The House of Favourite Newspapers

Faida ya zawadi mwenza kwa wapendanao!

0

WIKI ILIYOPITA tuliuliza swali, kama umeingia kwenye ndoa na mkeo akapata ujauzito. Mlipoenda kupima afya, mnabainika wote mmeathirika, ingekuwa ndio wewe ungefanya nini? Tuyaangalie baadhi ya majibu ya wasomaji:  Ukishagundua shida kama hiyo, haina jinsi tena, inabidi mzidi kupendana maana upendo utawarejeshea furaha katika ndoa yenu.

Basilius Robert.

Ni kushirikiana na mwenzangu kwa kufuata masharti ya afya tutakayopata Angaza. Hakuna kulaumiana maana hajulikani mwanzilishi.

Msomaji.

Hapo kwangu mimi itanibidi nikubaliane na hali halisi iliyopo sababu huwezi jua kuwa kisababishi ni mimi au mke wangu, hivyo tutafuata ushauri wa wataalam wa afya ili tuweze kuishi vizuri.

Mocy Mtolela, BARIADI.

Duuh huo mtihani kwa sababu mkiwa kwenye ndoa ni vigumu kugundua nani aliyesaliti. Kwa ushauri wangu, siwezi kumuacha, nikimuacha ni chanzo cha yeye kuumia na kuwaambukiza wengine. Nitapambana hivyo hivyo tutaishi kwa matumaini, maisha yataendelea.

Rajabu Mbemba, DAR.

Kwa kuwa wote tumekutwa na janga hilo, itabidi tufarijiane na kupata ushauri nasaha jinsi ya kumkinga mtoto wetu na maambukizi.

Muganda Paul, TARIME.

Ukimwi sio tatizo maana ni mipango ya Mungu, nitamshauri mwenza wangu tuishi kwa matumaini.

Muddy Madiley, TABATA.

Ingekuwa mimi baada ya kugundua mimi na mke wangu wote tumeathirika, nitakubaliana na hali hiyo, hakuna namna.

Dickson Lebana, Mnadani DODOMA.

SWALI LA WIKI HII:

Umepewa taarifa kuwa mumeo ana mwanamke mwingine baa, unafika na kuwakuta kweli wamekaa katika mkao wa kimahaba.

JUMAMOSI nyingine Mungu ametujaalia uhai. Ametupa nafasi ya kukutana mimi na wewe katika safu hii mahsusi kwa ajili ya masuala ya mahusiano. Tunazungumza mahusiano, tunaboresha mahusiano yetu ili angalau mahusiano yawe eneo salama.

Ukisikiliza maoni ya wengi sasa hivi kwenye masuala ya mahusiano, watakuambia sio sehemu salama. Kwamba watu wamekuwa waongo, watu wamekuwa hawana mapenzi ya kweli, usaliti umekua kwa kaisi kikubwa.

Inakatisha tamaa, watu hawaoni tena thamani ya urafiki, uchumba au hata ndoa. Walioko kwenye ndoa wanalia usaliti, wanalia matatizo mengi na hata kufikia hatua ya kutaka hata kutoka kwenye ndoa. Ndugu zangu hii ni hatari, wakati mwingine ni vyema kutenga muda na kutafakari maisha yetu.

Kwenye mahusiano kuna vitimbi vingi lakini ni wewe unachotakiwa ni kutuliza akili yako na kujua nini unatakiwa kufanya na nini hutakiwi kufanya. Mfano, kuna yale mambo ya kufuatiliana sana hayana maana. Mpe mtu uhuru lakini mueleze kabisa, amebeba dhamana yako.

Hapaswi kufanya ujinga, ajiheshimu kama mpenzi, mchumba, mume au mke wa mtu. Ajue ana dhamana ya kulinda afya yenu. Asijirahisi kijingajinga sababu ya tamaa ya mali na mambo mengine. Mueleze madhara ya usaliti, ni ugomvi, magonjwa na hata kuuana. Akiwa muelewa, atachagua kuishi kwenye misingi mizuri, akiwa si muelewa atafanya kinyume chake.

Ukishafanya hayo yote, wewe muachie Mungu. Usimbane, mpe uhuru na endapo atafanya ujinga wala usipate tabu, utaujua tu siku moja. Hapo ndipo utakapomwaibisha kwa kumwonesha makosa yake na utaangalia amepokeaje, amejutia? Ameomba msamaha na kuomba nafasi ya kujisahihisha? Akiomba hiyo nafasi, mpe.

Akirudia tena na tena kufanya mambo ambayo yanahatarisha afya na uhai wenu, omba ushauri wa ndugu, viongozi wa dini na kadharika. Ikishindikana hapo achana naye. Atakupasua kichwa bila sababu. Anaweza kukusababishia matatizo yasiyokuwa ya lazima. Ni bora ukaachana naye kwa amani. Kila mtu akaishi kwa amani, maisha mazuri yapo hata bila ya mahusiano.

Lakini pamoja na yote hayo, ni vizuri tukajua pia kuna kitu kinaitwa tabia ambacho kinaweza kujenga au kubomoa mahusiano. Ili muweze kuishi kwa amani, inawapasa kuishi kwa kusaidiana kitabia. Kila mmoja ajifunze kutoka kwa mwenzake.

Kujua nini anapenda na nini hapendi. Umfurahishe mwenzako kwa vitu ambavyo anavipenda. Sio kila siku kumlisha mwenzako vitu ambavyo havipendi. Hivyo ndivyo vitu ambavyo vinachangia kwa kiasi kikubwa matatizo katika mahusiano.

Kwenye kumfurahisha mwenza wako kuna suala la zawadi. Unaweza kuliona ni dogo lakini linaleta ustawi sana katika uhusiano. Niamini mimi, wewe jenga utamaduni wa kumnunulia mwenza wako vizawadi hata kama ni vidogovidogo halafu utaona matokeo yake.

Lazima mwenza wako atakuwa na furaha. Upendo wake utaongezeka kwako, ataongeza thamani kwako. Kitendo cha wewe kutenga muda na kumnunulia zawadi, kinaashiria kwamba umemjali. Umemfikiria wakati ambao haupo naye, hilo jambo linaongeza nguvu sana katika upendo.

Zawadi inajenga pia uaminifu. Mtu anapoona unampa zawadi, atakaa naye kukuamini kwamba unamjali, unamthamini, hivyo naye anajikuta tu anarejesha uaminifu. Anakujali kama ambavyo wewe umemjali. Zawadi pia ni ishara ya upendo, unapompa mwenza wako anakuwa na furaha lakini anauona upendo kutoka kwako, anajikuta naye anarejesha upendo kwako.

Kwa leo naishia hapo, unaweza kunifuata kwenye mitandao yangu ya kijamii, Instagram na Facebook: Erick Evarist, Twitter: ENangale.

 

Leave A Reply