The House of Favourite Newspapers

Ferooz: Benchi Imenifundisha Mengi

0

????????????????????????????????????Ferooz

Makala: Gabriel Ng’osha

UNAPOMTAJA Feruzi Mrisho maarufu kama Ferooz, unamzungumzia msanii ambaye miaka kumiiliyopita, usingeweza kupata nafasi kirahisi ya kumfikia pale alipokaa. Akiwa na uwezo mkubwa wa kuimba, kijana huyu ndiye aliyelibeba Kundi la Daz Nundaz, enzi hizo likitikisa kila kona.

Amefanya kazi nyingi zinazoendelea kupendwa na wakati f’lani kumshirikisha Ferooz katika wimbo, ilikuwa ni tiketi ya ‘kuubust’ kabla hata haujatoka.

Ukiachana na nyimbo alizoimba na Daz Nundaz, kama Kamanda na Barua, lakini alipata kukaa kileleni baada ya ngoma yake iliyoitwa Starehe, akiwa amemshirikisha Profesa Jay.

Ni combination nyingine tena na rapa huyo mkongwe, ambaye sasa ni Mbunge wa Jimbo la Mikumi (Chadema), Ferooz aliibuka na kuwa gumzo katika kibao alichoshirikishwa na Jay kilichoitwa Nikusaidieje?

???????????????????????????????Lakini katika hali ya kusikitisha, Ferooz akapotea ghafla na kuanza kuzusha maswali mengi yaliyokosa majibu, baadhi wakidai mshkaji anabwia unga. Tetesi hizo zilitiwa nguvu zaidi baada ya mmoja wa wasanii waliokuwa nguzo katika kundi lao la Daz Nundaz, Daz Baba, kuonekana kuhusishwa na madawa ya kulevya.

Lakini hivi karibuni mkongwe huyo ameibuka na kibao chake kipya kinachokwenda kwa jina la Nimejifunza, sasa akiwa chini ya uangalizi wa Meneja wa Kundi la TMK Wanaume Family, Said Fella ‘Mkubwa’.

Risasi Vibes ilimtafuta na kufanya naye mahojiano kama yanavyosomeka hapo chini.

KWA KIPINDI ULICHOKUWA NJE YA GAME, UMEJIFUNZA NINI?

Nimejifunza vitu vingi sana, kwani unapokuwa umekalia benchi utawajua wabaya na wazuri.

UNAMANISHA NINI?

Nilipokuwa nimefulia, washkaji na hata ndugu walinitenga na kuna kipindi nikahisi kama niko peke yangu.

UNADHANI NI KWA NINI?

Bila shaka ni kutokana na ukimya wangu, kwani sikuwa napiga shoo zozote zile, hivyo hata pesa sikuwa naingiza.

NINI KILICHANGIA WEWE KUKAA KIMYA?

Ni mzunguko tu wa maisha yetu ya Kibongo na mfumo wetu wa maisha ya sanaa.

KUNA TETESI ZA GANJA NA UNGA KUKUPOTEZA UNAJITETEAJE?

Si kweli, kwani bangi niliacha kuvuta kitambo sana, ila unga sijawahi kutumia kabisa zaidi ya uzushi na hasa baada ya kupotea.

BAADA YA KUFULIA MAISHA

YALIKUWAJE?

Ni lazima utayumba kwa kiasi f’lani, maana mishe zote zinakuwa zimesimama.

UMEJIPANGAJE KURUDI KWENYE GEMU?

Namshukuru Mungu, Said Fella amejitolea kunisimamia kwa kuwa jamaa ana uzoefu naamini nitasimama tena.

NI KWELI MALI ZAKO ZOTE ULIZITEKETEZA?

Si kweli, nilichouza ni lile gari aina ya Jeep lakini vingine vipo sema siwezi kutaja kila kitu.

NI KWELI ULIPELEKWA POLISI KWA DHULUMA?

Hapana, nilipata kesi kwenye nyumba ya Palestina, Sinza ambapo kuna mpangaji nilimpangisha, akazingua, nilipotaka kumbadilisha ndipo hapo msala ulipoanzia, ila nilimalizana nao.

KWA SASA UNAFANYA NINI?

Nimekuja na wimbo wangu mpya unaitwa Nimejifunza na ndani ya wimbo huo nimezungumzia sehemu kubwa ya misukosuko niliyoipata baada ya kukaa kimya.

UNAWAAHIDI NINI MASHABIKI WAKO?

Naomba wanipe sapoti kama mwanzo, Ferooz ana kipaji anaweza kufanya ngoma za ukweli hivyo nawategemea waniunge mkono sana, na kwa sasa wimbo wangu wa Nimejifunza uko hewani kwenye vituo mbalimbali vya redio na hata video inategemea kutoa hivi karibuni.

RISASI VIBES INAKUTAKIA KILA LAKHERI

Nashukuru, naomba sapoti yenu pia.

Leave A Reply