. Mumivu huwa makali zaidi siku 3 – 5 kabla ya hedhi na kupungua baada ya hedhi kuanza.

 

Robo tatu ya maumivu ya matiti ni matokeo ya kuzalishwa kwa homoni za ‘Estrogen’ na ‘Progesterone’ ambazo hutokea wakati wa hedhi ya kila mwezi.

 

Maumivu ya matiti yanayotokana na homoni yanampata kila mwanamke. Haijalishi wana miaka mingapi 14 au 44, kama bado wanapata hedhi wako katika hatari ya kupata maumivu ya matiti.

 

Kwa baadhi ya wanawake, maumivu hayo huondoka yenyewe ndani ya wiki moja hadi siku 10. Wengine hutumia dawa za kutuliza maumivu. Kubadili mlo inaweza kusaidia kutuliza maumivu yanayotokana na hedhi kwa sehemu ikiwa ni pamoja na ulaji wa mbegu za katani na kujiepusha na vyakula vyenye mafuta mengi.

 

UJAUZITO

Katika kipindi cha kwanza cha ujauzito, mwili huongeza uzalishaji wa homoni ambazo husababisha mabadiliko ya kimwili ikiwemo kutapika, kizunguzungu, kuchagua vyakula, kichefuchefu na maumivu ya matiti.

 

Tishu za matiti huongezeka, maziwa kujaa na chuchu kuimarika. Maumivu hayo ni kwa sababu ya mabadiliko ya homoni ambapo inajumuisha mfumo mpya wa uzalishaji homoni kwa ajili ya kulinda mimba.

 

KUFANYIWA UPASUAJI

Mshtuko wowote kwenye matiti unaweza kusababisha maumivu ikiwemo upasuaji, majeraha, kuondolewa kwa sehemu ya nyama ya mwili.

VIDONGE VYA UZAZI WA MPANGO

 

Aina yoyote ya dawa ambayo ina homoni za kuzuia mimba zinaweza kusababisha maumivu ya matiti. Muone daktari kama maumivu unayoyapata yamesababishwa na matumizi ya njia za mpango.

Kwa sehemu kubwa maumivu ya matiti hupotea yenyewe na yanaweza kutibika kwa urahisi. Ushauri ni kuwa, ikiwa maumivu yataendelea kwa wiki moja hadi mbili muone daktari na kama kuna dalili nyingine ikiwemo kutoka usaha, matiti kuvimba na kuwa mekundu.

 

Wengine huumwa matiti kutokana na kupatwa na maambukizi ya matiti, usaha kwenye matiti, kutanuka kwa mirija ya maziwana matumizi  ya dawa kama digitalis, aldactone methyldopa au kutokana na kukoma kwa hedhi. Jambo la kufahamu ni kwamba, ni aghalabu sana kwa saratani ya matiti kusababisha maumivu ya matiti.

 

MATIBABU

Mara nyingi maumivu ya matiti huisha yenyewe baada ya muda fulani. Kusaidia kupunguza maumivu ya matiti unashauriwa kuvaa sidiria isiyokubana, punguza unywaji wa chai na kahawa na tumia vitamini E. Kama unapata maumivu makali sana unaweza ukatumia dawa za maumivu kama paracetamol, NSAIDs. Maumivu yakizidi, muone daktari.

Comments are closed.