The House of Favourite Newspapers

FATMA KARUME; MWANAMKE WA CHUMA

Tokeo la picha la fatma karume
Fatma Karume

UNA msemo wa Wahenga kutoka Magharibi mwa Tanzania mkoani Kigoma unasema; Mungu anatoa, hana choyo, usipomuomba pia anakuwa ghali. Kesho ni kubwa kwa kila aombaye.

Huu ni msemo wenye maana kubwa uliyokuwa unatumiwa na Wahenga kwenye suala zima la mafanikio, iwe ya kiimani, mali pamoja na vitu vingine. Kiuhalisia suala la kumuomba Mungu halikusimamia kwa kukaa ndani na kupiga magoti kusubiri akupe kile unachotaka, bali kupambana katika yale unayoyataka ili Mungu akufungulie njia na kuikata kiu ya moyo wako, kwa upande mwingine hili ndilo lengo la safu hii.

Nia ni kukuhamasisha msomaji kwa namna moja au nyingine kupambania ndoto zako bila kujali mazingira uliyonayo wakati huu. Ndiyo maana tunakuletea mifano ya watu mbalimbali ambao wamefanikiwa kwenye tasnia tofautitofauti na leo tunaye Wakili Fatma Amani Karuma.

FATMA KARUME NI NANI?

Huyu ni wakili maarufu kwa sasa Tanzania na ni Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) lakini pia Fatma ni mtoto mkubwa wa Rais wa Awamu ya Sita wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Amani Abeid Karume na ndugu zake wengine ni Abeid, Shuwana na Ahmed. Fatma ambaye amezaliwa Juni 15, 1969, visiwani Zanzibar, ni mjukuu wa Rais wa Awamu ya Kwanza wa Zanzbar, Sheikh Abeid Aman Karume. Kwa upande wa elimu yake ya masuala ya kisheria kwa kiasi kikubwa amesomea nchini Uingereza.

Wanaomfahamu vema Fatma Karume, wanachokiona kwake sasa hakiingii akilini vizuri wanasema wakati wa utawala wa baba yake, Amani Karume, alipokuwa Rais wa Zanzibar na kabla ya hapo, alikuwa mgumu kupatikana na asiyejichanganya na watu. Fatma Karume ametoka kwenye familia yenye uwezo kwani mjomba wake ni Mansour Yusuf Himid, alikuwa Waziri wa Nishati wa serikali ya visiwa hivyo na baba yake mdogo, Balozi Ali Karume alikuwa Balozi wa Tanzania katika nchi za Ulaya.Tokeo la picha la fatma karume

Fatma amekuwa akiandika katika magazeti ya Kiingereza, amekuwa akijulikana kwa makala kali hususan kukosoa mwenendo wa Serikali ya Zanzibar (SMZ) baada ya baba yake kuondoka madarakani. Fatma sasa anajichanganya na watu, hata wale wanaoitwa wa kawaida, kwa mfano hivi karibuni aliwahi kuja katika ofisi za gazeti hili Sinza Moro Dar na kuzungumza na waandishi wetu.

Umaarufu wake umepaa zaidi huku Bara hivi sasa kutokana na mambo mawili yanayofanana; mosi ni hatua yake ya kumtetea mwanasiasa machachari, Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Antipas Lissu katika kesi yake ya uchochezi dhidi ya Jamhuri na hatua ya yeye kufungua kesi dhidi ya Ofisa wa Jeshi la Polisi, Inspekta Eugene Mwampondela, kwa madai ya kumshika mwilini na kumzuia kutekeleza kazi zake. Wengi wanasema kutokana na ujasiri wake, Fatma anastahili kuitwa mwanamke wa chuma-Iron Lady.

NI NANI HASA FATMA KARUME?

Fatma Karume ndiye mtoto mkubwa wa Rais Mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume ambaye familia yake imejaliwa kupata watoto watano ambao ni Fatma pekee ndiye ambaye sasa anafahamika zaidi miongoni mwa watoto hao ambao wengi wamejiingiza katika biashara binafsi.

Fatma sasa anajulikana zaidi na anaonekana hivyo alivyo kwa sababu ya kazi zake za kisheria ambazo kimsingi ni za kuzungumza sana kama wanasiasa. Amefanya kazi kwa muda mrefu katika Kampuni ya IMMA Advocates iliyopo Dar es Salaam na kutegemewa katika kusimamia masuala ya mashitaka mahakamani.Tokeo la picha la fatma karume

Vyovyote vile itakavyokuwa, ni wazi Fatma Karume ameingia katika hatua mpya ya maisha yake ambako sasa si binti mfalme tena bali ni wakili shupavu na alama ya mapambano dhidi ya wapinzani wa utawala wa sheria. Ikumbukwe kwamba katika historia ya nchi hii hajawahi kupatikana mwanasheria mwanamke machachari mwenye ujasiri kama Fatma, kumbuka amekuwa mstari wa mbele kupigania haki za watu bila kujali itikadi.

Mbali na Fatma kuwafundisha wanawake kutokuwa waoga katika kupigania haki zao, katika hali chanya ukiyasoma maisha yake unaona kabisa ili kufanya maisha yako kuwa na maana ni lazima usimamie kile unachokiamini ili kutimiza ndoto yako.

Makala: Boniphace Ngumije

Comments are closed.