The House of Favourite Newspapers

Fedha za Majini Zilivyoniendesha Puta-10

1

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:

“Nani abishaye?”
“Mimi mganga. Tafadhali nifungulie,” sauti ya yule mganga ikasikika huko nje.

SASA ENDELEA MWENYEWE…

Nilijiuliza mbona mganga huyo amenifuata usiku huo wakati tulipatana tukutane asubuhi? Na pia nilibaini kuwa, mganga hakuwa peke yake pale nje. Kulikoni sasa mpaka akaja na watu wengine?

Nikaenda kufungua mlango huku nikiwa na alama ya kuuliza usoni kwangu.
Hapo nje nilikuta watu wanne. Wawili walikuwa wamemshikilia yule mganga kama wakitaka asianguke. Mmoja alibeba lile sanduku la pesa. Na wa nne alikuwa ameshika ule mkoba wa ngozi niliokuwa nimempa yule mganga.
“Karibuni,” nilisema huku uso wangu ukionesha mshangao mkubwa.

“Tulikubaliana nije asubuhi lakini nimelazimika kuja usiku huu,” mganga aliniambia.
Jinsi sauti yake ilivyokuwa dhaifu nilitambua kuwa kulikuwa na jambo ambalo halikuwa la kawaida.
Mganga huyo aliendelea kuniambia:
“Nimekurudishia hili sanduku lako la pesa pamoja na mkoba ulionipa. Sivitaki tena, chukua mwenyewe.”
Mganga huyo akamuamuru yule mtu aliyebeba lile sanduku anipe.
“Mwenye sanduku hilo ni huyo bwana mpe mwenyewe sanduku lake tuondoke,” mganga alimwambia.

“Kwani vipi?” niliuliza baada ya kuona mambo siyaelewi. Tulikubaliana na  mganga huyo vingine, sasa naona mambo yamekuwa mengine.
Yule mtu aliyebeba sanduku aliliweka mbele ya kizingiti cha mlango wangu.
“Bwana sanduku lako ni hilo,” aliniambia yule aliyelibeba.

“Kwani vipi?” nilimuuliza yeye sasa na kuachana na mganga.
“Huyu bwana kidogo tu afe kwa sababu ya hili sanduku lako,” yule mbebaji aliniambia huku akiniangalia kwa macho ya ujasiri.
“Kwa sababu gani?” nilimuuliza.
“Havisemeki ndugu yangu, ni hatari tupu. Huyu mganga ni rafiki yangu na tunaishi nyumba moja. Tulikuwa tumelala tukasikia anapiga kelele chumbani mwake. Ilibidi tuvunje mlango wa chumba chake tukamkuta yuko hoi, mwili wake wote umejaa alama za kutandikwa bakora. Akikuonesha mgongo wake unaweza kulia,” alisema.
“Una maana alikuwa akitandikwa bakora?” nilimuuliza japokuwa nilimwelewa.

“Sisi tulimuuliza una nini akatuambia kuna mwanamke mmoja wa kijini aliyeingia chumbani mwake kimiujiza na kuanza kumtandika bakora, ndiyo sababu alikuwa anapiga kelele.”
“Huyo mwanamke alikuwa anampiga bakora kwa sababu gani?” nilimuuliza.
“Kwanza tulimuuliza huyo jini ni katika majini yake ya uganga, akatuambia si katika majini yake bali ni jini wa mtu mmoja ambaye alirithi pesa za majini kutoka kwa baba yake. Akatuambia kuwa aliyerithi hizo pesa alikuwa hazitaki na alifika kwake kumueleza hivyo.

“Yeye huyu mganga akaona achukue hizo pesa lakini jini anayehusika na pesa hizo hakukubaliana na jambo hilo na ndiye aliyemfuata usiku na kumtandika bakora huku akimwambia alirudishe hili sanduku la pesa alikolichukua.”
Nilihisi moyo wangu ukianza kwenda mbio zaidi ya kawaida. Hiyo habari ilikuwa imenitisha. Kama mganga mwenyewe aliyejitumainisha ametandikwa bakora na kuamua kulirudisha sanduku, ningepata wapi msaada mwingine mimi?
Yule mtu aliyebeba sanduku akaendelea kusema: “Sasa kwa vile tulimkuta yuko taabani akatuambia tumsindikize kwako akurudishie sanduku lako. Sisi tulipoingia mle chumbani mwake yule jini alikuwa ameshaondoka lakini alimwambia huyu mganga kama hatalirudisha hili sanduku na akaamua kulala nalo atarudi tena amtandike bakora hadi asubuhi.”
Yule mtu mwingine aliyekuwa ameshika ule mkoba naye aliuweka juu ya sanduku hilo.

Huku nikiwa nimetaharuki kutokana na kushtushwa na habari ile, nilimtazama yule mganga. Kweli alionesha alikuwa taabani  kwani alishikiliwa na watu wawili kama mgonjwa.

“Lakini wewe uliniambia hii kazi ungeimudu,” nilimwambia yule mganga.
“Kwa kifupi mimi nimeshashindwa. Dhoruba niliyoipata usiku huu si ndogo. Wewe chukua hizo pesa zako, tafuta mganga mwingine,” mganga aliniambia na kuwaambia wale watu aliokuja nao warudi nyumbani.
Jambo la ajabu nililoliona hapo ni kwamba, mara tu baada ya kunirudishia lile sanduku, mganga huyo alipata nguvu na akawaambia wale watu waliomshikilia wamuache.

“Nitarudi mwenyewe kwa miguu yangu, naona nimepata nguvu sasa,” alisema mganga.
Waliondoka na kuniacha nimeshangaa. Kusema kweli kuliingiza ndani lile sanduku niliogopa lakini pia kuliacha nje isingewezekana.

Hapo mwanzo sikuweza kujua kama sanduku hilo lilikuwa na matatizo makubwa kiasi hicho. Nilidhani kwa vile nililikabidhi kwa mganga, matatizo yangekwisha. Kumbe haikuwa hivyo.
Mganga niliyemtegemea aliniambia nitafute mganga mwingine, nitampata wapi mganga huyo? Nikajiuliza huku nikilitazama lile sanduku.

Sikutaka hata kulifungua nilitazame ndani. Wazo likanijia kuwa, niende nikalitupe lakini wazo hilo sikuafikiana nalo kwani wenye pesa hizo, yaani majini wangeweza kunifuata. Kama waliweza kumtandika mganga, wasingeshindwa kunitandika na mimi.
Itaendelea wiki ijayo

SOCIAL MEDIA ZETU:

KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA

INSTAGRAM: @Globalpublishers

TWITTER: @GlobalHabari

FACEBOOK: @GlobalPublishers

SUBSCRIBE YOU TUBE: GlobalPublishers

GLOBAL TV ONLINE: www.globaltvtz.com

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, ERIC SHIGONGO FACEBOOK PAGE: @shigongotz

1 Comment
  1. neema mikey says

    duh! hatar sana

Leave A Reply