Familia ya Kichawi -26

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:

Kama mchawi alitakiwa kumtoa mmoja wa watu wake wa karibu kwa ajili ya kuliwa nyama halafu akawa hana, akasema anakopa, yaani ale nyama za wenzake yeye atakuja kulipa, lazima atalipa. Awe amekufa, awe hajafa.

SASA ENDELEA MWENYEWE…

Ndiyo maana, umewahi kusikia mchawi amekufa mahali baada ya siku chache, mtoto wake naye anafuatia. Maana ni nini?

Maana ni kwamba, mchawi huyo alikufa akiwa ameacha deni na hakuna wa kulilipa. Maana wapo wachawi ambao wamemaliza ndugu wote kwa kuwatoa nyama halafu wanabaki wao na ndugu mmoja tu.

Basi, kufumba na kufumbua tulisikia kishindo kikuu ndani ya nyumba bati zikitetemeka. Niliogopa awali, lakini baba akasema ni wachawi wenzetu wamekuja kwa ajili ya shida au ufumbuzi.

“Tunataka. Tunataka ahadi itimizwe kwa kinywa chako mzee,” alisema mchawi mmoja huku wote wakiwa wameshajionesha.

Baba aliinamisha kichwa chini kisha akatuangalia sisi, akasema:

“Mama yenu alikuwa anadaiwa mtu mmoja na alikuwa hajalipa. Sasa hawa wanataka deni lao lilipwe hata kwa kauli yangu ili wajue kuwa watalipwa.”

“Kivipi?” nilimuuliza baba kwani sikuwa najua kulipwa mtu kivipi.

“Wanataka nitoe mtu mmoja awe nyama kufidia deni alilokuwa akidaiwa mama yenu.”

“Baba unataka kumtoa nani? Sitakubali kuona ndugu yangu hata mmoja anakufa kisa deni la mama. Alikopa mkiwa wote kwenye chama chenu, kama ni malipo jitoe wewe,” alisema kaka yangu wa kwanza.

“Sina maana ya kuwaua nyie.”

“Sasa nani?” niliuliza mimi.

Baba hakutoa majibu, lakini pia akawaambia wale wachawi kwamba wampe siku saba atatoa jibu. Wachawi walikubali, wakaondoka zao kwa staili ya kupotea.

Kifo cha mama kikajulikana na sisi tu, tulilia ndani kwa ndani. Majonzi yalitawala nyumba kwa maana ya kuondokewa na mama mzazi.

Kulipokucha, asubuhi kama saa kumi na mbili na nusu hivi, mlango mkubwa uligongwa, tukashtuka maana mgongaji wala hakusema yeye ni nani.

“Nani?” mimi nilimuuliza.

“Binti Ngomeleki.”

Wote tulikimbilia chumbani kwa baba, ni pamoja na baba mwenyewe. Kule chumbani wote tukataka kuingia chini ya kitanda ili kujificha.

“Jamani hodini,” binti Ngomeleki alibisha kwa kugonga.

Baba akasema anatoka ili ijulikane moja. Alisema kitendo cha kukaa chumbani kinaweza kutupa wakati mgumu wote kwani hatutajua ataondoka muda gani pale mlangoni.

Baba alitoka, mimi na kaka tukamfuata nyuma. Chumbani walibaki, dada na wadogo zetu wawili. Mimi niliwaambia wasitoke.

“Ni kwa nini mnafanya hivi?” binti Ngomeleki alimuuliza baba akiwa mlangoni. Hapo ni baada ya baba kufungua mlango na kusimama katikati akimzuia mwanamke huyo asiingie.

“Binti Ngomeleki naomba hili jambo liache kwenye familia yangu. Mimi ni mwanaume na ni baba pia. Umeniulia mke wangu, umewaulia hawa watoto wangu mama yao.”

“Nimemuua au nyie wenyewe mmesababisha afe. Hivi wewe baba Amani nini kimekusukuma kuwaingiza hata watoto wako kwenye chama cha uchawi? Siku zote hukuwahi kujua ni chama cha hatari?”

Baba aliposikia maneno hayo aliangua kilio huku akifunga mlango kwa nguvu. Akakaa kwenye kiti sebuleni. Na sisi watoto pia tulilia na baba. Watu wakaanza kuja wakimuuliza baba kama kweli mama amefariki dunia. Walisema wameambiwa na binti Ngomeleki.

Ilibidi baba akubali, na ndipo kilio kilipozidi mara kumi zaidi ya mwanzo. Ilikuwa kilio cha kufiwa. Majirani wengine walipofika waliguna na kuondoka, wengine waliungana na sisi katika kulia. Haiwezekani watu wote wakawa maadui zako.

Mipango ya mazishi ya mama ilifanywa. Lakini habari mitaani zilienea kwamba, mama alifariki akiwa katika harakati za kuwanga kwenye nyumba ya binti Ngomeleki. Na binti Ngomeleki mwenyewe ndiye aliyekuwa akisambaza habari hizi.

Baada ya mazishi, baba alitukalisha chini, akasema:

“Nimefikiria sana wanangu. Nimeamua kusema kwamba, mimi na uchawi basi! Na nataka na nyie wanangu pia kuachana na uchawi. Haiwezekani niishi na familia ya kichawi, baba, mama na watoto. Ni aibu.”

Kesho yake tulikwenda kwa mganga mmoja kwa ajili ya kunyolewa na kuzinduliwa ambapo kazi hiyo ilituchukua mchana kutwa, tukawa tumetolewa nguvu za kichawi na tukawa watu wa kawaida.

Nimeamua kusimulia haya ili kuonesha kuwa, katika jamii tunayoishi nayo, wapo wabaya, wapo wema. Lakini katika yote, wabaya hawatakiwi kuwepo kwani ndiyo wanaoivuruga dunia yenye watu wazuri. Mimi sasa ni mtu safi na familia pia. Lakini ni baada ya kumpoteza mama mzazi. Najutia yote.       MWISHO.   

JIUNGE NA GLOBAL BREAKING NEWS!

globalbreakingnews.JPG


Loading...

Toa comment