Fedha za Majini Zilivyoniendesha Puta

ILIPOISHIA

Kumekuwa na madai ya kuwepo kwa fedha za majini.Nimeshawahi kuoneshwa watu kadhaa na kuambiwa kuwa watu hao wametajirika kutokana na fedha za majini. Lakini nilikuwa sielewi fedha hizo za majini hupatikanaje au hupatikana wapi.

Kadhalika sikuweza kuelewa kunakuwa na mkataba gani kati ya majini hao na watu wanaopewa fedha hizo.

Kwa vile sikuweza kupata mtu yeyote wa kunielimisha juu ya upatikanaji wa fedha hizo na kujibu maswali yangu, nilikuwa siamini kama kuna pesa za majini.
Siku zote nilikuwa nikijiambia kuwa madai ya kuwepo kwa fedha za majini ni imani tu ya baadhi ya watu isiyo na ukweli wowote.

Lakini siku moja pesa hizo zilinijia kama ndoto. Ilikuwa ni kama kuoneshwa kuwa pesa hizo zipo. Ni pesa nyingi ambazo ningeweza kutumia hadi kufa kwangu.

Ilikuwa ni raha sana kuzimiliki lakini nilikiona cha moto. Hizo si pesa za kushughulika kuzitafuta. Bora uishi maskini na ufe maskini kuliko fedha za majini.

Je, nilizipataje fedha hizo na nini kilinitokea hadi nikasema bora nife maskini? Ungana nami tena katika mkasa huu wa kutatanisha.

SASA ENDELEA…
Naitwa Shafii Adam ni mzaliwa wa Manundu Korogwe, Mkoa wa Tanga.

Nilisoma Korogwe na niliajiriwa kazi na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) nikiwa hapohapo Korogwe.
Nina miaka tisa tangu nilipopata ajira hii katika jeshi la wananchi. Kituo changu cha kwanza cha kazi kilikuwa Dodoma. Baada ya kufanya kazi kwa miaka miwili kama mwanajeshi mpiganaji nikahamishiwa Dar es Salaam ambako ninaendelea kufanya kazi hadi hivi sasa.
Nilipokuwa Dodoma nilifanikiwa kufunga ndoa na msichana aliyeitwa Sikuzani na tulifanikiwa kupata mtoto mmoja wa kiume tuliyempa jina la Abdul.

Mama yangu alikuwa amefariki dunia tangu nilipokuwa ninasoma. Nikalelewa na baba yangu hadi nilipomaliza masomo ya shule. Baba yangu alikuwa mkulima, tena mkulima mdogo tu wa kutumia jembe la mkono ingawa shamba lake lilikuwa kubwa. Msimu wa kupanda unapowadia alikuwa akiajiri vibarua waliokuwa wakimlimia shamba lake.

Aliwahi kufungua duka la chakula kisha akalifunga. Pia aliwahi kununua gari. Baada ya kulitumia kwa miaka miwili akaamua kuliuza.
Siku moja nilimuuliza baba kwa nini alifunga lile duka, akanijibu kuwa wachawi wakiona ana mali watamuandama sana.
“Na kwa nini umeuza gari ambalo lilikuwa linatufaa?” Nikamuuliza tena.

“Nimeliuza kukwepa fitina za watu.” Hilo ndilo jibu alilonipa.
Wakati nimeshaanza kazi mzee wangu alinionesha mfano wa wazee wanaojitegemea na siyo tegemezi kama baadhi ya wazee wengine. Nakumbuka hakuwahi kutaka pesa yangu hata siku moja.
Kulikuwa na kipindi nilikuwa nikimtumia pesa bila yeye kuniomba. Siku ya likizo nilipokwenda nyumbani, alinisubiri siku ile naondoka kurudi Dar, akanirudishia pesa zangu zote nilizokuwa nikimtumia. Nikashangaa sana.
“Mwanangu usishughulike na mimi, shughulikia familia yako. Mimi sitaki fadhila yako. Nimekulea kama mwanangu na ilikuwa ni wajibu wangu kwa sababu hata mimi nililelewa hivyohivyo,” akaniambia.

Nikaona huyu baba yangu alikuwa mtu wa ajabu sana. Mtu mwenyewe alikuwa maskini lakini alikuwa maskini jeuri. Hakupenda kujiachia na kuwa legelege.
Kila nilipopata likizo nilikuwa ninarudi nyumbani kukaa na baba yangu ambaye kwa wakati ule alikuwa ameshaanza kuchoka. Likizo zetu za jeshi ni za miezi mitatu. Unakaa mpaka unajisahau.
Lakini unapata likizo ya miezi mitatu baada ya kufanya kazi kwa miaka mitatu bila likizo.

Siku chache kabla ya kupata likizo yangu ya tatu, mke wangu ambaye alikuwa mama wa nyumbani alipata taarifa kuwa baba yake alikuwa akiumwa sana huko kijijini kwao nje ya mji wa Dodoma.
Ikabidi aende kumjulia hali baba yake kwa vile alikuwa hajafika kwao kwa kipindi cha miaka mitatu. Alipoondoka aliniachia mtoto wetu Abdul ambaye wakati huo alikuwa anasoma shule ya msingi. Alikuwa darasa la tatu.

Zilikuwa zimebaki siku chache shule zingefungwa kwa likizo ya mwaka. Hivyo nilikuwa nikisubiri apate likizo ambayo haikupishana sana na likizo yangu, twende Manundu, Korogwe.
Kwa bahati njema mke wangu alipofika kwao alinipigia simu akanijulisha kuwa hali ya baba yake ilikuwa inaendelea vizuri na mimi nikamjulisha kuwa nitakapopata likizo nitakwenda Manundu, Korogwe pamoja na Abdul kwa vile likizo hizo hazitapishana sana.
Mimi ndiye niliyetangulia kuchukua likizo yangu. Baada ya wiki moja Abdul naye akapata likizo shuleni, tukafunga safari kwenda Manundu, Korogwe.

Tulipofika tu Korogwe Abdul alianza kuumwa na kichwa. Kichwa kilimuanza saa tisa tulipofika Korogwe, hadi kufika saa moja usiku Abdul akafariki dunia!
Baba yangu alishangazwa sana na tukio lile, akaniuliza kama Abdul alikuwa anaumwa tangu tulipokuwa Dar.
“Abdul alikuwa mzima kabisa. Kichwa kilimuanza tulipofika hapa Korogwe stendi,” nikamwambia.
Baba akabaki kutikisa kichwa kusikitika.
Usiku uleule baba alianza kutoa taarifa kwa ndugu, jamaa na majirani zake kuhusu kifo cha mwanangu kilichotokea ghafla. Wakati huohuo na mimi nilimpigia simu mke wangu kumjulisha kuhusu kifo hicho.

Mke wangu alishituka na kung’aka.
“Unasemaje baba Abdul?”
“Nimekwambia Abdul amefariki dunia sasa hivi.”
“Una maanisha Abdul huyu mtoto wetu?”
“Ndiyo yeye.”
“Hah! Mbona kama siamini. Alipatwa na nini?”
“Tulipofika hapa Korogwe alianza kuumwa kichwa. Mpaka inafika saa moja usiku akafariki dunia.”
Je, nini kitaendelea? Fuatilia hapahapa Jumanne ijayo.

Loading...

Toa comment