FAHAMU UGONJWA WA HOMA YA MAPAFU

HOMA ya mapafu ni mashambuliwa ya ugonjwa wa homa ya mapafu (pneumonia) unaoenezwa kwa njia ya hewa.  Pneumonia hutokana na kuvimba kwa mkusanyiko wa seli katika moja au mapafu yote mawili. Mara nyingi husababishwa na bakteria.  Mwishoni mwa mirija ya kupumulia mwa mapafu yote, kuna mifuko midogo. Unapokuwa na homa ya mapafu, mifuko hiyo huvimba na kujaa maji na hivyo kusababisha ugumu katika kupumua, homa, kukohoa, kutoka jasho kutetemeka au kupoteza jamu ya kula.

Watu wa umri wowote huugua pneumonia, lakini ugonjwa huo huwakumba sana watoto na wazee. Homa ya mapafu husababisha vifo vingi duniani. Kujikinga na ugonjwa huo watoto hupata chanjo mara tatu; wakiwa na wiki nane tangu kuzaliwa, wiki 16 na ya mwisho wanapotimiza umri wa mwaka mmoja. Wazee na wenye magonjwa sugu hupewa mara moja na kuzuia kwa kiasi kikubwa uwezekano wa kupata tena maambukizi hayo. Nimonia inatokana na hitilafu zinazotokea katika sehemu moja au mbili za mapafu. Inaweza kuwa ni uvimbe ambao husababishwa na bakteria au virusi vinavyoenezwa kwa njia ya hewa na kuifanya mishipa ya kupitisha hewa kushindwa kufanya kazi kutokana na kujaa maji.

Nimonia ni ugonjwa unaosababishwa na aina fulani ya seli nyeupe za damu ziitwazo eosinofil ambazo hukusanyika kwenye mapafu. Dalili za awali za nimonia huanza kuonekana ndani ya saa 24 mpaka 48. Moja ya dalili hizo ni kukohoa. Mgonjwa anaweza kutoa makohozi mazito ya rangi ya njano au kikohozi kikavu.

Dalili huonekana kwa watoto, watu wazima au wazee na zinajumuisha homa inayoambatana na kutetemeka mwili na maumivu ya kifua hasa upande wa pafu lililoumia. Nyingine ni kikohozi kikavu, kutokwa jasho hasa usiku, kichefuchefu, kutapika na maumivu ya misuli. Mgonjwa pia anaweza kuhisi mapigo ya moyo na pumzi kwenda kasi, kukata pumzi kukichukua muda mrefu kidogo na uzito unapungua.

Dalili za hatari zinazohitaji huduma za haraka za daktari ni pamoja na homa kali, kushindwa kupumua na rangi ya ngozi kuwa ya bluu. Nyingine ni kikohozi cha makohozi kutoka ndani, kupoteza kumbukumbu hasa kwa wazee, kupungua uzito ndani ya muda mfupi na mapigo ya moyo kwenda kasi. Mgonjwa anaweza kubanwa na kifua, kuhisi maumivu ya kichwa na kupoteza hamu ya kula. Watu wanaoshambuliwa zaidi ni wale ambao kinga zao za mwili ni dhaifu.

Mgonjwa anahitaji matibabu kwani akiachwa kwa muda mrefu anaweza kusababishiwa kifo. Vijana wanaweza kupona bila kupatiwa matibabu endapo watakunywa maji mengi. Kinga Nimonia unasababishwa na bakteria au virusi na namna ya kwanza ya kuuepuka ni kuzingatia usafi. Mgonjwa anashauriwa kutumia kitambaa kisafi kila anapokohoa au kupiga chafya na kujifuta.

Anashauriwa kukitupa kitambaa kilichotumika kwani wadudu wanaweza kukaa humo kwa muda. Vilevile mgonjwa anashauriwa kunawa mikono ili asiwaambukize wengine vimelea vya ugonjwa. Kulinda afya kwa kuepuka matumizi ya sigara kunakoathiri mapafu na kutoa mwanya wa maambukizi kunasaidia kutoshambuliwa na ugonjwa huo. Njia ya uhakika ya kukabiliana na nimonia ni chanjo ambayo hutolewa kwa watoto na wazee.

Watoto wenye umri chini ya miaka mitano hupewa Pneumococcal Conjugate Vaccine (PCV13) wakati wazee wenye zaidi ya miaka 65 hupewa Pneumococcal Polysaccharide Vaccine (PPSV23). Ugonjwa huu unatibika endapo muathirika atawahi hospitali na atazingatia ushauri wa daktari. Kupumzika muda wa kutosha na kunywa maji mengi au juisi ya matunda inasaidia kupunguza madhara ya ugonjwa huu.

Mgonjwa asiye na maambuki mengine, anaweza akapona kwa kuzingatia masuala yaliyobainishwa hapo juu na kujiepusha na mazingira hatarishi. Watu wenye upungufu wa kinga wanashauriwa kukaa mbali na mgonjwa wa nimonia mpaka atakapopona kabisa ili kuepuka maambukizi mapya. Mikusanyiko ya watu, ni miongoni mwa mazingira rahisi kwa mtu kupata maambukizi hayo.


Loading...

Toa comment