The House of Favourite Newspapers

Fahamu tatizo la vidonda vya tumbo kwa mjamzito

MJAMZITO anaweza kupata vidonda vya tumbo baada ya ujauzito na ukaleta matatizo kwa mtoto mchanga aliye tumboni.  Umakini unahitajika sana katika kumchunguza mama mjamzito ili kuelewa nini kitakuwa ndiyo chanzo cha vidonda vya tumbo kwake. Mwanamke unayeumwa vidonda vya tumbo hata kabla ya kushika ujauzito unaweza kuendelea kutumia baadhi ya dawa rafiki za kutibu au kuzuia dalili za vidonda vya tumbo hata baada ya kuwa umepata ujauzito.

Kwa kawaida, kila dawa huwa na matokeo ya aina mbili; yaani matokeo chanya (uponyaji) na matokeo hasi (uharibifu). Matokeo hasi yanapozidi huweza kusababisha kifo kwa mjamzito au mtoto aliye tumboni. Moja ya matokeo hasi ya matumizi mabaya ya dawa za kutibu vidonda vya tumbo kwa kina mama wajawazito ni pamoja na mtoto kuzaliwa kilema, mtoto kufia tumboni na hata kifo kwa mama.

Wakati wa ujauzito, mama mjamzito anaweza kutokewa na kiungulia mara kwa mara na hata kiasi cha asidi kuongezeka mwilini. Ni wakati huu mwanamke anaweza kuanza kutafuta matibabu kwa ajili ya vidonda vya tumbo na ndipo umakini mkubwa unapohitajika ili asimdhuru mtoto. Hivyo, dawa rafiki, yaani dawa ambazo hazina madhara hasi, ndizo zitumike kwa ajili ya mama mjamzito hasa katika kipindi cha majuma 10 ya kwanza ya ujauzito.

Licha ya kwamba dalili za vidonda vya tumbo hutoweka wakati wa ujauzito kwa wanawake wengi, baadhi ya wanawake hulalamika kuwa na maumivu makali. Hii kwa kawaida hutokea kwa wanawake ambao maumivu ya vidonda vya tumbo yalikuwa makali walipokuwa hawana ujauzito.

Kama nilivyosema hapo juu, kina mama wengi wanaweza kujihisi wamepona kabisa vidonda vya tumbo wakati wanapata ujauzito au wakati wote wa kipindi cha ujauzito, ingawa baadhi yao hutokewa na maumivu makali hata wakati wa ujauzito, na hii inatokea kwa wale ambao hata kabla ya kupata ujauzito walikuwa wakipatwa na maumivu hayo makali.

Hivyo bado nashauri wakati huu wa ujauzito mama apewe dawa rafiki tu hasa zile zitokanazo na vyakula na mimea hadi hapo atakapojifungua. Wakati huohuo mjamzito anatakiwa kuwa makini kutokutumia vyakula au vinywaji vyenye asidi nyingi. Kwa kawaida vidonda vya tumbo huzalisha dalili chache pindi tumbo linapokuwa halina kitu, inashauriwa mjamzito asikae muda mrefu bila kula chakula na ale mlo mdogomdogo ili chakula kiendelee kukaa tumboni.

Mjamzito pia aepuke kula kupita kiasi kwa sababu kula kupita kiasi huchochea uzalishwaji wa asidi nyingi tumboni. Kadharika, chakula kinapokuwa kingi tumboni hulifanya tumbo kujitandaza sana, na hatimaye kuchokoza vidonda vya tumbo.

Mjamzito aepuke kunywa maziwa. Watu wengi hudhani kwa kuwa maziwa hutumika kumpatia mtu mwenye tatizo la sumu mwilini, basi yanaweza pia kudhibiti kiasi cha asidi tumboni hasa yakitumika kwa mtu mwenye vidonda vya tumbo, hili si kweli.

Tafiti za kitaalamu za hivi karibuni zinathibitisha kwamba maziwa yasitumike kwa mtu mwenye tatizo la vidonda vya tumbo kwa sababu hayatibu vidonda vya tumbo.

TIBA & USHAURI

Muhimu kuliko yote ni kutambua kuwa vidonda vya tumbo vinatibika kabisa, unachohitaji ni kuufahamu hasa ugonjwa wenyewe huletwa na nini hasa mwilini na namna ya kuishi kwa maana ya kula na kunywa na hatimaye uponyaji ufanyike.

Dawa peke yake bila kujuwa nini ule na kunywa hazitasaidia uponyaji wa vidonda vya tumbo, nenda kwa wataalamu watakupima na kukupa dawa.

Kama wewe ni mjamzito na una vidonda vya tumbo, ni vema kuwasiliana na wataalamu wa afya ili wakuelekeze utumie dawa gani na nini cha kufanya ili afya yako na ya mwanao iwe imara. Usinywe dawa bila kupata ushauri wa kitaalamu kwa sababu kuna dawa hazipaswi kutumiwa na wajawazito. Kwa ushauri zaidi wasiliana nami kwa namba hiyo ya simu.

Comments are closed.