Familia: Kadi ya benki ya Mtikila imeibwa

mtikila_mchungaji

Mwenyekiti wa Chama cha Democratic (DP), Mchungaji Christopher Mtikila.

Na Haruni Sanchawa
KUFA kufaana? Tukio la ajali lililosababisha kifo cha aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Democratic (DP), Mchungaji Christopher Mtikila (pichani) limeendelea kuibua mazito baada ya familia ya marehemu huyo kubaini kuwa, kadi ya benki ya Mtikila haikuwepo kwenye mkoba wake.

Baadhi ya vitu ambavyo familia hiyo ilichukulia kipaumbele kufuatilia ilikuwa ni simu na kadi ya benki ambayo ilikuwa ni muhimu kuliko vyote ndani ya mkoba wake aliosafiria siku chache kabla ya ajali.

Akizungumza na Uwazi juzi, Naibu Katibu Mkuu wa DP, Abdul Juma alisema yeye kama kiongozi wa chama na familia ya marehemu Mtikila walifuatilia vitu vilivyokuwemo kwenye mkoba wa kiongozi huyo ambapo wanaamini ndani yake mlikuwa na kadi ya benki.

“Ndugu Mwandishi kazi hiyo ya kufuatilia ilifanyika siku ya Jumatatu (Oktoba 12) lakini ndani ya mkoba wake kadi ya benki haikuwemo kitu ambacho kilitushtua hadi hivi sasa,” alisema Juma.

Kiongozi huyo alisema kuwa, baada ya ajali hiyo, ule mkoba wake ulipelekwa nyumbani kwa Mtikila na aliyeupeleka ni Mchungaji Mgaya ambaye kwenye ajali hiyo alinusurika.

Uwazi lilibaini kuwa, kadi hiyo ilikuwa ni ya Benki ya NMB Tawi la Bank House yenye namba 15110006438 ambapo familia hiyo inaamini kuwa kulikuwa na kiasi kikubwa cha pesa ingawa iligoma kutaja idadi.

Juma aliongeza kuwa, katika mazingira ya kawaida kuna mtu anatuhumiwa lakini si vyema kumtaja kwa jina kwa sababu za kiuchunguzi.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, ACP Jafari Mohamed alipoulizwa kuhusiana na kadi hiyo alisema hajapata malalamiko kutoka kwa familia ya marehemu na kama kuna tatizo lolote ameitaka familia hiyo kufika ofisini kwake kwa maelezo zaidi.

Mchungaji Mtikila alifariki dunia Oktoba 4, mwaka huu kwa ajali ya gari iliyotokea katika Kijiji cha Msolwa, Bagamoyo, Pwani na kuzikwa kijijini kwake, Maro, Ludewa mkoani Njombe.

Loading...

Toa comment