The House of Favourite Newspapers

FBI Wakamata Boti ya Kifahari ya Mshirika wa Putin, Waongeza Presha kwa Urusi

0
Boti ya kifahari yenye urefu wa takribani futi 254, imekamatwa katika Mji wa Bandari wa Palma de Mallorca nchini Hispania

SHIRIKA la Ujasusi la Marekani (FBI) kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi na mamlaka nyingine nchini Hispania, wameikamata na kuishikilia boti ya kifahari iliyopewa jina la Tango inayomilikiwa na Viktor Vekselberg anayetajwa kuwa mshirika wa karibu wa Rais Vladimir Putin wa Urusi.

Kukamatwa kwa boti hiyo inayokadiriwa kuwa na thamani ya dola milioni 90 za Kimarekani, ni mwendelezo wa vikwazo vilivyowekwa kwa washirika wa karibu wa Rais Putin na nchi za Ulaya na Marekani kutokana na uvamizi na maafa makubwa yanayoendelea kufanywa na majeshi ya Urusi nchini Ukraine.

Vekselberg anayetajwa kuwa swahiba wa karibu wa Putin, alizaliwa nchini Ukraine na inaelezwa kwamba amepata utajiri mkubwa kutokana na biashara ya mafuta na aluminium.

Boti hiyo kubwa na ya kifahari, yenye urefu wa takribani futi 254, imekamatwa katika Mji wa Bandari wa Palma de Mallorca nchini Hispania na inaelezwa kuwa imekamatwa ikiwa inapeperusha bendera ya Kisiwa cha Cook cha Hispania.

                Boti hii inakadiriwa kuwa na thamani ya dola milioni 90 za Kimarekani

Boti hiyo imekamatwa Jumatatu ya April 4, 2022 ikiwa imetia nanga katika mji huo wa bandari, unaotajwa kuwa kivutio kikubwa cha wafanyabiashara wakubwa duniani kutokana na unafuu mkubwa wa kodi.

Inaelezwa kwamba FBI wameshirikiana na Homeland Security Investigations pamoja na Polisi wa Hispania ikiwa ni utekelezaji wa maombi ya serikali ya Marekani ambayo imeendelea kusisitiza kwamba Putin na washirika wake wanapaswa kuendelea kuwekewa vikwazo vikali kutokana na mauaji ya raia wasio na hatia yanayofanywa na majeshi ya Urusi nchini Ukraine.

Kukamatwa kwa boti hiyo ya kifahari kunatajwa kuwa hatua kubwa ya kwanza ya utekelezaji wa amri ya serikali ya Marekani kukamata na kuzuia mali za washirika wa karibu wa Rais Putin kama hatua ya kumshinikiza kiongozi huo kusitisha uvamizi wake nchini Ukraine.

Hatua hiyo imekuja saa chache baada ya kuanza kusambaa kwa picha na video za mauaji makubwa ya raia wa Mji wa Bucha uliopo nje kidogo ya Mji Mkuu wa Kyiv ambapo maiti kadhaa za raia zimeonekana zikiwa zimetapakaa mitaani, nyingine zikiwa zimefungwa mikono na kupigwa risasi.

                       Boti ya kifahari iliyopewa jina la Tango inayomilikiwa na Viktor Vekselberg

Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky ameyaita mauaji hayo ya Bucha kuwa ni mauaji ya halaiki yanayotekelezwa na majeshi ya Rais Putin nchini Ukraine ambapo ameyaomba mataifa yanayoiunga mkono Ukraine, kuongeza vikwazo dhidi ya Putin, serikali yake na washirika wake.

Kufuatia mauaji ya Bucha, Rais Joe Biden wa Marekani ameahidi kuendelea kuweka vikwazo vikali dhidi ya utawala wa Moscow na washirika wake na kurudia kauli yake kwamba Rais Putin anafanya makosa ya uhalifu wa kivita kwa kusababisha mauaji ya halaiki.

Leave A Reply