The House of Favourite Newspapers

Familia ilivyochinjwa

0

Na Victor Bariety, GEITA
VILIO simanzi na majonzi bado vimetawala katika Kijiji cha Iteja mkoani Geita kufuatia watu watatu wa familia moja kufa kwa kuchinjwa kama kuku kwa imani za kishirikina.

Tukio hilo lilijiri saa nane usiku wa Desemba Mosi, mwaka huu ambapo watu hao walikatwakatwa mapanga na mtu mmoja aliyenusurika alijeruhiwa vibaya na watu hao ambao hawakufahamika mara moja.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, SACP Latson Mponjoli mbali na kuthibitisha kutokea kwa tukio hilo, aliwataja waliouawa kuwa ni Sophia Sylvester (40), Mariam Lusafisha (48) na Shinje Honela (1).

Akisimulia tukio hilo, Kamanda Mponjoli alisema hivi karibuni mkazi wa kijiji hicho, Samuel Masebu (50) ambaye ni mume wa marehemu Mariam alifariki dunia kwa kuugua kwa muda mrefu maradhi ya kawaida.

Alisema Masebo alikuwa na wake watatu na siku chache baada ya kufariki kwake alianza kuonekana kwa njia za kishirikina nyumbani kwa mke wa pili ambaye kwa sasa ni marehemu.

“Wanasema eti marehemu alikuwa anaonekana usiku nyumbani kwa mke wa pili na kwamba hakufariki dunia, bali aliuawa kishirikina masuala ambayo sisi kama polisi hatuwezi kuyathibitisha,’’ alisema Kamanda Mponjoli.

Alisema siku ya tukio wakati familia hiyo ikiwa inaota moto usiku, lilitokea kundi la watu wasiojulikana wakiwa na mapanga na kuanza kuwashambulia kila mtu aliyekuwa mbele yao na kusababisha vifo hivyo.

“Ni tukio la kusikitisha sana, wameuawa kinyama, wametenganishwa vichwa na kiwiliwili lakini polisi tumeanza kuchukua hatua,’’ alisema Mponjoli.

Uwazi lilifika katika kijiji hicho na kukuta umati ukiwa umekusanyika nyumbani kwa familia ya Masebu aliyefariki dunia Novemba 12, mwaka huu ambapo kifo chake ndicho kinahusishwa na ushirikina.

“Jamani huu ni unyama wa hali ya juu. Hapa nyumbani palikuwa kama bwawa la damu. Tumekuta kiwiliwili kule, kichwa huku. Marehemu walipiga kelele kuomba msaada lakini watu walipofika, walikuta wameshakata roho na wahusika wameshakimbia,” alisema mkazi mmoja wa kijiji hicho aliyeomba hifadhi ya jina lake.

“Sisi tunaiomba serikali kupitia jeshi la polisi kuweka mikakati ya kukomesha mauaji ya namna hii. Hapa Geita baadhi ya watu wanaona ni kawaida kuchukua hatua ya kuchinja wenzao, serikali ikae macho na hili,” aliongeza mkazi huyo.

Baadhi ya wanawake, walionekana wenye simanzi bado huku wengi wao wakiwa wamejiinamia na wengine kuzungumza kwa sauti ya chini wakilaani tukio hilo.

Leave A Reply