Fei Toto Achimba Mkwara Mzito Ligi Kuu
BAADA ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Simba, Jumamosi, kiungo mshambuliaji wa Yanga, Feisal Salum ‘Fei Toto’, amefunguka kuwa sasa moto wao hauzimiki na wamepanga kufanya vizuri katika kila mchezo ulio mbele yao.
Yanga Jumamosi ilifanikiwa kushinda taji la Ngao ya Jamii baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Simba, ambapo sasa Yanga wameandika rekodi ya kutwaa taji hilo mara sita.
Fei Toto, alikuwa miongoni mwa nyota walioonyesha kiwango kikubwa katika mchezo huo ambapo alifanikiwa kupiga pasi 42, ambazo zilifika kwa walengwa.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Fei Toto alisema: “Kwanza kabisa tunawashukuru mashabiki wetu kwa sapoti yao na kujitokeza kwa wingi katika michezo yetu hata inapotokea tunapata matokeo mabaya.
“Ni jambo zuri kuona Jumamosi tumewapa furaha na tunawaahidi msimu huu kujituma kwa kila mchezo unaokuja kuhakikisha tunapata matokeo mazuri,” alisema Fei Toto ambaye kuanzia msimu uliopita amekuwa bora.
MARIA RAYMOND, Dar es Salaam