The House of Favourite Newspapers

Fedha za Usajili Zaivuruga Yanga SC

0

Wilbert Molandi, Championi Jumatano, Habari

SIKU chache baada ya timu ya Yanga kubeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa mara ya tatu mfululizo, kuna uwezekano mkubwa timu hiyo msimu ujao isiutetee ubingwa wake. Hali hiyo inatokana na kile kinachodaiwa kuwa klabu hiyo kwa sasa haina fedha za kutosha kwa ajili ya usajili lakini pia inajipanga kutumia bajeti kidogo kwa ajili ya zoezi hilo kuliko misimu yote iliyopita.

Habari za kuaminika kutoka ndani ya Yanga ambazo gazeti hili limezipata, zimedai kuwa hali hiyo inawavuruga vichwa viongozi wa klabu hiyo ikizingatiwa nusu ya wachezaji wa kutumainiwa wa timu hiyo mikataba yao imefikia ukingoni na ili wabakie wanahitaji fedha za usajili. “Kusema kweli bado hatujaanza harakati zozote za usajili kwani bado tunapambana kuhakikisha tunapata fedha kwa ajili ya zoezi hilo.

“Bajeti yetu mpaka sasa haijakaa sawa na ukizingatia safari hii tuna kazi kubwa ya kufanya, tusipokuwa makini msimu ujao tutakuwa na kikosi kibovu, hii ni kutokana karibia nusu ya wachezaji wetu wa kikosi cha kwanza mikataba yao inamalizika na ili tuweze kuwabakiza, fedha zinahitajika.

“Kwa hiyo kutokana na hali hiyo ndiyo maana hatujaanza usajili kama ilivyo kwa timu nyingine ila kuna baadhi ya wachezaji tumeshafanya nao mazungumzo ya awali ya kuwaambia nia yetu ya kutaka kuendelea nao na wengine kutoka nje ya kutaka kuwasajili,” kilisema chanzo hicho cha habari.

Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Mkwasa alipotafutwa ili aweze kuzungumzia suala hilo hakuwa tayari kuzungumza chochote: “ Siwezi kusema chochote kuhusiana na hilo ila ni lazima tutasajili kwa ajili ya kukiimarisha kikosi chetu na sasa tunaendelea kujipanga kwa ajili ya zoezi hilo.”

Katika msimu wa 2015/16, Yanga ilitumia zaidi ya Sh milioni 800 kwa ajili ya zoezi hilo ambapo baadhi ya wachezaji waliochukua fedha nyingi katika usajili huo ni Haruna Niyonzima, Donald Ngoma, Vincent Bossou, Thabani Kamusoko na Amissi Tambwe ambapo usajili wao kwa pamoja uligharimu klabu hiyo zaidi ya Sh milioni 400. Hata hivyo, wachezaji hao kwa pamoja mikataba yao ya kuendelea kuitumikia Yanga tayari imeishamalizika.

Yanga inapitia katika kipindi cha ukata, tangu aliyekuwa mwenyekiti wake, Yusuf Manji apate matatizo binafsi, na hali imekuwa mbaya zaidi baada ya hivi karibuni kutangaza kuachia ngazi. Pamoja na kupata fedha kutoka kwa wadhamini, bajeti ya Yanga inaonekana kuwa kubwa kuliko udhamini ilionao. Manji ndiye alikuwa anafadhili usajili na mambo yote yahusuyo fedha klabuni hapo.

Leave A Reply