The House of Favourite Newspapers

Faida za Kupata Mafanikio Yenye Baraka za Mungu!

NA Amran Kaima | RISASI MCHANGANYIKO | MAISHA NA MAFANIKIO

Awali ya yote nichukue fursa hii kumshukuru Mungu kwa yote ambayo amekuwa akinitendea katika kila siku ya maisha yangu. Niahidi tu kwamba nitaendelea kumuabudu ili nizidi kupata baraka zake katika kila nilifanyalo hapa ulimwenguni.

Mpenzi msomaji wangu, katika kutafuta mafanikio siku zote tumekuwa tukipanga tu mambo ambayo tunaamini tukiyafanikisha, tutapiga hatua. Lakini ukweli ni kwamba, kufanikiwa ama kutokufanikiwa kwetu kuko mikononi mwa Mwenyezi Mungu. Yeye akisema yes, ni yes! Akisema no, ni no!

Lakini wakati ukweli ukiwa hivyo, bado sisi binadamu tunajisahau sana na kudhani kupambana kwetu tu ndiko kunaweza kutuingiza kwenye mafanikio. Tunatumia muda mwingi sana kutafuta pesa lakini tunasahau kwamba kuna Mungu ambaye bila kumshirikisha kwenye mipango yetu, kufanikiwa ni ngumu sana.


Nimefikia hatua ya kuandika makala haya baada ya kubaini kwamba, tulio wengi tunatamani sana kuwa kati ya watu waliofanikiwa kimaisha lakini tunashindwa kuamini kwamba, kuna nguvu f’lani ambayo inatakiwa kushirikishwa ili mafanikio ya kweli yaweze kupatikana.

Kama ulikuwa hujui basi nikufahamishe tu kwamba, bila Mungu kutia tiki katika shughuli unazofanya, hata uzifanye usiku na mchana huwezi kufanikiwa. Ndiyo maana unaweza kumkuta mtu kwa muda mrefu sana amekuwa akipambana lakini haoni mabadiliko yoyote kwenye maisha yake. Kwa nini? Yawezekana kuna sababu nyingine lakini pia huenda amekuwa akifanya mambo yake bila kumshirikisha Mungu.

Ndiyo maana nasema, Mungu ana nafasi kubwa sana katika mafanikio yako. Yeye anazo funguo za kukufungulia milango ya baraka na ukashangaa kila unalolifanya linafanikiwa lakini ukijifanya mjuaji, Mungu atakuacha uhangaike.

Hivyo basi, kuanzia sasa mtangulize Mungu wako katika kila unachokifanya na utashangaa miujiza atakayokuwa anakufanyia. Ila sasa, katika hili la kumkumbuka Mungu katika harakati zetu za kutafuta mafanikio, nikumbushe jambo moja kwamba, tusimgeukie Mungu pale tunapokuwa na shida zetu.

Kila mmoja kwa imani yake ajue, kwa maisha ya sasa tunatakiwa kufanya sana ibada. Tunakabiliwa na changamoto nyingi sana za kimaisha, tunapata mitihani mingi inayotufanya tuyaone maisha magumu lakini bado hatuoni sababu ya kujiweka mbele za Mungu.

Hivi unadhani mafanikio yatakujia bila ya wewe kutumia sehemu ya muda wako kumuomba Mungu? Unadhani mafanikio yanaweza kuja kwa ujanjaujanja wako tu?

Hayo ni mambo yasiyowezekana na hata ukifuatilia utagundua waliopata mafanikio yasiyokuwa na baraka za Mungu, wengi wamefilisika na kuanguka kiajabu. Wanabaki kusema wamerongwa lakini wamesahau kwamba walipata mafanikio katika mazingira yasiyomfurahisha Mungu.

Ndiyo maana nasema, tufanye yote lakini tukumbuke kufanya ibada na kumshirikisha Mungu katika mipango yetu. Tusiufanye ubize huu wa kutafuta pesa utuweke mbali na Mungu na tukaja kuanza kukimbilia makanisani na misikitini pale ambapo yametufika makubwa.

SIKILIZA ALICHOKISEMA NAPE BAADA YA KUKABIDHIWA RIPOTI SAKATA LA MAKONDA VS CLOUDS

Comments are closed.