Faili la Fiston, Metacha Mikononi Mwa Migne

UONGOZI wa Yanga, umepanga kumkabidhi Kocha Mkuu mpya wa timu hiyo, Mfaransa Sebastien Migne faili la wachezaji wote wanaotarajiwa kumaliza mikataba yao haraka mara baada ya kutua nchini.

 

Kocha huyo muda na siku yoyote kuanzia sasa atatua hapa nchini tayari kwa ajili ya kujiunga na timu hiyo inayoongoza katika msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 50, ikifuatiwa na Simba yenye 46.

 

Baadhi ya wachezaji wanaomaliza mikataba yao ndani ya Yanga ni kipa Metacha Mnata, Said Makapu, Abdoulrazack Fiston na Farouk Shikalo.

 

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Spoti Xtra, kocha huyo mara baada ya kutua nchini, atasaini mkataba na haraka atapewa kupitia mikataba ya wachezaji kabla kutoa mapendekezo ya usajili mpya kuelekea msimu ujao.

Mtoa taarifa huyo alisema kuwa kocha atapewa nafasi ya kuamua wachezaji wa kuwaacha wenye mikataba na wasiokuwa nayo baada ya kuwaangalia kabla ya ligi haijamalizaka.

 

Aliongeza kuwa, kocha huyo hatakuwa na muda wa mapumziko mara baada ya ligi kumalizika, kwani ataendelea kukaa na kikosi hicho kwa ajili ya kuendelea na ‘pre season’.

 

“Uongozi unafanya mawasiliano na kocha ambaye siku yoyote atatua nchini kujiunga na timu, lakini katika kipindi hicho baada ya kutua majukumu yote atakuwa anayafanya Mwambusi (Juma).

 

“Yeye atakuwa katika sehemu ya ushauri kama akiwa anakaa katika benchi, kwani bado hajawajua wachezaji na ligi kwa jumla, hivyo ngumu kwake kusimamia timu katikati ya ligi na badala yake atakuwa Mwambusi.

 

“Migne atakuwa ana kazi ya kukiangalia kikosi na kikubwa kuangalia wachezaji atakaowahitaji kuwabakisha kwa ajili ya kuwatumia msimu ujao, katika kipindi hicho kocha atakabidhiwa mikataba ya wachezaji kwa ajili ya kuipitia,” alisema mtoa taarifa huyo.

 

Alipoulizwa Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela kuzungumzia hilo, alisema: “Ni mapema kuzungumzia hilo la usajili katika kipindi hiki, kwani akili za uongozi zote tumezielekeza kwenye ubingwa wa ligi na Kombe la FA.“Hilo la usajili litakuja baadaye, isitoshe muda wa usajili bado, ni bora tukasubiria muda ukifikia tutakuwa katika sehemu nzuri ya kulizungumzia hilo.”

STORI: WILBERT MOLANDI, DAR ES SALAAMTecno


Toa comment