The House of Favourite Newspapers

Fedha za Majini Zilivyoniendesha Puta 05

0

ILIPOISHIA

Baada ya kutopata jibu nilitoka mle chumbani nikaingia katika chumba cha marehemu baba yangu. Nilichutama chini ya kitanda nikatia mkono na kutoa ule mkoba ambao niliuona mvunguni.
Niliutoa na kuona ulikuwa umejaa vumbi. Nikaukung’uta kisha nikaketi kitandani na kuufungua.

SASA ENDELEA
Ndani ya mkoba huo, niliona kitabu kidogo kilichokuwa na maandishi ya Kiarabu. Nilikuta pete ya fedha ambayo baba yangu alikuwa akipenda kuivaa. Ilikuwa na kito cha rangi ya bahari kilichowekwa alama ya nyota na mwezi.

Pia nilikuta chupa ambayo ndani yake mlikuwa na yai zima lililoandikwa maandishi ya Kiarabu kwa wino mwekundu. Pia mlikuwa na talasimu iliyokuwa na picha ya mtu. Sikuweza kujua lile yai liliingia vipi ndani ya ile chupa wakati mdomo wa chupa ulikuwa na uwazi mdogo sana.
Mbali ya ile chupa kulikuwa na kipande cha ubao mweusi uliokuwa na maandishi ambayo sikuweza kutambua yalikuwa ya lugha gani, Kigiriki si Kigiriki, Kichina si Kichina! Pia kulikuwa na vikorokoro vingine ambavyo sikuweza kuvielewa. Vitu hivyo kwa kweli vilinishangaza.
Baada ya kuviangalia kwa dakika kadhaa nilivirudisha ndani ya ule mkoba.
Nilichukulia kwamba wazee wa zamani walikuwa na vikorokoro vingi vya kiasili walivyokuwa wanavihifadhi kwa imani mbalimbali. Na kwa kweli nisingeweza kujua baba yangu alikuwa amehifadhi vitu vile kwa sababu gani.

Nikaamua kuurudisha ule mkoba mvunguni nilikoutoa. Mkoba huo haukushughulisha sana akili yangu. Akili yangu ilikuwa imeshughulishwa zaidi na zile pesa. Nilipotoka pale chumbani nilitaka kurudi tena chumbani mwangu nizitazame tena zile pesa kwenye lile sanduku la chuma lakini nikajizuia. Niliona kama nilikuwa ninafanya jambo la kitoto.
Kwa vile sikuwa na kazi nyingine ya kufanya nikaamua kukaa barazani mwa ile nyumba yetu na kupanga mambo yangu. Jambo la kwanza nililolipanga ni jinsi ya kuondoka na zile pesa kwenda nazo Dar.
Utata ulikuwa ni namna nitakavyoweza kusafiri kwenye basi nikiwa na sanduku hilo zito bila watu kujua kama lilikuwa na kiasi kingi cha pesa.

Nilijiambia kwa vyovyote vile lazima ningetiliwa mashaka na abiria wenzangu na kama sanduku hilo litafikishwa polisi na kufunguliwa, polisi wangeshuku kuwa nilikuwa jambazi kwani wasingeamini kuwa pesa zile nimezirithi kutoka kwa baba yangu.
Nikazidi kujiambia kuwa hata kama nitafika Dar na pesa hizo, nisingeweza kuzihifadhi benki kwani nisingeweza kujieleza nimezipata wapi. Mwisho wake ningeangukia mikononi mwa polisi na kutakiwa nijieleze vizuri.
Usiku ulipowadia nilikwenda kula kwa mama lishe kwa vile nyumbani nilibaki peke yangu. Baada ya kula chakula nikarudi nyumbani kulala.
Hata huo usingizi wenyewe haukunijia. Nilikuwa nikiwaza zile pesa tu. Nakumbuka nilitazama saa yangu na kuona ilikuwa saa nane usiku nikatoka uani kujisaidia kisha nikarudi kulala. Safari hii nilipofumba macho yangu tu usingizi ukanichukua hapo hapo.
Vile napata usingizi tu ikanijia ndoto ya ajabu. Nilimuota mwanamke mmoja wa Kiarabu amekaa kwenye kiti kilichokuwa mle chumbani.
Alikuwa mzuri sana. Mavazi yake ndiyo yaliyonishitua. Alikuwa amevaa shuka nyeupe tupu huku miguu yake ikiwa pekupeku. Kichwani alikuwa amejifunga kilemba cha rangi nyekundu.
Wakati namtazama huku nikijiuliza mwanamke yule ametokea wapi, aliniuliza.
“Unanijua mimi?”
“Sikujui,” nikamjibu.
“Mimi ndiye niliyekuwa mke wa baba yako. Mimi ni mwanamke wa kijini. Jina langu ni Maimuna. Kwetu ni Kisima cha Giningi Zanzibar. Baba yako alifika mahali hapo kutafuta fedha za majini. Akakutana na baba yetu aliyekuwa akitufuga, mzee Habibu Sultani wakakubaliana kwamba ili baba yako apate fedha za majini aozeshwe mke wa kijini miongoni mwa majini wanaokalia mali.”
Mwanamke huyo akaendelea kuniambia.
“Mzee Sultani akaniozesha mimi kwa baba yako baada ya baba yako kukubaliana na masharti yetu. Masharti yetu yalikuwa kwa kunioa mimi yeye atapata fedha za majini na atakuwa tajiri lakini lazima amtoe kafara mke wake aliyekuwa naye awe dondocha. Na baada ya miaka kumi amtoe kafara mtoto wake au mjukuu wake naye pia awe dondocha.”
Wakati nikielezwa hayo nilikuwa nimeduwaa nikimsikiliza mwanamke huyo ambaye aliendelea kunieleza.
“Sharti letu jingine lilikuwa lazima amtaje mrithi wake ili nimjue mapema. Baba yako akakutaja wewe na ndiyo sababu alipokaribia kufa alikwambia urithi wako uko mvunguni mwa kitanda.
“Zile pesa zilizomo kwenye lile sanduku ni pesa zangu. Kila siku zinaongezeka. Zile haziishi, utatumia mpaka unakufa. Baada ya baba yako kutimiza masharti yetu nilianza kumuingizia zile pesa kwenye sanduku mpaka hivi sasa limejaa. Alimfanya mke wake dondocha na juzi juzi tu alimfanya dondocha mjukuu wake, yaani mtoto wako.”
“Ninavyojua mimi ni kuwa mama yangu alikufa na mwanangu pia alikufa mwenyewe,” nikamwambia mwanamke huyo.
“Hivyo ndivyo ilivyoonekana kuwa watu hao wamekufa lakini hawakufa, wako hai. Ni kama vile wamechukuliwa msukule. Mama yako na mwanao wako kule kwenye pango ambako baba yako alitaka kukupeleka siku ile usiku lakini akafikwa na umauti.
Itaendelea wiki ijayo

Leave A Reply