The House of Favourite Newspapers

FANYENI HAYA MDUMISHE PENZI LENU

RAHA ya mapenzi ni wapendanao kupendana kwa dhati. Japo mara nyingi hutokea watu wanaoana ikiwa mmoja wao hampendi sana mwenzake lakini asikwambie mtu, unapoingia kwenye ndoa na mtu ambaye mnapendana kwa dhati maisha yenu huwa matamu zaidi.  Kila mmoja anainjoi kuwa na mwenzake. Anajivunia kumpata mwenzake, mnaishi kwenye dunia yenu ya kipekee na kila mmoja anampa thamani ya juu mwenzake. Penzi la dhati huwa linatengenezwa na mambo mengi ambayo wapendanao wanayaishi. Kumbukumbu nzuri huwa zinazinogesha zaidi penzi kuliko zile mbaya. Ni vyema zaidi kujitahidi kuweka kumbukumbu nzuri katika uhusiano wako maana zinaufanya uhusiano uwe mpya kila mnapozi-kumbuka.

Kumbukumbu mbaya huwa zinaondoa ladha ya mapenzi. Mathalan unamsaliti mwenzi wako, akagundua umefanya hivyo, mwenzi wako ataumia sana. Hawezi kusahau kirahisi. Wapendanao wanapaswa zaidi kutengeneza kumbukumbu nzuri kwenye maisha yao ya uhusiano kwani zinanogesha penzi. Kwa kuzingatia hilo, leo twende tukayaangazie mambo matano ambayo ukimfanyia mwenzi wako yanaweza kuweka kumbukumbu nzuri na kuufanya uhusiano wenu uzidi kuwa bora.

KUSAFIRI PAMOJA

Dunia ya sasa imejaa mahangaiko mengi. Watu wapo bize kutafuta fedha za kujikimu hivyo kujikuta hata wakishindwa kufanya jambo hili linalotengeneza kumbukumbu nzuri. Unaweza kutenga muda na mwenzi wako mkaenda hata kusalimia wazazi wa upande mmoja, kisha baadaye upande mwingine. Kama mnaona mnaweza hata kwenda nje ya nchi pamoja, mnaweza kufanya hivyo kwani kumbukumbu ya kusafiri huko mkiwa wawili, mkipeana kampani za hapa na pale huwafanya muikumbuke safari hiyo na inanogesha penzi pia.

MANUNUZI YA BIDHAA

Hili nalo ni muhimu. Siyo kila siku baba anajua tu kuacha hela za matumizi na mama anakwenda kununua mwenyewe gengeni, kununua mahitaji ya nyumbani pamoja kunaleta kumbukumbu nzuri ya penzi.

Kile kitendo cha wapendanao kushirikiana katika zoezi hilo mara mojamoja, linamfanya mwanamke ajione ana mlinzi mzuri pembeni yake na mwanaume pia kujiona kweli yeye ndiye mume. Tengeni muda wa kufanya manunuzi ya vitu pamoja. Siyo tu vitu vya jikoni, hata vitu vya watoto na mahitaji mengine ya familia.

KAZI ZA NYUMBANI

Kusaidiana baadhi ya majukumu ya nyumbani huwa pia kunakuza uhusiano mzuri kwa wapendanao. Mke na mume wanaposhirikiana kwa pamoja kufanya kazi za nyumbani, huweka kumbukumbu nzuri ya penzi lao.

ZAWADI

Hili pia ni la msingi sana. Tunaposema zawadi siyo lazima iwe kubwa, unaweza kumpa mwenzi wako zawadi ndogo tu lakini ikaweka kumbukumbu nzuri sana katika masuala ya uhusiano. Mathalan unaweza kumnunulia kiatu, gauni, saa au hata pafyumu itamfanya akukumbuke kila wakati anapokuwa amevaa au kutumia kitu husika.

KULEA PAMOJA

Kama wanandoa wamebahatika kuwa na watoto au pengine kuna watoto baki mnaowalea wa pande zote mbili, ni vizuri mkashirikiana katika kuwajali, kuwapa matunzo stahiki kwa pamoja.

Saidianeni kuwabeba watoto, muwalee pamoja siyo mmoja amuachie mwenzake jukumu hilo, mnapolifanya kwa pamoja jambo hilo huleta maana kubwa sana katika mapenzi yenu. Kwa leo inatosha, tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri. Unaweza kunifuata kwenye mitandao yangu ya kijamii, Instagram na Facebook natumia Erick Evarist, Twitter natumia ENangale.

Comments are closed.